Licha ya changamoto, wadau wausifu mfumo mpya ununuzi wa pamba

Thursday July 12 2018

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Pamba si tu ni zao la biashara bali la kimkakati kwa mikoa 17 inakolimwa hasa Kanda ya Ziwa ambayo ni wazalishaji wakuu.

Mnyororo wa thamani wa pamba unaojumuisha wakulima, wauza pembejeo, wanunuzi, wamiliki wa viwanda vya kuchambua, viwanda vya nguo na bidhaa, na biashara zingine zinazohusiana na sekta hiyo umeajiri zaidi ya watu milioni19.

Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga anasema tofauti na utaratibu wa misimu iliyopita zao hilo liliponunuliwa na kampuni binafsi, msimu huu ununuzi utafanywa na Vyama vya Msingi vya Ushirika (Amcos).

Mabadiliko hayo yamefanywa wakati ambao uzalishaji unatarajiwa kutoka tani 132, 928 zilizovunwa msimu wa 2017/18 hadi tani 600, 000 msimu huu, 2018/19.

Katika utekelezaji wa mpango huu mpya, kampuni binafsi zinazotaka kununua pamba zitaingia mkataba na Amcos ambazo zitanunua pamba kwa ada ya Sh33 kwa kila kilo.

Makato hayo, zitatumika kufanya malipo kwa maofisa na makarani wa ununuzi na zitakuwa mtaji wa kujenga na kuviimarisha vyama vya ushirika ambavyo vingi vilishakufa kutokana na ubadhirifu pamoja n auongozi mbaya.

Kutokana na mfumo wa ununuzi kupitia ushirika, yapo mafanikio na changamoto kadhaa zilizoshuhudiwa tangu msimu ulipozinduliwa na Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba katika Kijiji cha Bukama wilayani Igunga. Uzinduzi ulifanyika Mei Mosi.

Mafanikio

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole anasema mfumo mpya umerahisisha utaratibu na usimamizi wa ununuzi tofauti na kulipokuwa na soko huria ambapo kila kampuni ilijipangia ipendavyo.

“Ubora wa pamba inayonunuliwa pia umeongezeka kwa sababu wakulima wanaelimishwa kuchambua vema kabla ya kuuza. wanaopeleka pamba chafu hurejeshewa wakaichambue upya,” anasema Kipole.

Wakulima wanasema mfumo mpya umewahakikishia malipo ya fedha taslimu tofauti na awali walipokuwa wanakopwa na kampuni binafsi.

Katibu wa chama cha msingi Kalebezo kilichopo wialani Buchosa, Mary Musa anasema kituo cha ununuzi kijijini hapo kupokea fedha za kuwalipa wakulima kila siku.

Msimu huu wa mavuno, anasema zaidi ya kilo 100,000 zinatarajiwa kununuliwa kituoni hapo.

Kaimu ofisa kilimo wa Halmashauri ya Buchosa, Lameck Obwago anasema zaidi ya tani 2,700 za pamba zinatarajiwa kununuliwa wilayani Buchosa na, hadi Juni 30, zaidi ya tani 400 zilikuwa zimenunuliwa huku wakulima wakilipwa zaidi ya Sh500 milioni.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema inayoundwa na halmashauri za Sengerema na Buchosa, Emmanuel Kipole, anasema zaidi ya tani 6,000 zinatarajiwa kuvunwa kwenye eka 48,000 zilizolimwa msimu huu zikilinganishwa na eka 28,000 za msimu wa 2017/18.

Awali, wilaya hiyo ilitarajia kuvuna zaidi ya tani 20,000 lakini mvua nyingi zilizonyesha kuliko mahitaji ya pamba pamoja na wadudu waharibifu walioishambulia wamepunguza mavuno.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Dk Joseph Chilongani naye anasema uhakika wa malipo kwa wakulima, udhibiti wa mizani, urahisi wa uratibu, usimamizi, utoaji wa elimu na huduma kwa wakulima umeongeza ufanisi msimu huu.

“Kupitia Amcos 87 zenye vituo vya ununuzi 246, Wilaya ya Meatu inatarajia kununua zaidi ya tani 53,000 kutoka tani 19,000 zilizonunuliwa msimu wa 2016/17,” anasema Dk Chilongani.

Changamoto

Kutokana na upya wa mfumo huo, baadhi ya Amcos zinakailiwa na changamoto ya kukosa mtaji hivyo kulazimika kutegemea fedha kutoka kampuni binafsi na ada ya Sh33 kwa kila kilo inayonunuliwa.

Changamoto nyingine ni viongozi wa vyama hivyo kutokuwa na elimu ya kutosha na uzoefu wa masuala ya ushirika, kukosa ofisi za kununulia na maghala ya kuhifadhia pamba na usalama mdogo wa fedha vituoni.

“Kukosekana kwa eneo au vifaa maalum na salama za kuhifadhia fedha kwenye vituo vya ununuzi kunaongeza gharama za uendeshaji kwa sababu fedha zinapelekwa kituoni kila siku kulingana na kiwango cha pamba inayotarajiwa kununuliwa,” anasema Dk Chilongani.

Kutokana na changamoto ya usalama, baadhi ya viongozi wa Amcos wanalazimika kuzihifadhi majumbani mwao fedha zinazosalia baada ya malipo ya siku hali ambayo tayari imesababisha upotevu wa zaidi ya Sh1.8 milioni katika Amcos ya Mwanuzo wilayani Meatu.

Kutokana na hilo, Dk Chilongani anasema mhasibu wa Amcos hiyo, Fabian Charles anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusu upotevu huo.

Wakulima

Baadhi ya wakulima walioanza kuona utendaji wa mfumo huo, wameusifia na kuitaka Serikali kuziimarisha Amcos kwa kushughulikia changamoto zilizopo.

Mkulima wa Kijiji cha Mwabusalu kilichopo Meatu, Bertha Kitumbu anaiomba Serikali kuwajengea uwezo wa usimamizi na udhibiti wa fedha viongozi wa Amcos hizi mpya.

“Ni mfumo usio na usumbufu. Mkulima unakuwa na uhakika wa kupata fedha zako. Vyama vikiimarishwa zaidi, manufaa yataonekana kwa wengi,” anasema.

Mkulima mwingine, John Kisunzu anausifia mfumo huo akisema umewaondolea adha ya kukopwa. Akizungumza muda mfupi baada ya kuuza kilo zake 700 na kupokea Sh880,000 anasema hali imebadilika.

“Natarajia kupata fedha nyingi zaidi kutoka kwenye eka tano nilizolima mwaka huu. Haya ni mavuno ya kwanza, pamba nyingi bado ipo shambani,” anasema Kisunzu.

Mkaguzi wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) wilayani Sengerema, Stella Albert anasema Amcos zimerahisisha usimamizi wa sheria, kanuni na utaratibu wa kulinda ubora kuanzia shambani, vituo vya ununuzi, kwenye maghali hadi kiwandani.

“Tulikuwa tunapata shida kuwadhibiti wanunuzi binafsi. Baadhi yao walikuwa wakifunga vituo na kukimbia wanapoyaona magari ya TCB. Mfumo wa Amcos umerahisisha kazi na majukumu yetu huku ukilinda ubora wa pamba,” anasema Stella.

Viwanda vya kuchambua

Akizungumzia mfumo wa ununuzi msimu huu, meneja wa Kiwanda cha Kahama Oil Mill kinachonunua na kuchambua pamba wilayani Maswa, Dionis Mudo anasema kumekuwa na ongezeko la ubora msimu huu.

“Gharama za uendeshaji zimepungua kwa sababu ununuzi unafanywa na Amcos, zamani tulilazimika kuajiri makarani kufanya kazi hiyo. Pia, tunapata pamba kirahisi kulinganisha na zamani tulipokuwa tukikimbizana huko vijijini,” anasema Mudo.

Hadi Julai 6, meneja huyo anasema kampuni hiyo ilikuwa imenunua zaidi ya tani 2,100 huku zaidi tani 1,200 zikiwa zimefikishwa kiwandani hapo kwa ajili ya kuchabuliwa.

Hata hivyo, ameiomba Serikali kudhibiti upendeleo unaoonyeshwa na baadhi ya maofisa wa Amcos kwa kuuza ya kampuni.

Zaidi ya tani 600,000 zinatarajiwa kuvunwa msimu huu kutoka eka milioni tatu zilizolimwa na zaidi ya wakulima 500,000 wa wilaya 54 katika mikoa 17 inayolima zao hilo nchini.

Mafanikio yamepatikana baada ya kuwekeza zaidi ya Sh36 bilioni kwenye ununuzi wa pembejeo, huduma za ugani na kutoa elimu kwa wakulima.

Takwimu za Bodi ya Pamba zinaonyesha kushuka kwa uzalishaji kuanzia msimu wa mwaka 2012/13 zilipovunwa tani 357,133 ambazo mpaka 2017/18 zilipungua hadi tani 132,928.

Kilimo cha mkataba kilichorejeshwa msimu huu kinatarajiwa kuongeza mavuno endapo udhibiti wa wadudu waharibifu utafanywa.

Advertisement