Mambo 10 ya kuzingatia kabla ya kufungua kesi ya ardhi

Muktasari:

  • Kwa mazingira yaliyopo nchini, kesi nyingi zinazofunguliwa huchukua muda kabla ya hukumu kutolewa. Kati ya maeneo yenye migogoro mingi ni sekta ya ardhi. Ili kuipata haki yako kwa wakati, unapaswa kuyatambu amambo muhimu 10 kabla hujafungua kesi ya ardhi.

Kesi ya ardhi ni mashitaka yaliyowasilishwa mbele ya mahakama kuhusina na mgogoro wa ardhi uliopo ili kuyatolea uamuzi.

Mgogoro huo unaweza kutokana na sababu nyingi tofauti kama vile kuvunjika kwa mkataba upangaji wa nyumba, uvamizi wa kiwanja au matumizi mabaya ya kiwanja.

Hata hivyo, si kila kesi iliyopo mahakamani kwa sasa ilipaswa kuwapo. Endapo mambo ya msingi yangezingatiwa kabla ya kufunguliwa, yamkini asilimia kubwa ya kesi zisingefika mahakamani.

Yapo mambo 10 ya kuzingatia kabla hujafungua kesi ya ardhi. Kwanza ni kuhakikisha unayo mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.

Sheria ya mwenendo wa kesi za madai ya mwaka 2002 ikisomwa pamoja na Sheria ya Mahakama za utatuzi wa migogoro ya Ardhi ya 2002 inasema kila mtu anayefungua kesi ya ardhi mahakamani anapaswa kuwa muhusika mkuu au muathirika wa vitendo vilivyofanywa na anayemshitaki. Hata hivyo, sheria inaruhusu kuwakilishwa.

Jambo jingine ni kufahamu thamani ya eneo la mgogoro, ni muhimu kwa kuwa husaidia kufahamu kesi yako inapaswa ifunguliwe katika mahakama gani. Baraza la kata husikiliza kesi za maeneo yenye thamani isiyozidi Sh3 milioni, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya thamani isiyozidi Sh50 milioni na mahakama kuu inayozidi Sh50 milioni.

Hakikisha unafahamu kiini cha kesi husika. Usikurupuke kufungua kesi kama hufahamu nani hasa alifanya kitendo gani na nini kilifuata mpaka kufika hapo.

Hakikisha muda wa kufungua kesi haujapita. Sheria inatoa ukomo wa mashauri ya ardhi kuwa ni ndani ya miaka 12 kuanzia mgogoro ulipojitokeza. Kwa hiyo, endapo utafungua zaidi ya hapo utakuwa umepoteza haki yako.

Pia kuna muda wa kukata rufaa ambao ni siku 45 kutoka kata kwenda wilaya na siku 60 kutoka wilaya kwenda mahakama kuu. Piga hesabu vizuri ili udai haki yako pasipo mashaka yoyote.

Hakikisha unayemfungulia kesi ndiye muhusika. Usimfungulie mtu kesi kwa hila au kwa kubahatisha. Kutomfahamu muhusika kutakupotezea muda.

Hakikisha unafahamu mahakama sahihi ya kupeleka shauri lako. Kesi zote za ardhi zinatakiwa zifunguliwe katika baraza la kata, wilaya au mahakama kuu na sio mahakama za kawaida.

Kigezo kingine ni kwamba, thamani ya eneo la mgogoro huamua mahakama inayofaa kufungua kesi yako.

Kesi zote huamriwa kwa ushahii, hakikisha unao wa kutosha. Usifungue kesi kwa kuiga, fungua ukiwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yako. Sheria inaeleza wazi, mlalamikaji ndiye mwenye jukumu la kuthibitisha madai yake dhidi ya mdaiwa.

Kila kesi ina gharama za uendeshaji wake, hakikisha unao uwezo wa kuzilipa. Kila hatua ya kesi kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi mahakama kuu ina gharama zake. Usidhani utaendesha kesi bure. Kuna gharama za kufungua, kuandaa nyaraka, mahakama kutembelea eneo la mgogoro na gharama nyinginezo.

Hata kama kesi yako itaendeshwa kwa msaada wa kisheria bado wewe mwenyewe utahitajika kuhudhuria mahakamani.

Jambo jingine la kuzingatia ni kuhakikisha upo tayari k-kushinda au kushindwa kesi. Usiende mahakamani na matokeo ya kesi au hukumu ya kesi mkononi. Kumbuka mwamuzi sio mashahidi, wakili au mtazamo wako bali hakimu anayetumia sheria zilizopo.

Hakikisha unafahamu kitakachofuata baada ya kesi. Baada ya hukumu kutoka kitakachofuta inategemea jinsi kinavyokugusa. Ikiwa umeshinda omba nakala ya hukumu na kazia hukumu na dai gharama. Kama hujaridhika na hukumu, kata rufaa mahakama ya juu yake.