Mapro wanavyonogesha Ligi ya Wanawake

Muktasari:

  • Mashindano Ligi Kuu ya Wanawake yameshika kasi Tanzania Bara na ushindani mkubwa umejitokeza baina ya timu zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu. Ligi Kuu Wanawake ilianzishwa Mwaka 2017 chini ya usimamizi wa aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi.

Imezoeleka Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) ndizo zinasajili wachezaji kutoka nje ya nchi ‘mapro’ ili kuongeza ushindani wa mashindano hayo yenye hadhi kubwa nchini.

Upepo umebadilika mapro sasa wapo hadi katika Ligi Kuu ya Wanawake ikiwa ni miaka miwili tangu ilipoanzishwa mwaka 2017.

Mashindano hayo yameshika kasi Tanzania Bara na ushindani mkubwa umejitokeza baina ya timu zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu. Ligi Kuu Wanawake ilianzishwa Mwaka 2017 chini ya usimamizi wa aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi.

Ligi hiyo inapambwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ambao wameongeza msisimko wa mashindano hayo msimu huu. Miongoni mwa timu zenye wachezaji wa kigeni ni Simba Queens, Evergreen na Alliance Girls. Sporti Mikiki imezungumza na baadhi ya wachezaji wa kigeni ambao wameeleza maisha ya soka la kulipwa hapa nchini yalivyo.

JOELLE BUKULU-SIMBA

Nyota huyu raia wa Burundi ni kiungo mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha Kocha Omary Mbweze wa Simba Queens.

Joelle ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaolipwa mshahara mzuri na posho ya kutakata kutokana na kipaji chake cha soka.

Akizungumza na Spoti Mikini, Mbweze anamuelezea Joelle ni mchezaji mwenye mchango mkubwa ndani ya timu hiyo.

“Joelle anajua soka ametengeneza pasi nyingi za mabao ni hodari uwanjani na kwa namna wanavyoishi wote kambini. Posho za wachezaji wote ni sawa tofauti ni kwamba mshahara wake umeboreshwa,”anasema Mbweze.

Joelle anasema kikubwa ni ushindani ambao alianza kuonyesha kwenye ligi hiyo muda mfupi baada ya kuanza mashindano hayo.“Ligi ya huku ina ushindani mkubwa tofauti na kwetu Burundi, hilo pekee ndilo limechangia nije Tanzania naamini nitaendelea kubaki katika kiwango bora,” anasema Joelle.

Anasema maisha ya Tanzania ni kawaida kama ilivyo Burundi, hivyo hapati shida kwa kuwa wachezaji wenzake wanampa ushirikiano jambo linalomfanya aendelee kufurahia maisha. “Kuhusu maisha kwa maana ya vyakula havina tofauti na nyumbani, awali lugha ilinisumbua kidogo lakini kwa sasa naenda na wenzangu sawa ingawa siwezi kunyosha maneno kama wanavyozungumza wao,”anasema kiungo huyo.

Anasema endapo wachezaji wazawa wakiendelea kujituma kwa bidii anaamini watafika mbali kwa namna ya uchezaji wao na amewataka kujitambua katika kazi.

Pia Simba Queens imemsajili mshambuliaji mwingine kutoka Burundi, Asha Jafari ambaye amecheza nusu msimu kabla ya kurejea nyumbani wakati mashindano hayo yakiendelea.

RECHAL BUKURU- EVERGREEN

Huyo ni mchezaji wa timu ya Taifa ya wanawake ya Burundi. Rechal ana mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Evergreen

Katibu wa Evergreen Salim Luheka anasema Rechal anaishi maisha ya kawaida sawa na wachezaji wa Tanzania.

“Tuna wachezaji wawili wa kigeni kwenye timu yetu, Rechal na Mmalawi Tamala Simeza ambaye anacheza timu ya Taifa ya vijana ya Malawi chini ya miaka 17,” anasema Luheka.

Mtendaji huyo anasema mshahara wake hauna tofauti na wanaolipwa wachezaji wazawa, tofauti iko kwenye posho ambapo wageni wameongezwa kuwasaidia,”anasema mchezaji huyo.

Kwa upande wa Rechal raia wa Burundi anasema soka la Tanzania lina ushindani wa juu unaomsaidia kumuweka kwenye njia ya kuelekea kwenye ndoto za kuwa mchezaji tegemeo ndani ya kikosi cha timu ya Taifa.

“Ninanufaika zaidi kwenye kiwango kuhusu uchumi ipo siku nitakuja kula matunda ya kipaji changu, tofauti na Burundi ambako ushindani sio mkubwa kiasi kwamba inakuwa ngumu kujipima kiwango changu,” anasema Rachel.

ALLIANCE NAYO IMO

Alliance ya Mwanza imesajili wachezaji wanne kutoka Kenya, Maria Anes (kiungo mshambuliaji), Ivone Atione (mshambuliaji), Reila Kamanda (Winga) na Anitha Adongo (beki wa kati).

Kocha Ezekiel Chobanka anasema uwepo wa wachezaji hao umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya klabu hiyo.

Anitha anasema soka la Tanzania ni la kutumia akili zaidi kuliko nguvu kama ilivyo nchini kwao ambako wanatumia ‘chakula’. “Soka la Kenya tunatumia nguvu kupita kiasi lazima mchezaji awe fiti kwa kufanya mazoezi kweli kweli, lakini akili kidogo,”anasema Anitha.

Anitha anasema tangu alipojiunga na Alliance anajiona yuko nyumbani kwa kuwa haoni tofauti ya mgeni na mzawa, wote wanafurahi maisha.

“Maisha yapo vizuri ndio maana naendelea kucheza napewa stahiki zangu kama mfanyakazi wa Alliance. Nimechagua soka ndio chanzo cha kunitengenezea fedha lazima niliheshimu hata nikirudi kwetu nachukuliwa kwa heshima kwamba nacheza soka la kulipwa,” anaongeza libero huyo.