Mtaalamu wa ugavi anayetengeneza kashata

Thursday October 25 2018

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Mara nyingi tumezoea kutumia tui la nazi kupikia, kutengeneza mafuta au shughuli nyingine huku machicha tukiyatupa na kuyaona hayana umuhimu tena.

Basi tambua, ukitupacho kama uchafu kwa Asha Swedi (26) na Ally Saleh ni dhahabu kwani wamekuwa wakitumia machicha pamoja na tui lake kutengeneza kashata.

Licha ya udogo wake na kutengenezwa kwa dizaini tofauti lakini wao waliamua kutumia nazi hizo bila kuchuja tui lake ili kuongeza ladha kwa mlaji na kuwa wa tofauti na wafanyabiashara wengine wanaotengeneza bidhaa hizo.

“Utamu wa nazi upo katika tui, unapolichuja na kuacha machicha peke yake yanakuwa hayana ladha lakini ukiacha na tui lake linakuwa bora zaidi,” anasema Asha.

Muhitimu huyo wa shahada ya kwanza ya ununuzi na ugavi anasema aliamua kuachana na kitu alichosomea na kuanza kujifunza ujasiriamali wa kashata kupitia mtandao wa Youtube na makundi mbalimbali ya mapishi ya WhatsApp. “Nilipomaliza tu chuo nikaanza, nikiwa na mtaji wa Sh10,000 ambao niliutumia kununua malighafi zote hadi kashata kukamilika. Baada ya kuuza iliweza kuzaa mara mbili,” anasema Asha.

Anasema jambo hilo lilimtia moyo na kumfanya aongeze bidii ya uzalishaji ili kukuza bishara yake. Hivi sasa anazalisha kashata za ladha tofauti ikiwamo nazi, maziwa na karanga.

Kutokana na juhudi alizoweka, anasema mtaji wake umeongezeka na sasa unakaribia Sh700,000 na kwa siku ana uwezo wa kutengeneza kilo 15 hadi 20 za kashata na kuziuza jumla na rejareja.

Kutokana na uzalishaji huo, anasema kwa wiki anaingiza kati ya Sh300,000 na Sh400,000 huku kila kilo moja akiiuza kwa Sh18,000 hadi Sh20,000. “Ubora wa bidhaa zetu umewafanya watu wengi watuchague na kuamua kununua bidhaa zetu huku kwa wiki huwa tunatumia zaidi ya nazi 100,” anasema.

Mbali na kashata, Asha alisomea utengenezaji keki pamoja na vitafunwa vya aina mbalimbali zikiwamo tambi.

Kama alivyojifunza mtandaoni, anasema masoko ya bidhaa zake pia huyapata kupitia mitandao ya kijamii hasa Instagram na Facebook ingawa wapo wanaotembelea ofisini kwao au wanaopewa taarifa na wateja wa awali waliowahi kuzitumia bidhaa zao.

Biashara ya mtandao, kama zilivyo nyingine, ina changamoto. Anasema kubwa anayokutana nayo mara nyingi ni baadhi ya wateja kutokuwa waaminifu huku baadhi wakitaka mzigo bila kutoa fedha kwanza.

“Ni ngumu kumtumia mteja bidhaa kabla ya pesa kwa sababu hii ni biashara hauwezi kumuamini mtu ambaye humfahamu vizuri. Wengi huwa wanakosa uaminifu,” anasema Asha.

Kila mtu anapofanya biashara huwa ana malengo ya kufika mbali ndivyo ilivyo kwa Asha ambaye malengo yake ni kuikuza biashara hiyo akishirikiana na mbia aliyenaye kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuajiri watu wengi zaidi na kuwafikia Watanzania wengi.

“Sasa hivi tupo wawili tu lakini wateja wetu wa jumla tunaweza kuwafikia sehemu yoyote walipo kulingana na mahitaji yao ya siku. Huwa tunafundisha watu utengenezaji wa kashata na bidhaa nyingine kwa Sh300,000 mpaka mteja atakapoelewa mwenyewe,” anasema Asha.

Advertisement