Namna ya kukabili maumivu wakati wa tendo la ndoa

Kuna mambo yanayochangia maumivu wakati wa kushiriki tendo la ndoa kwa wanawake.

Ikumbukwe kuwa dalili kubwa ya tatizo hili ni mwanamke kuhisi maumivu wakati au baada ya tendo la ndoa.

Tatizo hili linaweza kuambata na kukaamaa kwa misuli ya maeneo ya ukeni na kuwa na hali ya ukavu. Pia, tatizo hilo linaweza lisihitaji matibabu kwa kutumia dawa, mwathirika na mwenza wake wanaweza kupewa elimu ya afya ya uzazi na tatizo likatatulika. Kama chanzo ni tatizo la kuumizwa kihisia au kuathirika kisaikolojia mgonjwa atapewa ushauri nasaha.

Kama kuna ni mifarakano ya uhusiano ni vyema ikamalizwa ili kupata utulivu wa kiakili.

Vile vile waliowahi kunyanyaswa au kudhalilishwa kijinsia ikiwamo kubakwa au kulazimishwa kuolewa pasipo hiyari watahitaji kupata ushauri nasaha ili kukabiliana na tatizo hili. Kwa wale ambao wametoka kujifungua ni vyema kutowahi kushiriki tendo ndoa angalau mpaka zipite wiki sita, kwa kuwa baada ya kujifungua njia ya ukeni huwapo na vijeraha vinaweza kuchangia mwanamke kuhisi maumivu wakati wa tendo.

Kwa wale wanaopata tatizo hili kwa sababu ya ukavu ukeni ikiwamo wale wanaokaribia ukomo wa hedhi au ambao tayari wameisha fikia ukomo wa hedhi wanaweza kutumia vilainishi maalumu.

Vile vile zipo krimu za kisasa zenye kiambata cha homoni ya kike ya oestrogen ambazo zikitumiwa zinaweza kutatua tatizo la ukavu wa uke na kukakamaa kwa njia ya uke. Kama chanzo cha maumivu ni uwepo wa maambukizi ukeni na maeneo ya mji wa mimba ikiwamo maambukizi ya fangasi (yeast), uambukizi wa bakteria na virusi (herpes) watatibiwa kuendana na bainisho la uambukizi.

Vile vile maambukizi ya mji wa mimba na maeneo ya jirani ikibainika chanzo maumivu kinachangiwa na matatizo haya mgonjwa atapewa matibabu ya dawa za antibiotiki. Wale wote watakaobanika kuwa na maambukizi yatokanayo na magonjwa ya zinaa (sexual Transmitted disease) watahitaji kutibiwa na wenza wao ila kuzuia kuenea kwa maambukizi. Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu.