SIASA ZA KITAA : Nassari pigo kwa taifa, vijana kuliko Chadema

Muktasari:

  • Kwa hiyo Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikuwa na taarifa? Katibu mkuu wa chama au Katibu wa wabunge Chadema hakujua kinachoendelea? Nassari ‘kauza’ mechi kutojua anatakiwa afanye nini na yeye ni nani. Inasikitisha sana.

Joshua Nassari ana wakati mgumu sana. Achana na kupokwa ubunge wake pia haaminiki na baadhi ya wana Chadema. Pamoja na maelezo yake mengi, kwa mara ya kwanza baadhi ya wana Chadema nao wanaungana na maamuzi ya Spika Job Ndugai.

Kosa kubwa la Nassari ni kuruhusu hili litokee wakati huu mgumu kwa siasa za upinzani. Alionywa na Mkuu wa Wilaya, Jerry Muro juu ya kutoitumia ofisi yake muda mrefu. Kwamba anaichukua kwa matumizi mengine. Dogo akawa kimya akitupia picha mitandaoni kutoka Marekani. Kosa hilo.

Chadema ya sasa, ukiwa tofauti kimtazamo wanaamini umenunuliwa. Katengeneza mazingira mabaya kwake muda mrefu. Ametajwa mara kadhaa kama mmoja wa wabunge watakaounga mkono juhudi. Akawa kama hasikii. Hii ni kutokana na ushiriki wake mdogo ndani ya chama.

Ndiyo maana tatizo lake lina maswali mengi kuliko majibu. Kibaya zaidi kukataa kwake maswali katika mkutano na waandishi wa habari ilishangaza wengi. Anaogopa nini kuulizwa maswali kama kweli kaonewa? Aliwaita waandishi ili washuhudie akilia tu basi? Lilikuwa kosa lingine kubwa.

Anadai alimpeleka mkewe Marekani ili akajifungue. Mazingira ya tiba Marekani hayawezi kufanya Nassari ashinde ‘wodini’ hata akose vikao vitatu. Eti atamuachaje mkewe kwa vikao vya laki tatu kwa siku. Anashindwa kuelewa ubunge siyo posho tu bali ni uwakilishi wa watu.

Kwa hiyo Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haikuwa na taarifa? Katibu mkuu wa chama au Katibu wa wabunge Chadema hakujua kinachoendelea? Nassari ‘kauza’ mechi kutojua anatakiwa afanye nini na yeye ni nani. Inasikitisha sana.

Chadema ni kama mtu aliyeng’atwa na nyoka. Hata akiguswa na jani anashtuka sana. Nassari alitakiwa atambue hili, badala ya kuishi kimazoea akidhani Ndugai ni sawa na Anne Makinda.

Siwalaumu Chadema wanaomshutumu na kuungana na Ndugai. Hata kaka zake huko Arusha Godbless Lema na Binamu Bananga sishangai kukaa kwao kimya. Dogo kafanya faulo ya wazi kwa makusudi, kwa kupuuzia au kuishi kwa mazoea.

Kinachoshangaza siyo mgeni na shughuli za kibunge. Huu ni mwaka wake wa saba bungeni. Inakuaje afanye mambo kiholela kiasi hiki? Hajaonewa bali karuhusu hili litokee akisahau njia wanazopitia wenzake awamu hii. Ukisikiliza utetezi wake. Mtu timamu inabidi ajivishe ujasiri wa kulazimisha kumwelewa. Hili siyo pigo kwa Chadema, ni pigo kwa vijana na taifa. Atafanya vijana watiliwe shaka kupewa nafasi za uwakilishi. Pili marudio ya uchaguzi yanatafuna pesa nyingi za walipa kodi.