Neema yawasubiri wanahisa DCB ikipata faida ya Sh1.9 bilioni

Muktasari:

  • Benki ya DCB imeumaliza mwaka 2018 kwa mafanikio makubwa ambayo huenda yakawafurahisha wanahisa wake kwa gawio watakalolipwa baadaye mwaka huu. Benki hiyo, imepata faida ya Sh1.9 bilioni.

Dar es Salaam. Baada ya kuvumilia biashara mbaya iliyokuwapo 2017, Benki ya DCB inatarajia kuwafurahisha wanahisa wake baada ya kutengeneza faida ya Sh1.9 bilioni mwaka jana.

Faida hiyo kabla ya kodi imepatikana kutokana na usimamizi mzuri wa mikakati iliyowekwa na kufanikiwa kuiondoa kwenye hasara ya Sh6.9 bilioni katika kipindi hicho.

Mkurugenzi wa biashara wa benki hiyo, James Ngaluko amesema sera ya gawio inaruhusu kutoa asilimia 50 ya faida kama gawio kwa wanahisa, hivyo utaratibu ukimalishwa utekelezaji utafanywa.

“Ila hilo litategemea uamuzi wa kikao cha mkutano mkuu wa mwaka utakaofanyika hapo baadaye. Endapo wanahisa wataridhia, gawio litatolewa,” amesema Ngaluko.

Katika hesabu za mwaka ambazo bado hazijakaguliwa zilizotolewa juzi na mkurugenzi wa fedha wa DCB, Zacharia Kapama, ufanisi wa benki hiyo umeongezeka kutoka kupata hasara ya Sh6.9 bilioni mwaka 2017 hadi faida hiyo ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 463.

Kapama anasema mafanikio hayo yametokana na juhudi pamoja na ushirikiano wa menejimenti kusimamia mipango na mikakati iliyowekwa.

“Tumeimarisha mfumo wa teknolojia katika uendeshaji wetu, tumeongeza utoaji mikopo pamoja na kupunguza kiasi ch amikpo isiyolipika,” amesema Kapama.

Kupata faida hiyo, amesema mapato ya riba yalikua mpaka Sh90.6 bilioni kutoka Sh88.4 bilioni zilizopatikana mwaka 2017 wakati Sh65 bilioni zilikopeshwa zikiwamo Sh21 bilioni za mikopo iliyotolewa kwa wafanyabiashara wadogo.

Tengo la mikopo isiyolipika, amesema limepungua kutoka Sh4.5 bilioni za mwaka 2017 hadi Sh264 milioni mwaka jana ingawa uwiano wa mikopo hiyo na jumla ya mikopo yote iliyotolewa imeendelea kubaki asilimia 18.

Katika mwaka huo mmoja, benki hiyo imepunguza gharama za uendeshaji kutoka Sh21 bilioni hadi Sh16.9 bilioni na kwamba bado wanaendelea kuangalia namna ya kuboresha maeneo tofauti. “Mwaka jana tulianza kuuza hisa stahiki ili kukuza mtaji. Hali ikiendelea hivi, nina uhakika mizania yetu inakua kwa walau asilimia 20 kila mwaka,” anasema.

Suala jingine linaloongeza matumaini ya kufanya vyema kwa benki hiyo iliyorodheshwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ni ongezeko la wateja.

Kw amiezi 12 iliyopita, wateja wake waliongezeka kwa asilimia 21.3 na kufika 175,204 mwaka jana wakilinganishwa na144,475 waliokuwapo mwaka 2917.