Ni vita ya filamu na muziki

Saturday June 30 2018

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi [email protected]

Tamasha la filamu za Zanzibar (Ziff) litafanyika kuanzia Julai 7 hadi 15 katika Viwanja vya Ngome Kongwe katika eneo la Stone Town, Unguja.

Tamasha hilo litahudhuriwa na waigizaji wakubwa kutoka mataifa mbalimbali wakiongozwa na Jordan Riber ambaye ameandaa filamu ya Bahasha iliyochezwa na waigizaji nyota kama Ayoub Bombwe, Godliver Gordian, Omary Mrisho na Catherine Credo.

Akizungumza kuhusiana na tamasha hilo la 21, Profesa Martin Mhando alisema mwaka huu tamasha hilo linatarajiwa kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na mabadiliko waliyoyafanya.

Alisema kuwa moja ya mabadiliko ni kuingiza filamu mbalimbali za zilizochaguliwa ambazo ni fupifupi na ndefu moja.

“Kuna zawadi mbalimbali nono kwa mwaka huu, mfano Dola 1,000 za Kimarekani, kombe na cheti kwa mshindi wa kwanza. Naamini kila mwandaaji wa filamu atataka kushinda zawadi hiyo,” alisema Mhando.

Alisema kuwa majaji mbalimbali watakuwa ‘busy’ kuchagua filamu bora. Mbali ya Bahasha, filamu nyingine ni Daladala, Binti Zanzibar ambayo ilishinda Sh4 milioni kwenye Tamasha la Filamu la Azam.

Profesa Mhando alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Sema na usikike’ yenye maana ya kupaza sauti katika kuhakikisha Tamasha la Ziff linazidi kuimarika.

“Tukiwa na haja moja, ya kupaza sauti katika kuhakikisha tamasha letu la ZIFF liweze kuzidi kuimarika siku hadi siku, Wanzibari na hata wageni watakaoshuhudia filamu hizi wataweza kuchukua utamaduni huo na kuupeleka nje kwa furaha kubwa katika kufikia hatima ya pamoja,” alisema Profesa Mhando.

Upande wa burudani

Mbali na filamu, tamasha la mwaka huu litahudhuriwa na wasanii mbalimbali ambao watafanya maonyesho ya muziki yatakayokuwa yakifanyika kila siku ndani ya Mambo Club, ukumbi uliopo ndani ya Ngome Kongwe kila baada ya filamu.

Kwa upande wake, Edward Lusala anayeshughulikia muziki kwenye tamasha hilo, alisema kuwa kutakuwa na filamu zaidi 120 ambazo zitaonyeshwa.

Lusala alisema mwaka huu wanatarajia kufanya ‘surprise’ kwa kumleta msanii mkubwa katika filamu ambaye bado wako kwenye mazungumzo naye.

Bahasha kufungua dimba

Mamia ya filamu zitaonyeshwa mwaka huu ikiwa ni pamoja na Bahasha ambayo itafungua uzinduzi wa tamasha hilo.

Bahasha imeandaliwa na taasisi ya MFDI ambayo pia ilitunga filamu maarufu ya Siri ya Mtungi.

Lusala alisema wamejiandaa kutoa burudani ya aina yake ambayo itaacha historia kwa mwaka huu.

Aliwataja wasanii wa muziki wanaotarajiwa kutumbuiza kuwa ni Darasa, Shetta, Aslay, Nandy, Ruby pamoja na kundi la The Mafik na wengine ambao wataingia kwenye orodha baada ya taratibu zilizobaki kukamilika

Advertisement