KUTOKA LONDON : Ongezeko la maradhi ya akili Majuu kutokana na ufukara na bangi

Muktasari:

  • Mathalan kutotumia dawa za kulevya au pombe. Hasa bangi. Kiasi kikubwa cha omba omba wana matatizo makubwa ya kisaikolojia na wameshaharibika akili.

Jumapili iliyopita tulizungumzia omba omba na mafukara wanavyoongezeka London. Kila pembe hukosi mwanamke, kijana, mzee, mwanaume akibembeleza.

Omba omba huchagua vituo vya kutolea fedha benki (ATM), masoko bomba, vituo vya usafiri (kama tulivyoona wiki jana), mikahawa na mahoteli. Omba omba hutumia lugha na maneno ya kiufundi. Wengine hulia hawana mahali pa kulala. Ambayo si kweli maana mashirika ya fadhila hutoa nafasi za kulala. Ila kwa kuwa baadhi yao hukataa kufuata masharti yanayotolewa katika makazi hayo.

Mathalan kutotumia dawa za kulevya au pombe. Hasa bangi. Kiasi kikubwa cha omba omba wana matatizo makubwa ya kisaikolojia na wameshaharibika akili.

Miaka mingi safu hii imezungumzia kuzidi kuenea uvutaji bangi, duniani. Namna bangi inavyochanganywa na dawa kali zinazoharibu ubongo. Wapo wanaotetea kwa kuwataja wanamuziki maarufu kama merehemu Bob Marley aliyetukuza bangi na kutunga nyimbo tamu za kuelemisha jamii.

Wanasahau kuwa ingawa Rasta huyu Mjamaika alivuta bangi alikuwa na fedha, nidhamu, alikula vizuri na kufanya mazoezi ya kukimbia, kuogelea na soka, karibu kila siku.

Wengi Afrika tunavuta bangi kutokana na ufukara na kutokuwa na ajira. Tunasahau ukiwa na matatizo huwezi kuyafumbua kwa ulevi au unga muflis.

Kwanza kabisa bangi na ulevi ni nini hasa?

Bangi, ulevi, kahawa, soda (kama Cocacola au Red Bull), na sigara ni “vichangamshi.”

Miili yetu ina mishipa ya fahamu kupitia ubongo, uti wa mgongo, ngozi, pua, macho, masikio, nk. Tunapojisikia vibaya hisia zetu zina vitu asilia vinavyoweza kutuchangamsha. Kwa mfano ukila matunda unapata sukari inayokupa nguvu na uchangamfu. Ukifanya mazoezi ya viungo, mapenzi au kuona jambo la kuchekesha, ubongo hutoa kemikali inayoitwa “Serotinin”...

Usipotegemea sasa uasilia wako (ulioumbwa nao) na kutafuta vichangamshi vya nje (pombe, kahawa, soda, bangi) unaupa mwili kazi ya kuchambua jambo la nje. Moja ya muathirika ndiyo figo tuliyoizungumzia makala zilizopita. Pili ni mishipa ya fahamu kama ubongo, ngozi, na moyo. Ndiyo sababu ukivuta sana bangi unajisikia kuchangamka (au kutulia) lakini baadaye unashupaza ubongo.

Sayansi imeshatafiti na kugundua athari kuu za bangi ni usahaulifu, kubadilika badilika tabia (hasira za ghafla au furaha ya kuja na kuondoka) hatimaye ubongo kubatilika. Sasa hivi kiasi kikuu cha walemavu akili Ughaibuni ni waathirika bangi.

Wanaofaidika ni wafanyabiashara

Karibuni bia mpya inayochanganya bangi imetolewa California na Nevada, Marekani na Ontario , Canada. Miaka mingi pia Uholanzi (iliyohalallisha bangi miongo kadhaa sasa) imejenga mikahawa inayouza bangi katika chai, kahawa na keki.

Watumiaji huonekana wamelemaa lemaa na hapo hapo wanaochangamka ni wafanya biashara. Bia hizi moya zitawatajirisha sana maana baada ya miaka michache itazagaa duniani.

Nilipozungumza na jamaa wanaopenda bangi hapa London walidai eti sasa hakuna tena maradhi ya saratani inayotokana na moshi wake.

Tatizo ni hili

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya hawaathiriki. Namfahamu mmoja anayedai alivuta bangi mara moja tu akiwa kijana miaka 40 iliyopita.

“Kwangu ni biashara kama nyanya. Naziuza nyanya lakini sizili...”