Serikali ichague mbinu muafaka kuchochea uchumi

Muktasari:

  • Ni hali ya kawaida uchumi kuyumba duniani lakini hilo linapojitokeza, hatua za haraka huchukuliwa kukabiliana na madhara yake. Zipo njia tofauti za kufanikisha hilo.

Siku zote, uchumi ndio unaoamua siasa na mambo mengine yote ya kijamii. Ustaarabu wa jamii pia hutegemea uimara wa uchumi pamoja na mambo mengine.

Kama ilivyo maeneo mengine, uchumi nao hubadilika. Kuna kipindi hushamiri na wakati mwingine kusinyaa. Wiki iliyopita, kwa mfano, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga alisema hali ngumu ya uchumi ni jambo la mpito.

Kuna mijadala inaendelea mingi ikiwa imejikita katika dalili za mdodoro wa uchumi. Mdororo wa uchumi una viashiria mbalimbali kama kuzorota kwa uzalishaji, uuzaji, ununuzi, usambazaji na matumizi ya bidhaa na huduma.

Viashiria vingine ni kupungua kwa mzunguko wa fedha, faida na ongezeko la hasara katika biashara za aina tofauti. Makusanyo ya Serikali kushuka yakiwamo ya kodi na yasiyo ya kodi, ugumu wa kupata na kulipa mikopo, upungufu wa ajira na kipato.

Kati ya mambo ambayo hayajawekewa mkazo wa kutosha ni namna ya kutoka katika mdororo wa uchumi ingawa zipo njia tofauti za kukabiliana na hali hiyo.

Matumizi ya Serikali

Kati ya mbinu za kuchochea uchumi zilizopo ni matumizi ya Serikali ambayo hujumuisha shughuli za maendeleo na kawaida. Matumizi ya kawaida ni pamoja na uendeshaji wa ofisi kila siku, mishahara ya watumishi, semina na safari mbalimbali.

Shughuli za maendeleo ni kama ujenzi na ukarabati wa miundombinu kama vile barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege.

Kinachofanyika katika kuchochea uchumi kutokana na matumizi ya umma ni uingizaji wa fedha katika uchumi. Serikali ni mlaji mkubwa wa bidhaa na huduma. Inavyozidi kutumia ndivyo inavyochochea na kusisimua uchumi kwa kuongeza fedha katika mzunguko.

Serikali inapotumia inalipa watu na kampuni. Walipwaji nao hutumia fedha hizi kununua bihaa na huduma. Hii huchochea uzalishaji na kukuza ajira. Matokeo ya ajira ni kipato ambacho hukuza matumizi mapya. Ni muhimu kwa Serikali kutumia ili kuchochea na kusisimua uchumi.

Sekta binafsi, kaya

Matumizi ya sekta binafsi ni muhimu kuchochea uchumi hasa yanapoelekezwa kwenye uwekezaji ukiwamo wa uanzishaji na upanuzi wa vitega uchumi na uendeshaji wa siku hadi siku wa vitega uchumi hivi.

Matumizi haya hulazimisha ajira kutokea katika minyororo ya thamani na mafundo yake. Ajira hizi huleta kipato. Hivyo, ni muhimu kuwapo kwa mazingira rafiki yatakayovutia na kushawishi kukua kwa sekta binafsi ili kuchochea na kusisimua uchumi.

Matumizi ya kaya na mtu mmoja mmoja ni muhimu katika kuchochea na kusisimua uchumi. Matumizi haya huhusisha ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali kama vile vyakula, vinywaji, mavazi, viatu hata kufanikisha ujenzi.

Matumizi haya yanapofanyika fedha hubadilishana mikono. Wale wanaopokea fedha huzitumia pia hivyom kuimarisha mzunguko wake. Kiwango cha matumizi haya hutegemea kiasi cha fedha kinachobaki baada ya kulipa kodi. Hii ina maana kuwa sera za kikodi za nchi ni muhimu sana katika kuchochea na kusisimua uchumi.

Sera

Sera za kodi na fedha ni muhimu sana katika kukuza uchumi. Kodi ni makato yanayofanywa na mamlaka husika kwenye mauzo na kipato kingine chochote halali. Ni mojawapo ya vyanzo vya mapato ya nchi.

Mapato haya hutumika kugharimia bidhaa na huduma za umma kama vile afya, elimu, maji, ulinzi, usalama, miundombinu hata kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Sera za kodi zinaweza kuwa za kupanua uchumi au kuufanya usinyae. Sera za kupanua uchumi hujumuisha idadi ndogo na aina chache za kodi zinazochochea na kusisimua uchumi.

Sera za aina hii hubakiza kiasi kikubwa cha fedha mikononi mwa walipakodi. Kwa kadiri fedha nyingi zinavyobaki kwa walipakodi ndivyo uchumi unavyoweza kuchochewa na kusisimuliwa kwa haraka zaidi.

Kinyume chake ni sera za kodi zinazominya uchumi ambazo huwa na viwango vikubwa na aina nyingi za kodi. Pamoja na kodi, ruzuku ni muhimu sana kama chombo cha kutekeleza sera za kodi katika upana wake.

Ruzuku ni fedha inayotolewa na Serikali kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho. Ruzuku ni afya huchochea uchumi.