Serikali iziwezeshe mamlaka za Serikali za mitaa kutekeleza majukumu yao

Thursday August 9 2018

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 

By Joseph Alphonce

Takwimu zinaonesha kwa zaidi ya asilimia 90 mamlaka za Serikali za mitaa zinategemea ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi, kulipa mishahara na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Uwapo wa mamlaka za Serikali za mitaa na majukumu yake unatamkwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na 146.

Mamlaka za serikali za mitaa kwa tafsiri nyepesi ndiyo sehemu kuu ya wananchi wa kawaida na masikini kuamua mustakabali wa maisha yao. Ni sehemu pekee ya wananchi kushiriki kikamilifu kuweka malengo na mikakati ya kupambana na umasikini, ujinga na maradhi.

Kwa mtazamo wangu, ili mamlaka za serikali za mitaa ziweze angalau kujisimamia na kutekeleza majukumu yake vyema ni jukumu la Serikali Kuu itakapoona inafaa na kwa wakati muafaka iache baadhi ya vyanzo vya mapato vya uhakika vikusanywe na kutumiwa na mamlaka za serikali za mitaa. Hakuna namna ambayo wananchi hasa wanyonge na masikini wanaweza kupambana na umasikini na kujiletea maendeleo katika maeneo yao bila wao wenyewe kubuni na kuweka mikakati ya kusimamia yale wanayoyaamua katika vitongoji na mitaa, vijiji, kata na halmashauri.

Takwimu zinaonyesha wastani wa asilimia 65 za kazi za Serikali zinatekelezwa katika mamlaka za serikali za mitaa kwa kusimamiwa na Serikali Kuu.

Ni wastani wa asilimia 35 pekee ya majukumu ya Serikali ambayo yanatekelezwa na Serikali Kuu.

Zipo changamoto zinazoripotiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo kukosa fursa ya kukusanya mapato kutoka kwenye baadhi ya vyanzo ambavyo kwa sasa vinasimamiwa na Serikali Kuu.

Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekosa fursa ya kuajiri, ikiwemo kada ambazo wangeweza kusimamia mchakato wa ajira zao.

Kwa upande wa Serikali Kuu imekuwa ikitajwa kushindwa kuziachia Mamlaka kamili mamlaka za serikali za mitaa kwa sababu kadhaa ikiwemo upungufu mkubwa wa watumishi wenye uwezo wa kujisimamia na kutoa maamuzi sahihi.

Mamlaka za serikali za mitaa haziishii kwenye ngazi ya halmashauri za majiji, manispaa, miji au wilaya tu, zinaenda mpaka ngazi ya kitongoji.

Takwimu zinaonyesha kuwa vijiji, mitaa na kata nyingi nchini hazina watendaji wenye sifa.

Vipo baadhi ya vijiji, wananchi wa kawaida ndiyo wanashikilia nafasi ya ofisa mtendaji wa kijiji kwa kujitolea, tafakari na unyeti wa nafasi hii.

Ofisa mtendaji wa kata ndiye mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli zote za kata katika eneo lake, hivyo hivyo kwa ofisa mtendaji wa kijiji au mtaa.

Hizi ni nafasi nyeti ambazo Serikali inapaswa kuajiri watu makini, ikiwezekana wenye kiwango cha chini cha elimu kiwe stashahada katika nyanja za maendeleo ya jamii, mipango au nyingine kadiri ya mahitaji.

Kwa sasa wakati hali ya rasilimali watu wenye sifa katika ngazi ya chini si ya kuridhisha, Serikali Kuu ikipendezwa inaweza kufanya yafuatayo;-

Mosi, kufanya uamuzi wa kimkakati wa kuajiri maofisa watendaji wa kata, vijiji na mitaa wenye sifa na vigezo nchi nzima. Lengo kuhakikisha kila Kata, kijiji na mtaa vina watendaji makini wanaoweza kusimamia rasimali za nchi na kusimamia maendeleo katika maeneo yao.

Pili, utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya mamlaka za serikali za mitaa uzingatie ushirikishwaji wa wananchi.

Wananchi wenyewe ndiyo wabuni aina ya miradi wanayohitaji kwa ajili ya kujiletea kipato na kupambana na umasikini.

Tatu, mafunzo ya mara kwa mara kwa watendaji wa halmashauri wakiwemo maafisa watendaji wa kata, vijiji na mitaa. Utaratibu wa kuanza kuzipa mamlaka kamili mamlaka za serikali za mitaa ni vema ukafanyika kwa awamu ili kuepusha upotevu na mgawanyo usio sawa wa rasilimali.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Advertisement