Simba ilinza na Mbabane, ikamalizia kwa AS Vita

Novemba 28, 2018 mabingwa wa soka Tanzania, Simba walianza safari ya kuusaka ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ilipotia mguu Uwanja wa Taifa dhidi ya Mbabane Swallows.

Katika mchezo huo, Simba iliipiga mabao 4-1 na Desemba 4 mwaka jana ikahitimisha mchezo huo kwa kuibandua mabao 4-0 mjini Mbabane.

Baada ya mchezo huo, Simba ilikutana na kigongo kingine. Nkana Red Devils ya Zambia. Miamba ya Zambia iliwatoa jasho, mchezo wa kwanza kule Kitwe, iliwafunga mabao 2-1. John Bocco ndiye aliyefunga bao la penalti.

Desemba 16, Simba ilitua Dar es Salaam na kuweka mikakati kwa mchezo wa marudiano, Desemba 23.

Jonas Mkude, Meddie Kagere na Clatous Chama walihitimisha safari ya Nkana kwani walipindua matokeo na kuwa mabao 4-3.

Mchakamchaka wa Simba hata kutengeneza viporo vya Ligi Kuu ni kutokana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubadilisha utaratibu wa mashindano yake, kwani yatakuwa yakianza Agosti na kumalizika Mei yam waka unaofuata.

Matokeo ya Nkana, yanaipekeka Simba kwenye makundi. Miamba hiyo ilikuwa na Al Ahly ambayo imefuzu na Simba, JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DR Congo.

Pamoja na kupoteza mechi zote ugenini, Simba ilijiwekea malengo, kwamba inachotaka ni pointi moja tu ugenini. Haikujiandaa kisaikolojia kushinda ugenini, lakini ikafanya kweli nyumbani, matokeo yaliyowapa ahueni.

Simba ilifungwa mabao 5-0 na Al Ahly na AS Vita, lakini ikachapwa mabao 2-0 na Saoura huku yenyewe ikizifunga timu hizo, 3-0 JSS, 1-0 Al Ahly na 2-1 AS Vita. Zilikuwa mechi ambazo Simba ilipambana.

Wachezaji wa Simba walipambana kwenye mechi mbili muhimu, dhidi ya Nkana Red Devils na ile ya AS Vita. Hizi mechi zilikuwa na umuhimu wake.

Kwanza, mechi ya Nkana ilikuwa lazima wapambane kwa kuwa lengo la kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems ni kuhakikisha Simba inacheza makundi Afrika na ikatimia, Simba kushinda mabao 4-3.

Mechi ya AS Vita, ilikuwa ya kufa au kupona. Wachezaji walipigana ili kucheza robo fainali. Hapo wameua ndege wawili kwa jiwe moja kwamba mpango wa makundi ulitimia na sasa robo fainali kuwa ni hatua nyingine ambayo pamoja na kwamba Simba inaelekea huko, lakini hawakuwa wameifikiria.

Mpango wa Simba kwa mujibu wa mkakati, ni kuifikisha makundi na kwa kuwa haikuwa na uhakika, mpango mwingine ni kutwaa ubingwa wa Bara na kurudi na kuingia jumla hadi fainali.

Baada ya kuvuka hatua ya sasa ambayo haikutarajiwa, Mwekezaji Mkuu wa Simba, Mohamed Dewji ‘MO’ alisema sasa kinachofuata ni kutwaa ubingwa wa Afrika.

Akizungumza baada mechi na AS Vita ambayo Simba imeingia kati ya miamba nane ya soka Afrika, MO anasema: “Kinachofuata ni kuleta kombe la ubingwa Tanzania.”

Anasema hakuna kitakachoikwamisha Simba kufika mbali Afrika. Simba sasa inacheza na TP Mazembe kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CAF wiki iliyopita. Mechi zitakuwa kati ya Aprili 5 na 7 wakati Simba na TP Mazembe itapigwa Aprili 6.

Simba vs TP Mazembe

Simba itakuwa nyumbani kuialika TP Mazembe ikiwa ni miaka nane na siku tatu kwa mchezao wa kwanza wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezo huo Simba ililala kwa mabao 2-3.

Tayari kocha Aussems ameanza mikakati ya kuwanoa wachezaji wake ili kuhakikisha anapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kwanza wa nyumbani kisha kwenda kujihami wakiwa ugenini mjini Lubumbashi .

TP Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa michuano hii mikubwa ngazi ya klabu Afrika, walikuwa Kundi C, walimaliza katika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 11, wakifatiwa na CS Constantine na pointi zao 10.

Miamba hiyo ambayo juzijuzi ilifungwa mabao 3-0 na AS Vita Ligi Kuu ya DR Congo, ilimaliza makundi ikiwa timu ya pili kukusanya pointi nyingi ikitanguliwa na Esperance de Tunis iliyomaliza ikiwa na pointi 14 katika makundi yote. Mazembe ilimaliza ikiwa na pointi 11.

Aussems ataanza kukiweka kikosi chake kwenye hali ya mapambano kuanzia leo Jumatatu katika uwanja wao wa mazoezi wa Boko Veterans, baada ya kuwapa mapumziko wachezaji wake ambao hawakwenda kwenye majukumu ya timu za Taifa.

Baada ya kazi nzito, kocha huyo aliwapa mapumziko ya siku tano mara baada ya kumaliza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting. Wachezaji ambao waliitwa katika timu za Taifa kuna ambao wataanza mazoezi leo na wengine siku za mbele kulingana na umbali wa nchi walipo.

Simba watafanya mazoezi kwa siku nane kuanzia leo kabla ya Aprili 4 kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao, watautumia kama uwanja wao wa nyumbani kwa mechi za Ligi Kuu kabla ya siku mbili baadaye kuwavaa Mazembe.

AUSSEMS NA TP MAZEMBE

Akizungumzia TP Mazembe, Aussems anasema ameanza kutumia muda kuwafuatilia kuanzia mfumo wa soka lao na mambo mengine ya kiufundi. Anasema hatua hiyo ndio itamuwezesha kukiweka kikosi chake tayari kwa mapambano baada ya kufahamu mbinu za wapinzani wao ambao, hakuwa akiwatarajia kukutana nao kwenye hatua hiyo.

“Kabla ya droo na ratiba kupangwa nilikuwa natamani kukutana na Wydad Casablanca, hawa nilishawaweka katika mipango yangu na soka lao sio la kutisha katika mashindano haya kama TP Mazembe. “Sina sababu ya kuwa na hofu kwa sababu ninawafahamu TP Mazembe wale wa miaka mitatu nyuma sio hawa, na tunaendelea kujipanga ili kupata matokeo mazuri hapa nyumbani.

“Tunakutana na Mazembe bila ya kuwa na presha kwani, tunacheza na timu kubwa hapa Afrika ambayo kwa hatua ya robo fainali ilikuwa ni lazima tukutane na timu kama hii,” anasema Aussems.

VIONGOZI NAO

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Simba inatisha Afrika. Magori amekuwa na timu katika mechi zote 10 hadi kufikia sasa, ikishinda mechi sita na kupoteza nne huku akiwataka Watanzania kuiunga mkono Simba kwa kuwa ndiyo inayopeperusha bendera.

Akizungumzia ushiriki wa Simba kwenye michuano hiyo ya klabu Afrika, anasema kuwa pamoja na kufikia hapo, matunda yake yataanza kuonekana misimu inayokuja.

“Tumeingia robo fainali ambako imekuwa na mafanikio makubwa kwa soka letu na tumeweka malengo ya kwenda fainali na Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mohammed Dewji ‘MO’ itafanya kazi kwa umakini mkubwa ili kufanya vizuri katika hatua hii,” anasema Magori.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ anasema safari ya Simba kufika kileleni ni kama imeanza. “Baada ya kumaliza mechi na AS Vita na kufuzu, ndio ulikuwa mwanzo wa mikakati ya mechi inayofuata.

Tunataka kuiona Simba ikitikisa Afrika, na kila taifa la Afrika lifahamu kuna timu inaitwa Simba.

“Tuko katika mapambano, malengo yetu ni kucheza fainali Afrika hivyo, maandalizi na mikakati ya msingi inafanyika kuhakikisha Simba inafika mbali.

Anasema Simba inataka timu ifike mbali na motisha pekee ni kuongeza posho na kuamsha hamasa.

“Tulikuwa tunawapa posho, bonasi na vingine vichocheo vya hamasa kwa wachezaji na benchi la ufundi hizi zitaongezwa ili timu yetu iwe na ari ya kufika mbali Afrika.”