Teknolojia za kilimo zilizovutia wengi Sabasaba

Saturday July 28 2018

 

By Jackline Masinde, Mwananchi [email protected]

Dunia ya sasa kila kitu kinahitaji kutumia teknolojia ya kisasa ili kiwe na tija.

Kwa mfano, katika sekta ya kilimo na ufugaji, kinachowarudisha nyuma watu wengi ni matumizi madogo ya teknolojia au kutotumia kabisa. Na hii ndio tofauti kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazojikongoja kimaendeleo.

Nchi zilizoendelea zimeshajitosheleza kwa chakula kwa kuwa zinatumia teknolojia kuzalisha mazao mengi. Wanatumia teknolojia kuanzia kwenye mifumo ya kilimo na ufugaji, usimamizi wa miradi, pembejeo hadi masoko.

Kwa Tanzania, nasi hatuko nyuma wataalamu wamekuwa wakijihimu kubuni aina mbalimbali za teknolojia kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji wa miradi ya kilimo.

Makala haya yanadurusu baadhi ya teknolojia zilizowavutia wengi katika maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu ‘Sabasaba’ yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Farm Spray Robot

Hii ni mashine maalumu kwa ajili ya kumwagilia maji na dawa mashambani. Imetengenezwa na wasichana wawili wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT), Amina Shaweji(28) na Radhiana Idowa(23).

Wavumbuzi hawa wanasema mashine hiyo inatumia rimoti katika kufanya kazi yake na ina matairi yanayoiwezesha kutembea yenyewe inapokuwa inafanya kazi. Pia ina uwezo wa kumwagilia mazao hadi umbali wa mita 300 kutoka ilipo mashine, itategemea itakavyowekwa na mkulima.

“Mbali na matairi pia mashine hii ina mkono ambao unaweza kuinama na kuinuka. Mkono huu ndiyo unaofanya kazi ya kumwagilia”anasema Amina.

Amina aneleza kuwa mashine inaweza kumwagilia mazao yanayotambaa chini na yanayomea kwenda juu kama mahindi, miohogo, alizeti, pamba, mbogamboga na mazao mengine ya aina hiyo.

Radhiana anasema wakati wanaitengeneza walilenga zaidi mashamba yeye njia kwa kuwa zinazotoa nafasi nzuri kwa mashine hiyo kutembea.

“Pia mashine yetu ina tanki la maji na dawa lenye ujazo wa lita tano lakini tuna uwezo wa kuiboresha zaidi likawa na ujazo mkubwa kulingana na mahitaji ya mkulima, ”anasema Radhiana.

Wasichana hawa wanasema ndani ya mashine kuna kifaa kinaitwa GSM ambacho kina uwezo wa kutoa taarifa kuwa dawa au maji yamekwisha kwenye tanki hata kama mkulima yuko mbali na mashine hiyo.

“Inaweza kutoa sauti kama uko mbali. Pia tumeweka kamera ya CCTV ambayo imeunganishwa na simu ya mkononi”anafafanua Amina.

Anasema mkulima anaweza kuwa mbali na eneo la shamba lakini kupitia kamera ya CCTV , mashine itamuonyesha kila kitu kinachoendelea shambani kupitia simu ya mkononi.

Wanasema mashine hiyo mbali na kutoa mlio pale maji au dawa inapokwisha, pia ina uwezo wa kusimama kufanya kazi yenyewe.

Lakini kama maji na dawa vipo itaendelea kufanya kazi mpaka pale mkulima mwenyewe atakapoona kuwa mazao yake yamekunywa maji ya kutosha.

Amina anasema mashine hiyo pia inapokuwa inafanya kazi zake za kumwagilia ikikutana na jiwe ama kisiki, ina uwezo wa kukwepa na kuendelea na kazi bila ya kutumia rimoti.

Kwa kutumia rimoti mkulima anaweza kuwa umekaa hata nyumbani au mbali na shamba lake, lakini ana uwezo wa kuibonyeza na kuielekeza. Inatumia umeme jua kufanya kazi zote hizo.

Wavumbuzi hawa wanasema mkulima au mtu yeyote anayehitaji, afike katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mtambo wa kufukuza ndege na wanyama waharibifu shambani

Huu ni mtambo wa kufukuza wanyama na ndege waharibifu wa mazao unaotumia kengele na sauti za ndege aina ya tai na wanyama kama mbwa.

Mtambo huo unatumia umeme jua na unaweza kuufunga shambani na kutegesha aina ya mlio unaotaka kulingana na aina ya wanyama na ndege ambao wanashambulia mazao yako.

Akielezea mtambo huo, mkufunzi wa wa Chuo cha Mafunzo na ufundi Stadi Mikumi(VETA), Ludovick Saronga anasema mtambo huo umetengenezwa kwa kutumia muundo wa ndege aina ya tai na una sauti za wanyama na ndege ambazo zinaogopewa na wanyama kama nyani, ngedere na ndege aina ya kolekole wanaoshambulia zaidi mazao kama mpunga, mahindi, mtama na viazi vitamu.

“Tumebuni mtambo huu ili kuwasaidia wakulima kuweza kuvuna mazao mengi, maana wengi wanashindwa kuvuna kwa wingi kutokana na mazao yao kuliwa na ndege na wanyama shambani,”anasema.

Saronga anasema mtambo huo unaweza kutoa sauti ya mbwa au ndege aina ya tai kulingana na mkulima atakavyotaka mweyewe. Mlio unaweza kulia muda wote au kwa saa kadhaa kulingana na mahitaji ya mhusika.

“Unaweza kuufunga shambani ukawa unalia muda wote au ukapangilia mwenyewe kulingana na unavyotaka. Mtambo huu unapatikana Veta Mikumi ikitokea mtu anahitaji afike chuoni ili aweze kutengenezewa na gharama za kutengeneza ni maelewano,”anasema Saronga .

Advertisement