Uelewa mdogo ‘waifinya’ nishati ya makaa ya mawe

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika ufunguzi ya wiki ya maonyesho ya nishati mbadala yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Mei, alitoa maelekezo kwa taasisi za umma na zile binafsi zianze kutumia nishati mbadala kwakuwa inapatikana nchini kwa nia ya kuokoa mazingira.

Pamoja na Serikali kuwa mstari wa mbele katika kampeni ya matumizi ya nishati mbadala kama makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia na kupunguza utowekaji wa misitu, lakini bado Watanzania wengi wana uelewa mdogo juu ya nishati hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika ufunguzi ya wiki ya maonyesho ya nishati mbadala yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam Mei, alitoa maelekezo kwa taasisi za umma na zile binafsi zianze kutumia nishati mbadala kwakuwa inapatikana nchini kwa nia ya kuokoa mazingira.

Mwananchi lilifuatilia maonyesho hayo na pia kupata fursa ya kutembelea Maonyesho ya 42 ya Saba Saba ambayo baadhi ya watengenezaji wa nishati mbadala nao walihudhuria, ikiwamo kampuni ya Kiasi Limited.

Katika maonyesho ya mwaka huu ya Nanenane kampuni ya Kiasi pia imeshiriki kunadi umuhimu wa nishati hii.

Mwananchi Ilipata fursa ya kuzumgumza na uongozi wa kampuni hiyo ambayo inazalisha mkaa unaotokana na makaa ya mawe, kama nishati mbadala wa kuni na mkaa wa kuni.

Meneja masoko na mauzo wa kiasi Ltd, Grayson Kavumo anasema mbali na tatizo la kukosekana kwa umeme wa kuendesha mashine za kuchakata bidhaa hizo katika kiwanda chao kilichopo Zogowale mkoani Pwani, kina tatizo kubwa la watu kutoelewa faida za matumizi ya nishati ya mkaa wa mawe ijulikanayo kwa jina la Coal Briquettes (Briketi).

Kavumo anasema kikwazo kikubwa cha kukuza mradi wao wa kuzalisha bidhaa nyingi zaidi za makaa ya mawe ya kupikia ili kukomesha matumizi ya mkaa wa kawaida unaoharibu misitu mingi hapa nchini.

Anasema kiwanda chao kina uwezo wa kuchakata tani 16 za briketi ndani ya saa 24, lakini bado wanachangamoto kubwa ya upanuzi wa soko kutokana na ufahamu finyu wa wananchi juu ya nishati hiyo,

Kwa mujibu wa takwimu za 2014 zilizoandaliwa na watafiti wa mamlaka ya misitu nchini, Tanzania Forestry Services (TFS), jiji la Dar es Salaam pekee lilitumia tani 500,000 za mkaa kwa 2014.

“Tumeanzisha kiwanda cha kuchakata nishati ya mkaa wa mawe hivi karibuni huko Kibaha katika Kijiji cha Zogowale, Pwani kwa kulenga soko kuu la jiji hili kubwa zaidi hapa nchini ambalo linategemea sana nishati yenye gharama kubwa ya matumizi ya mkaa wa miti na inayo teketeza miti na misitu,” anasema Kavumo.

Anasema nishati hiyo ni nafuu zaidi kulinganisha na mkaa wa miti au kuni.

“Watu wengi bado wanahofu juu ya ufanisi wa nishati hii ambayo ingewakomboa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha,” anasema na kusisitiza kuwa elimu kwa umma haijatolewa vya kutosha, inabidi iwe endelevu.

Kavumo anasema Kiasi Ltd itajikita zaidi katika kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi.

Anasema kiwanda chao kinazalisha bidhaa za aina mbili na zote zitauzwa kwa gharama ya Sh1,000 kwa kilo na zinapatikana kuanzia kilo moja na kuendelea.

Briketi kubwa zinatumika kwa ajili ya jumuiya mbalimbali kama vile shuleni, kwenye vyuo, magereza, kwenye migahawa, akina mamalishe na maeneo mengine yanayoandaa vyakula vya watu wengi.

Kuhusu faida zake, amezitaja sita, zikiwemo urafiki wa mazingira kwa kuzuia matumizi mengi ya misitu kutokana na kuni na kuhifadhi uoto asilia.

Faida ya pili ni kuokoa pesa nyingi zinazotumika kwenye nishati nyingine ghali. Faida ya nne ni mkaa wa mawe wa kupikia unadumu jikoni kwa muda mrefu kuliko mkaa wa miti hivyo kuzidi kupunguza gharama za matumizi nishati na maisha kwa ujumla.

Kwamujibu wa utafiti uliofanywa na wanasayansi hapa nchini, kilo moja ya briketi inatoa nishati jikoni si chini ya saa sita na kuendesha mapishi mbalimbali mfululilzo, anasema ofisa huyo wa kiasiLtd.

Faida ya tano ni kuboresha usafi wa jikoni na maeneo ya nyumbani yanayochafuliwa na mkaa wa miti.

Hata hivyo, vyombo vya kupikia vinanavyochafuliwa na mkaa wa msituni havichafuki kutokana na matumizi ya mkaa wa mawe,” anasema. Faida ya sita ni matumizi ya majivu ya mkaa huo kwa kurutubisha ardhi shambani, wanasayansi wamebainisha kuwa majivu ya mkaa wa mawe yanaviinilishe vya mimea, yakiwamo mazao mbalimbali yanayostawishwa na wakulima.

Mmoja wa watumiaji wa briketi ambaye ni mkazi wa Kimara, Dar es Salaam Elias Kimaro, anasema amevutiwa na matumizi ya briketi hasa zile pana za kilo moja kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake, zimpunguzia gharama kubwa.

“Pale nyumbani tunamia kwa miezi sita na wapishi wamefurahishwa jinsi mkaa huo unavyohifadhi moto mkali kwa muda mrefu wa takribani saa sita tunapikia maharage au kande na vyakula vingine,” anasema Kimaro.

Anasema familia yake imegundua kuwa matumizi ya gesi na mkaa wa miti unagharimu sana kuliko matumizi ya mkaa wa mawe.

Anasema mkaa wa mawe pia hudhibiti uchafu wa jikoni na ni rahisi kusafisha jiko bila gharama kubwa.

Takwimu zilizobainishwa na Mwananchi hivi karibuni juu ya gharama za nishati za kupikia, zinaonyesha gharama zifuatazo kulighana na matumizi yake;

Mkaa wa kuni wa Sh1,500 unatumika kupika kwa saa tatu tu na chakula cha kati ya watu watatu au mmoja tu.

Umeme wa Sh1,000 hauwezi kukidhi mahitaji ya chini kabisa ya kupikia.

Mafuta ya taa ya Sh2,100 kwa lita hayawezi kupikiwa kwa zaidi ya siku moja kwa milo yote.

Gesi ya petroli (LPG) inayouzwa Sh48,000 kwa mtungi wa kg47 inaweza kutumika peke yake kwa wiki mbili tu kwa mfululizo bila kuchanganya na nishati nyingine, hivyo kwa wastani kutumia sh4,000 kwa siku.

Mkaa wa mawe wa Sh1,000 unatumika kwa kwa siku bila kuhitaji nishati nyingine. Hivyo Sh48,000 zitumikazo kwa kununua LPG zinaweza kutumika kununua briketi kwa matumizi ya mwezi na zaidi ya nusu mwezi.

Mbali na manufaa hayo ya mkaa wa mawe, wanamazingira wameshabainisha kutoweka kwa misitu katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na matumizi ya miti kwa ajili ya nishati na shughuli za kiuchumi nyingine, pia wanasema matumizi ya makaa ya mawe kwa nishati ya kupikia yataokoa misiti mingi.

Ripoti ya wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka jana pia inaonesha kuwa Tanzania inapoteza hekta 370,000 za misitu kila mwaka.