Ununuzi wa umma unahitaji ufuatiliaji, usimamizi makini

Thursday October 25 2018Joseph  Mwacha

Joseph  Mwacha 

By Joseph Alphonce

Ununuzi wa umma ni nyenzo ya kurahisisha kufanikisha mipango ya maendeleo ya kitaifa. Usipofanywa kwa umakini unaohitajika, unaweza kudhoofisha jitihada hizo.

Taarifa zinaonesha changamoto zinazolikabili eneo la ununuzi wa umma katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kitaifa.

Kumbukumbu zinaonyesha matumizi ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa na huduma kwa umma hupewa kipaumbele cha kwanza baada ya mishahara ya watumishi.

Aidha, wastani wa asilimia 60 hadi 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kila mwaka kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa, zabuni za ujenzi na huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kati ya mwaka wa fedha wa 2007/08 hadi 2014/15 baadhi ya taasisi zilizokaguliwa zilitumia Sh30.787 trilioni kwa kipindi hicho cha miaka minane ambazo ni sawa na wastani wa Sh3.848 trilioni kwa mwaka.

Taarifa hiyo inathibitisha ukweli kuwa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali zinatumika katika ununuzi wa huduma na bidhaa mbalimbali kufanikisha malengo ya Serikali.

Pamoja na Serikali kutumia kiasi hicho cha fedha katika ununuzi, eneo hilo halikupewa kipaumbele kinachostahili kwa takriban miaka 35 iliyopita, kuanzia mwaka 1965.

Hadi mwaka 2000, Tanzania ilikuwa inatumia mwongozo wa ununuzi wa umma ulioridhiwa na Serikali ya kikoloni. Mwongozo huo haukuakisi mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia yaliyokuwa yakitokea hivyo baadhi ya watendaji wasio waaminifu kuutumia kuiingiza nchi katika ununuzi usio na tija.

Ili kuendana na kasi ya mabadiliko, Serikali iliachana na mwongozo huo na kutunga sheria kadhaa za ununuzi wa umma na ugavi ikiwamo sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2001, ya 2004, 2011 na 2016.

Kuanzia 2001 hadi 2018 kumefanyika mabadiliko ya sheria ya ununuzi wa umma mara nne. Mabadiliko hayo ya mara kwa mara pamoja na mambo mengine yanatokana na changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Natambua Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma inaendelea kuandaliwa ambayo itakuwa nyenzo muhimu kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.

Dira ya sera ya Taifa ya ununuzi wa umma inataja kujenga ushindani, usawa, uwazi, uwajibikaji na ubora wa kazi katika mfumo wa ununuzi wa umma nchini.

Pamoja na changamoto za ununuzi wa umma katika matumizi yasiyo sahihi ya gharama za huduma na bidhaa, muda, mawanda na ubora panahitajika kuwapo uzalendo kwa watumishi wanaosimamia eneo hilo.

Wakati anazindua Bunge la 11 mwaka 2016, Rais John Magufuli alisema haiwezakani kalamu inayouzwa Sh1,000 kwa wateja wengine wa kawaida inunuliwe kwa Sh10,000 kupitia ununuzi wa umma.

Tofauti ya Sh9,000 inaweza kutumika kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma maeneo mengine. Eneo la ununuzi wa umma halipaswi kuwa kichaka cha wizi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Ili kutekeleza hili kwa ufanisi, ni vyema Serikali ikatengeneza mfumo imara wa ufuatiliaji na usimamizi wa ununuzi wa umma. Aidha, taasisi yoyote ya Serikali isiruhusiwe kufanya ununuzi wa huduma au bidhaa bila kuhakikisha ina fedha ya kulipia huduma husika kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.

Kufanikisha haya yote, watendaji wa Serikali wanapaswa kuwa wazalendo, wenye kuipenda nchi yao na kutanguliza masilahi ya nchi mbele badala ya maslahi binafsi.

Hakuna linaloweza kufanikiwa endapo watu waliopewa dhamana ya kuongoza shughuli zake hawatakuwa tayari kuwatumikia wananchi. Mtumishi w aumma anayejali zaidi masilahi yake binafsi ana muda mdogo zaidi wa kuwahudumia wananchi.

Hata linapokuja suala la matumizi ya fedha, hawezi kuwa tayari kuzingatia vigezo vyote muhimu kuipata bidhaa au huduma yenye ubora uliokusudiwa ili anufaike yeye kwanza.

Taasisi za Serikali zishirikiane katika utekelezaji wa majukumu, kwa mfano, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) liutumie Wakala wa Taifa wa Majengo (TBA) katika ujenzi na mifano mingine inayofanana na hii. Serikali pia iweke viwango vya kutoa zabuni kwa wageni na wazawa. Pia, mikataba ya ununuzi kwa zabuni za huduma na bidhaa ibainishe rasilimali za kuagiza nje kwa lengo la kuimarisha viwanda na uchumi wa ndani.

Wajasiriamali wa ndani wakiwezeshwa kuzalisha bidhaa na huduma zenye ubora, watasaidia kuimarisha mzunguko wa fedha kwani mahitaji ya Serikali yatamalizwa nchini. Hili litasaidia kukuza ajira hivyo kuondoa umasikini uliopo kwa wananchi wengi.

Ushiriki wa wadau wote ni muhimu kufanikisha hili. Taasisi na mamlaka zilizopo zisaidie kuweka mazingira rafiki kwa zabuni nyingi kutekelezwa na wazawa isipokuwa kwa chache zinazohitaji utalaalamu ambao haupo nchini.

Fedha za umma zikitumiwa vyema, wananchi wengi zaidi watanufaika.

Advertisement