Upatikanaji wa mikopo kwa wahitimu vijana

Muktasari:

Kama mbadala wa kuajiriwa, baadhi hulazimika kujiajiri kama wajasiriamali. Hata hivyo wapo wale wanaoamua moja kwa moja kutoajiriwa na badala yake kujiajiri hata kama wanapata kazi za kuajiriwa.

Kutokana na hali ya soko la ajira kwa maana ya kuajiriwa kuwa ngumu, vijana wanaomaliza ngazi mbalimbali za elimu wanapata changamoto kubwa katika soko la ajira hasa ajira rasmi.

Kama mbadala wa kuajiriwa, baadhi hulazimika kujiajiri kama wajasiriamali. Hata hivyo wapo wale wanaoamua moja kwa moja kutoajiriwa na badala yake kujiajiri hata kama wanapata kazi za kuajiriwa.

Pia wapo wale ambao waliwahi kuajiriwa lakini kwa sababu mbalimbali wanaamua kujiajiri au kwa asilimia 100 au kuchanganya kuajiriwa na kujiajiri. Vijana wengi wanakumbana na changamoto kubwa katika azma yao ya kujiajiri. Kati ya changamoto kubwa ni ile ya upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya mitaji. Makala haya yanatoa mitizamo kadha wa kadha ya kiuchumi kuhusu upatikanaji wa mikopo kwa wahitimu vijana.

Kundi la vijana

Kati ya maswali ya msingi katika suala la upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali ni kwa nini kujikita katika kundi la vijana.

Kundi hili ni kubwa sana katika idadi ya watu nchini. Kama ilivyo katika nchi kadhaa zinazoendelea, Tanzania ni nchi yenye kundi kubwa la vijana. Vijana ni jeshi kubwa lenye nguvu nyingi, ubunifu mwingi, mitizamo mingi katika mambo kadhaa na ni rasilimali watu kubwa na muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Kwa bahati mbaya kundi hili lina changamoto kubwa zaidi katika soko la ajira kuliko kundi la wasio vijana. Katika muktadha wa upatikanaji wa mitaji kundi la wajasiriamali vijana lina changamoto nyingi na kubwa. Changamoto hizi zinasimama kati ya vijana wajasiriamali kwa upande mmoja na fursa kadhaa za ujasiriamali kwa upande mwingine.

Mahitaji ya mitaji

Wajasiriamali wengi wanahitaji mikopo. Hii ni muhimu kwa ajili ya kulipa gharama ya mambo kadha wa kadha katika shughuli za kijasiriamali. Shughuli hizi zinaweza kuwa ni pamoja na kuanza biashara kwa maana pana. Biashara zinaweza kuanzishwa katika hatua mbalimbali.

Hatua zote hizi hugharimu fedha hivyo kufanya wajasiriamali kuhitaji mitaji. Mitaji inaweza kuhitajika ili kulipia gharama kama vile za mpango wa biashara kwa mapana yake, eneo la kufanyia biashara kwa mapana yake, malighafi, wafanya kazi, usafiri, vibali na kadhalika. Kwa wajasiriamali wanaoanza, mitaji ni muhimu sana katika kutoka katika hatua ya mawazo, mipango, matamanio na njozi kwenda katika utekelezaji. Kwa waliopo katika ujasiriamali tayari, mitaji ni muhimu katika kuendeleza kilichopo na kukikuza katika hatua nyingine kubwa zaidi.

Changamoto kwa vijana

Japokuwa wajasiriamali wote wana changamoto ya kupata mitaji katika ujumla wake, kundi la vijana lina changamoto za ziada. Hizi ni changamoto zinazotokana na wao kuwa vijana. Baadhi ya changamoto zinatoka katika upande wa ugavi wa uchumi kwa maana ya vyombo vya fedha na baadhi zinatoka katika upande wa uhitaji wa soko kwa maana ya vijana wenyewe.

Nini muhimu kuainisha na kuchambua changamoto hizi ili kupata suluhisho sahihi. Kati ya changamoto zinazotokana na taaisi za fedha zenye kutoa mikopo ni masharti ya mikopo husika.

Wakopeshaji

Ni muhimu kuelewa kuwa vyombo vingi vya fedha vinavyokopesha vipo kufanya biashara. Ni lazima kukidhi mahitaji ya kimsingi ya kibiashara na yale ya mamlaka thibiti kama vile benki kuu.

Hata hivyo inabaki kuwa kweli kuwa masharti haya yanakuwa changamoto kwa wajasiriamali hasa vijana kwa ujumla na wale wanaotaka kuanza ujasiriamali kwa mara ya kwanza kimahususi.

Masharti haya ni pamoja na kuwa katika sekta rasmi kwa maana ya kuwa na leseni na vibali vya biashara, kuwa na sehemu maalumu na anwani ya mahali pa kufanyia biashahara, kuwa na biashara inayoendelea kwa maana kuwa mikopo kwa ajili ya kuanzisha biashara ni nadra kupatikana, kuwa na kumbukumbu za taarifa rasmi zikiwemo za ukaguzi na malipo ya kodi kwa kipindi fulani, kuwa na mali isiyohamishika kama dhamana, kuwa na wadhamini na kadhalika. Pia vyombo kahaa vya fedha huepuka kukopesha wajasiriamali katika sekta ya kilimo kwa maana ya kulima mazao japo viko tayari kukopesha kwa ajili ya biashara ya mazao. Vijana wengi hawakidhi vigezo tajwa hapo juu. Hivyo ndoto za kujiajiri kama wajasiriamali zinaweza kwisha. Ndoto hizi zinapokwisha maana yake ni kuwa faida zinazotokana na ujasiriamali kama vile ajira, mapato ya serikali, ukuaji uchumi na kupunguza umasikini nazo zinapotea.

Changamoto kutoka kwa vijana

Kimsingi, masharti tajwa katika haya hapo juu yanawahusu wakopaji wote bila kujali umri. Katika muktadha wa makala haya, changamoto zinakuwa kubwa na nzito zaidi kwa vijana kwa sababu ya hali zao.

Kwa vijana waliomaliza ngazi mbalimbali za elimu kanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu ni nadra kukudhi vigezo na masharti ya mikopo kutoka vyombo vya fedha hasa vilivyojikita zaidi katika biashara na faida.

Vijana wengi hawana mali zisizohamishika kama vile nyumba na ardhi.

Ni kweli pia kuwa hawana hata mali zinazoamishika kama magari. Kwa kijana anayetaka kuanza biashara kwa mara ya kwanza hatakuwa na taarifa za nyuma za biashara na mahesabu yaliyo kaguliwa. Vijana wengi hawana makazi ya kudumu na anwani ya kudumu. Bado ni watafutaji na pengine wanapomaliza elimu katika ngazi mbalimbali huama kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine. Hapa wanapoteza sifa ya kuwa katika anwani maalumu kwa muda mrefu. Maana yake ni pamoja na kukosa mitandao na mitaji ya kijamii kama taasisi, marafiki na watu wanaoaminika, kufahamika na kuheshimika. Mitandao na mitaji hii ya kijamii ni pamoja na serikali za mitaa, viongozi wa dini na makundi kadhaa ya kiuchumi na kijamii.

Nini Cha Kufanya

Ni muhimu sana kila mdau atekeleze wajibu wake katika kufanya upatikanaji wa mitaji kwa vijana wajasiriamali kuwa rahisi zaidi. Vyombo vya fedha lazima vifikirie tofauti na kuona vijana kama fursa ya wateja badala ya kuonekana kama tishio. Lazima view na ubunifu na utayari wa kuwa na vigezo mbadala vya kutoa mikopo ikiwemo kutoa mikopo ya vitendea kazi vitakavyokuwa dhamana.