Zaidi ya Sh600 milioni zimegharama kesi ya makinikia mwaka jana

Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James

Muktasari:

  • Sakata la kuzuia usafirishaji wa makinikia lilisababisha Serikali kushtakiwa kutokana na hali hiyo, imelazimika kuuwatuma mawakili wake kwa ajili ya kuitetea. Kati ya Julai na Desemba mwaka jana Serikali ilitenga zaidi ya Sh612 milioni kugharamia kesi hiyo.

Dar es Salaam. Kwa miezi sita iliyopita, Serikali ilitenga zaidi ya Sh612.86 milioni kuendesha kesi iliyotokana na zuio la usafirishaji wa makinikia lililolitoa dhidi ya kampuni ya Acacia.

Itakumbukwa, Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini uliokuwa unafanywa na kampuni hiyo mwaka 2017 jambo lililolalamikiwa na mchimbaji huyo kiasi ili kulinda masilahi yake.

Ingawa majadiliano bado yanaendelea baina ya Serikali na kampuni mama ya Barrick, kesi dhidi ya zuio hilo bado inaendelea na taarifa ya mabadiliko ya matumizi ya Serikali kw akipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2018 inaonyesha kutengwa kwa kiasi hicho.

Katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amethibitisha kutolewa kwa fedha hizo. “Waziri wa Fedha ndiye mwenye mamlaka ya kuidhinisha kiasi chochote kinachoombwa na ofisi yoyote ya umma. Akijiridhisha na sababu zilizotolewa, fedha huwa zinatoka,” amesema Dotto.

Kabla ya kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini, Serikali ilifanya uchunguzi kwa Rais Johnh Magufuli kuunda kamati maalumu ambayo iligundua kampuni nyingi za uchimbaji madini hazijalipa kodi na ushuru mbalimbali unaotakiwa kwa muda mrefu.

Kwenye orodha hiyo, Acacia ilikuwamo na ikatakiwa kulipa kodi na faini zake ambazo jumla yake ni Dola 190 bilioni (zaidi ya Sh418 trilioni). Hata hivyo, mazungumzo kati ya Serikali na Barrick bado yanaendelea kupata muafaka wa faini hiyo.

Mwanaharakati wa haki za binadamu na mwanasheria nguli nchini, Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema mazungumzo yanayoendelea yamekuwa siri kubwa ingawa wananchi wangependa kufahamu kinachojadiliwa.

Akizungumzia gharama za kesi hiyo, amesema umakini zaidi unahitajika Serikali inapotaka kufanya mabadiliko kwenye mikataba iliyopo.

“Kuendesha kesi ni gharama kubwa ndio maana huwa inashauriwa kumalizana nje ya mahakama. Hata hivyo hatukuwa na sababu ya kufanya uamuzi uliotufikisha apa. Kila mkataba unachokipengele kinachoruhusu kufanya mabadiliko pindi yanapohitajika ni suala la kuzingatia kipengele hicho na kukifuata,” anasema Dk Hellen.

Mkurugenzi mtendaji wa Repoa, Dk Domald Mmari anasema kila Taifa linawajibika kulind arasilimali zake kwa gharama yoyote ile kwa kufuata sheria na mikataba ya kimataifa kuepuka kupata hasara.

“Kupigania mali na rasilimali ni kipaumbele cha nchi yeyote. Hata Canada imefanya hivyo kwa kuipitia mikataba na wawekezaji iliowakaribisha,” amesema.