Kitwana Manara: Bibi alinipeleka Yanga

Muktasari:

Mkongwe anafichua kuwa licha ya kucheza kama kipa, kwenye klabu yake, Yanga lakini alibadili maisha ya soka akiwa mshambuliaji wa kati.

Manara, wengi wakiwamo mashabiki wa soka hasa wa siku hizi wanamtambua kama mshambuliaji mahiri wa miaka ile.

Lakini, kumbe Kitwana ndiye aliyekuwa kipa wa kwanza wa timu ya Taifa  ya Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961.

Mkongwe anafichua kuwa licha ya kucheza kama kipa, kwenye klabu yake, Yanga lakini alibadili maisha ya soka akiwa mshambuliaji wa kati.

Mchezaji huyo mwenye historia katika soka la Tanzania anasema kuwa awali hakuipenda Yanga, bali mapenzi yake yalikuwa Cosmopolitan, timu iliyomuibua na kumfanya  awe Mtanzania wa kwanza kucheza soka ya kulipwa.

Wazee wakutana, bibi aingilia kati usajili Yanga

“Nilikuwa nachezea timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL) kabla ya kujiunga Yanga, nilicheza kwa mafanikio kule, niliporudi likizo bibi yangu mzaa mama, aliiitwa kwa jina la Salma binti Zuma alinikalisha chini na kutaka nirudi nyumbani nikaichezee Yanga.

“Bibi alifanya hivyo baada ya kikao chake na wazee wa Yanga ambao walimfuata na kutaka mimi nichezee timu yao, usajili wa zamani mchezaji ulikuwa hufuatwi, bali wazee wa Yanga wanawaendea wazazi wa mchezaji husika na kuwaomba mtoto wao aichezee timu yao,” anasema Manara.

Anasema wazee wa pande zote mbili wakikubaliana, basi mchezaji huwezi kupinga, unaitwa na kuambiwa ujiunge na timu na hivyo ndivyo lilivyotokea kwake kujiunga Yanga  iliyokuwa ikiendeshwa kwa michango ya wananchi, ambao ni wanachama.

“Bibi alikuwa ana mapenzi na Yanga, mimi kwa wakati huo sikuwa naipenda Yanga, niliipenda Cosmopolitan, baada ya yeye (bibi) kuzungumza na wazee alinifuata na kuniambai inabidi nijiunge na Yanga.

“Kwa kweli nilisajiliwa Yanga kwa busara za bibi yangu na wazee wa klabu hiyo ambao walizungumza, nami nikapewa taarifa  za mazungumzo yao ambapo nilitakiwa kutii maagizo ya wazee.

“Usajili wa wakati ule haukuwa na fedha na ulifanyika kila baada ya msimu, huo ndio ulikuwa utaratibu wa usajili wa zamani ambapo wachezaji walisajiliwa upya kila baada ya mwaka mmoja, hakukuwa na mkataba wa kuzidi mwaka,” anasema.

Anaongeza kuwa licha ya kutokuwa na fedha za usajili zaidi ya busara za wazee, unaposaini kuitumikia Yanga, maisha yako yanakuwa ya klabuni ambapo huduma zote kama usafiri, chakula na gharama za matibabu na nyumba unagharamiwa na wanachama.

“Sharti jingine lilikuwa huwezi kusajiliwa na kuwa mchezaji wa Yanga kama siyo mwanachama, waliamini kama utakuwa ni mwanachama basi utacheza kwa juhudi, ukiamini Yanga ni mali yako hivyo na yeye akajiunga na uanachama wa Yanga katika msimu wa 1966/1967,” anasema Manara.

 

Manara apewa jina baharini

Kitwana Manara alijulikana zaidi kwa jina la utani la Popat, anasema jina hili alipewa baharini na raia wa India aliokuwa akikutana nao katika eneo hilo.

“Mazoezi ya kipa nilipenda kwenda kufanyia kando ya bahari, mara kwa mara huko nilikutana na Wahindi waliokwenda kupumzika, hivyo wakanizoea na kunipa jina la Popat ambalo kwa lugha yao ni maji,” anasema.

Anasema alipewa jina hilo baada ya kuonekana akijifua baharini peke yake, hivyo kudhani kuwa anapenda kuona maji na siku moja walimfuta na kumwitia Popat ‘Bwana Maji’, hivyo jina hilo likazoeleka na kuamua kulitumia kama jina lake la utani.

Uchawi ulivyofanyika kwenye soka

“Uchawi ni imani, hata sasa mambo hayo yanafanyika, tofauti na zamani wanaofanya, hivyo sasa wanavaa suti, ilikuwa ni kawaida watu kuamini hawawezi kucheza bila kuloga, kuna waliofanya hivyo na wakashinda hivyo kuamini lakini kama huna mazoezi hata ubebe hirizi, kibuyu na vitu vingine mpira aulogeki.

“Zamani timu hazikucheza bila kuroga, kuna mechi tulizoshinda na kuna nyingine tulifungwa, ingawa uchawi wa zamani ulionekana wazi kwani atatokea mtu kavaa kaniki, kashika kibuyu, tofauti na huu wa sasa ambapo mtu anayeroga hajulikani kwani sasa wanavaa suti.”

Aondoka Yanga kwa mizengwe

Mwaka 1975, Manara aliondoka Yanga, anasema aliamua kuihama timu hiyo baada ya mgogoro uliotokea ambapo baadhi ya wachezaji akiwamo yeye kutuhumiwa kuihujumu timu kufuatia matokeo ya sare ya 0-0 kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika katika mojawapo ya mechi na timu ya Nigeria nchini humo,  kisha kutoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya maruadiano jijini Dar es Salaam.

“Ile timu ya Nigeria ilisonga mbele kwa faida ya goli la ugenini, pale ndipo mizengwe ikaanza, akatafutwa ‘mchawi’, hivyo nikaondoka na baadhi ya wachezaji tukaenda kuanzisha timu ya Pan African.

“Baada ya miezi kadhaa wazee wa Yanga walinifuata na kunishawishi nirudi, sikuona sababu ya kukataa,  nikafanya hivyo, niliendelea kuichezea timu hiyo hadi nastaafu kucheza soka mwaka 1986 sikuwahi kuihama tena Yanga.

Kwanini aliamua kucheza namba tofauti Stars na Yanga

Manara akiwa Yanga alicheza kama mshambuliaji wa kati, akivaa jezi namba tisa, lakini kwenye timu ya taifa alicheza kama kipa ambapo alivaa jezi namba moja.

“Sikuwahi kucheza Yanga kama kipa, vivyo hivyo kwa Taifa Stars sikuwahi kucheza kama mshambuliaji, nikiitwa stars nacheza kama kipa  na nikirudi mimi ni mshambuliaji,” anasema Manara.

Anasema alianza kujifunza kucheza namba nyingi uwanjani tangu akiwa shule ya msingi, hivyo kuzoea kucheza nafasi tofauti tofauti ndani ya uwanja na kuamua kucheza kama mshambuliaji kwenye klabu ya Yanga na kuwa kipa kwenye timu ya taifa kwani zote alizimudu.

“Nilicheza namba tofauti kwa kuwa nilipenda kubadilika na kujua vitu vingi hivyo mbali na kuwa kipa na mshambuliaji kuna wakati nilicheza pia namba 5 ingawa namba hii sikuitilia mkazo,” anasema.

Historia ya Kitwana Manara

Manara aliyezaliwa Mei 5, 1941, mkoani Kigoma anasema alianza kujifunza kucheza soka akiwa shule ya Msingi Mchikichini  mwaka 1951,  baada ya kuhamia Dar es Salaam kuishi na mama yake aliyetengana na baba yake 1945, ambapo mwaka 1960 alijiunga na timu ya Cosmopolitan kabla ya kuihama na kujiunga na TPC ya Moshi mwaka uliofuatia.

Manara anasema yeye ni baba wa watoto wanane na mtoto wa pili kuzaliwa kati ya sita kwenye familia ya Ramadhan Manara, amewahi kuwa kocha mchezaji wa Yanga kabla ya kustaafu soka mwaka 1986 na kuwa katibu mwenezi wa Yanga, ingawa sasa amestaafu kujihusisha na masuala ya soka na anaendelea na maisha yake binafsi, maeneo ya Tabata Barakuda, jijini Dar e