Ninogeshe ya Nandy na hali halisi

Saturday June 30 2018

 

By Dk Levy

“Aai ni wewe ubavu wangu mwenyewe,

Ukifa nizikwe na wewe, nikifa uzikwe na mie

Oh baby wee...”

Umemsikiliza huyu Nandy kwenye wimbo huu? Maneno mazuri na sauti yake kindandanda haswa na watu hasa jinsia ya kike wanapenda sana.

Siyo yeye kina dada wengi na wavulana kibao wanaimba nyimbo za mahaba. Lakini kwenye uhalisia wao wenyewe na wanaowaimbia ni tofauti kabisa. Inashangaza sana.

Kuna wakati unamsikiliza Diamond na wenzake kwenye nyimbo za mapenzi kama “Ukimuona” na maisha yao halisi. Unaweza kudhani walipata tenda tu ya kuwaimbia watu wa sayari nyingine siyo hawa wa nchi hii.

Mwanamke kutwa unalalamika wanaume waongo kwenye mapenzi wakikutumia tu wanasepa, huna hata akili ya kufikiria kwa nini kwako wagonge na kusepa bila kuingia ndani?

Unahudhuria harusi za wasichana wenzio wakiolewa? Au wao wanaolewa na majini eti? Si ni wanaume hawa hawa unaopishana nao kwenye foleni mjini, bank, kwenye mabaa mitaa ya Sinza, Tabata na kwingineko?

“Aaah kwachukwachu kushea na watu sitaaki,

Ooh baby...

Bodaboda yangu vipi nipande mishikaki

Siwezi...”

Haya maneno ya Nandy sidhani kama yanawalenga hawa wasichana wa kujiona wa mjini, wa kisasa sijui, wanakuwa kama makuku ya kisasa kweli hayafai kwa kufugwa shida tupu.

Maana kuku wa kisasa ukitaka kuwafuga basi ujipange kuanzia mtaji wa kipesa hadi muda wa kuyahudumia. Huo muda wa kunogeshana hawana wanaitwa CCS. Yaani kirefu chake ni “Chukua Chako Sepa.”

Madem wa siku hizi hata ladha imeisha kabisa wewe unataka mwanaume akuoe wakati hujawahi kujiongeza hata kusema umfulie, kazi kumsifia kapendeza hujui hata anafuliwa na nani?

Hujawahi hata kumpikia kazi kumsifia ananenepa hujui hata anakula wapi, halafu unataka ndoa? Kila siku ukienda kwake kazi kuulizia ‘sirizi’ za Kikorea kama kaleta mpya, huulizi hata leo unanunua mboga gani nije kukupikia.

Mtoto wa kike bila haya unaenda kwa mchumba unafika na kulia njaa halafu unamuagiza akakununulie chips kuku. Kisha unataka atoe posa kwenu? Labda atoe kosa siyo posa.

“Unanipaga furaha hivi,

Ukiniacha utanipa jaka la roho...

Nipe mimi kwingine we useme no..

Ishinde ibilisi kwenye kichwa chako ooohoo.”

Haya maneno ya Nandy ni tofauti na fikra za madem wa mjini wa sasa. Wanachojua ni kuomba hela kama watoza ushuru wa manispaa.

Wakifulia wanajifanya kusema “Bby nimekumis nataka nije leo...” Kumbe pesa ndo inayokupeleka. Hata kilio cha kusalitiwa kwao siyo penzi bali ni mgao wa kipato kupungua. Kuna wasichana wako radhi kushea bwana mradi anapewa pesa ya kula tu.

Wakishashea mashuka na bwana fasta kuomba nauli na hela ya kula hata kukumbuka kutoa shuka atandike lingine hana muda, kudanga imekuwa kama kawa, wengi wao wasipodanga na kunywa mapombe basi ujue huyo mchawi.

Haya mambo mnayaona ya kipuuzi lakini ndo uchawi kwa mwanaume ajue thamani yako, asifikirie kukupoteza hata siku moja. Lakini hawa kina hawa wa sasa wao wanaona kudanga na kushinda baa ni jambo la maana. Wanaingiza hesabu kwa madanga kama daladala.

Sasa nyie endeleeni tu kufuata hela, mnaenda kwa wanaume mmejikoki marangi kama sadolin mdomoni, machoni mpaka mtu anashindwa kukukis. Hana muda wa kunogesha kama Nandy anavyotaka kutuaminisha.

Umefuga kucha kama visu vya kukeketea. Mnasafishaje? Mnachoweza ni kisafisha picha na kuziediti ili mtupie instagram. Na huko insta na kwenda ‘grupu’ za what’sApp ni eneo tengefu la kudanga mjini.

Unakuta anang’aa usoni utadhani duka la ‘Wahindi’ lakini ndani ya mwili na roho ni uvundo mtupu, hana haya wala soni. Hadharani anaropoka utadhani mpiga debe au muuza dawa ya mba upele mapunyee sumu ya panya.

“Mi mwenzako mkiwa baba...

Mkiwa wa wapenzi baba

Usinione nalia sana,

Nalilia mapenzi...

Chochote utachoniambia (sawa)

Mimi nitaridhia baba

Hata ukiwa mbali nitasubiria...”

Nandy hapa hawaimbii wenzake wanaomzunguka Bongo hii. Kawaimbia watu wa dunia anayoijua yeye. Wapenzi hawasikilizani wala kuvumiliana kwenye jamii tuliyopo.

Imefikia hatua kwamba ili uishi kwa amani na mke au mpenzi wako. Basi iwe mguu kwa mguu kama Chama na Mogella. Mume anaishi Mwanza mke anaishi Mtwara halafu mnasema mmeoana? Unachekesha, hiyo ilikuwa zamani.

Na si kwamba zamani dunia ilikuwa takatifu. Kumbuka Eva alirubuniwa na nyoka baada ya kuona Adam ametoka. Eva angekuwa na mumewe kando yake nyoka asingemsogelea na kumdanganya.

Kuna mambo mengine mkiwa mnaishi pamoja mke na mume shetani hawezi kuthubutu kuyaleta ila kule kutengana shetani anapata mwanya wa kuwajaribu. Ndoa nyingi zimepigwa chini kwa jinsi hii.

Nioneshe aliyewahi kuthamini ajira kuliko ndoa halafu ndoa ikabaki salama kwa muda mrefu. Mnaweza kusema tunaaminiana, mara ohooo, mke wangu/mume wangu hawezi kunisaliti. Mmekutana ukubwani mkiwa mmebalehe nakuvunja ungo halafu unaleta stori za tunaaminiana?

Maombi yanaweza kuhamisha kitu, lakini kuna mambo mwilini hayahami kwa maombi. Wewe umekomaa na ajira Mwanza mumeo yuko Dar, halafu unategemea maombi ya Nabii Tito, eti Mungu amlinde mumeo kule Dar? Subiri uvune mabua, ndio utaelewa!

Aliyewaambia mmoja akiacha ajira kumfuata mwingine mtakufa na njaa nani? Shida ni kwamba mkielezwa juu ya ujasiriamali mnaona kama hayawahusu, ndio maana mnatetemekea ajira kiasi cha kupuuza ndoa zenu.

“Tusiwe Tyson na Evander kisa kosa...

(Kupendana na wewe)

Presha kupanda kushuka kisa nini?

(Kupendana na wewe)

Mi mwenzako nakupenda nafurahi...

(Kupendana na wewe)

Nivike pete ya roho isiyotoka, mmmh!”

Huko Dodoma mchunga kondoo wa bwana alimcharanga mapanga mkewe mpaka kufariki juzi juzi tu kisa mapenzi.

Na wakati wa mazishi ya mkewe mchunga kondoo mwingine aliyeendesha misa ya mazishi akaomba wanandoa kuachana haraka mambo yanapokuwa hovyo, badala ya kusubiri watu watangulizane kuzimu. Siyo kufa kuzikana hivi sasa ni kufa bila kuzikana.

Wasichana wa mjini wana machaguzi sana, na machaguzi yao hayana msingi. Mwanaume huwezi kumridhisha mwanamke wa mjini kwa kila kitu.

Wanatamaa sana na kila kizuri wanataka kuwa nacho.

Huwezi kuwa handsome, ‘gentlomani’, pia ukawa na ‘six packs’ halafu una digrii, hapo hapo ukawa na pesa nyingi, mrefu mweusi mwenye misuli halafu hapo hapo ukawa mrefu mweupe na gari zuri na ajira yenye kipato kikubwa.

Wanawake wanaumizwa kimapenzi kwa kuchagua chagua sana. Ndo maana wanaume tumeambiwa tuishi nao kwa akili. Usimpende sana utaumia wala usimchukie maana wana umuhimu kwetu, ila kwenye mapenzi tanguliza akili siyo moyo.

Wasichana wengi wa mjini ni wale wa kampani tu. Mwanamke wa kweli anajua six packs hazileti kitu mezani. Wapo wanaoridhika na jinsi mwanaume alivyo na kumpenda hivyo hivyo.

Kama ilivyo tofauti kati ya mwanaume na mvulana, mwanamke makini ni mbeba maono, hawezi hadaika na vipande sita vya kifua cha mwanaume, umbo, elimu au swaga.

Lazima ajue anataka nini na nini anastahili katika maisha. Kuna vitu ni ziada tu na siyo muhimu katika maisha. Lakini hawa wa Ninogeshe anaowaimbia Nandy na wenzake ni ngumu sana kuelewa haya mambo.

Mwanamke ni kiti cha shetani, kumbuka shetani alihangaika na Adam akamshindwa na kwenda kwa Eva mambo yakawa rahisi. Shetani amewekeza kwa mwanamke ili aikamate dunia.

Bob Marley alisema, “Bila uwepo wa mwanamke kusingekuwa na kilio,” hili fumbo lina maana kubwa sana. Wanawake kiasili wanapenda kwa hisia hawa wa leo wanapenda kwa macho kwenye mifuko ya mwanaume.

Ukifikiria kwa kina hizi nyimbo wanazoimba kina Nandy na wenzao ni nzuri sana. Zina ujumbe wenye maana kubwa sana, lakini walengwa wa nyimbo hizo siyo hawa tunaoishi nao mitaani.

Ni ngumu sana kumridhisha binadamu. Jangalie vizuri kwa kioo. Siyo kazi ya mwanamke pekee kukupa urahisi wa kumuelewa na kufanya maisha yako yawe rahisi, wewe pia inakupasa uhangaike kuhakikisha unamuelewa.

Ukiona huwaelewi wanawake ujue wewe ndio mwenye kosa na sio mwanamke. Unaweza kuwa unakosea kuchagua aina ya mwanamke wa kuwa naye kwenye uhusiano au umekataa kumuelewa huyo mwanamke anachotaka.

Kwa hiyo basi kosa ni lako, hakikisha unachagua kilicho bora, vile vile uhakikishe wewe ni bora pia, ndiyo utapata mwanamke bora. Kivipi “Ninogeshe” wakati wengi wao ni “Kivuruge” tu?

Advertisement