MAONI YA MHARIRI: Polisi wajifunze kesi dhidi ya Nondo

Hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa iliyomuachia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TSNP), Abdul Nondo imefichua namna Jeshi la Polisi linavyodaiwa kuwaonea raia kwa kuwageuzia kibao au kuwabambikia kesi.

Tunaungana na Hakimu Chamshana Liad kuwashangaa polisi kwamba, inakuwaje mtu anayekwenda kituoni kulalamika kutendewa jinai wao wanamgeuza mtuhumiwa.

Mshangao mwingine ulionyeshwa na Hakimu Liad inakuwaje polisi badala ya kupeleleza malalamiko yaliyowasilishwa kituoni, wao wanamgeuzia kibao mlalamikaji na kumgeuza mtuhumiwa kabla hata ya kumfikisha mahakamani.

Ukifuatilia kesi ya Nondo ilikoanzia utaona namna gani Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza jukumu lake la kusimamia usalama wa raia na mali zao.

Machi 7, zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ametekwa na watu wasiojulikana na alituma ujumbe kwa wanafunzi wenzake akiwaeleza yuko kwenye hatari kubwa.

Wanafunzi wenzake walitoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam wakieleza kupokea ujumbe kutoka kwa Nondo kwamba, yuko kwenye hatari. Machi 8, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa lilitoa taarifa kwamba Nondo alipatikana Machi 7, saa moja asubuhi baada ya kufika Kituo Kidogo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi na kueleza kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Hata hivyo, mkanganyiko kuhusu kesi hiyo ulianza pale Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa walipotoa taarifa ya kumsafirisha Nondo kwenda Dar es Salaam kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuhojiwa juu ya madai yake ya kutekwa.

Mkanganyiko huo wa polisi na hoja zilizotolewa na Hakimu Liad ni wazi kuwa jeshi hilo linatakiwa kubadilika katika utendaji wake wa kazi.

Hatuoni mantiki ya polisi kumgeuza raia aliyelalamika kuwa mtuhumiwa kabla hata ya kumfikisha mahakamani. Tunajiuliza ni raia gani atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi ambayo inatia shaka katika utendaji wake.

Pia, tunajiuliza kama suala la kugeuziwa kibao lililotokea kwa Nondo, ni raia wema wangapi wamekuwa wakigeuziwa kibao na polisi katika mtindo huo na wangapi wamekwenda jela kwa tuhuma zisizowahusu?

Lakini, tunachoona kwa upande wa Nondo ni kwa vile alikuwa na mawakili waliokuwa wakimtetea. Je, hali ikoje kwa raia wengine wasiokuwa na uwezo wa kuweka mawakili wa kuwatetea mahakamani?

Tumesikia matamko mengi kutoka kwa viongozi wa juu ndani ya Jeshi la Polisi; Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na watangulizi wake, lakini tunaona hayatoshi kulifanya jeshi hilo liendelee kuonekana kufanya kazi kizamani, huku likiandamwa na lawama za namna hii.

Pia, tunaendelea kujiuliza ni Watanzania wangapi maskini wamehukumiwa vifungo jela au kupewa adhabu yoyote mahakamani kutokana na tabia ya baadhi ya polisi ya kubambikia kesi au kuwageuzia kibao. Tunajiuliza kama hili la Nondo limetokea hata baada ya onyo la viongozi wao, ni Watanzania wangapi wameendelea kuteseka na tabia hiyo? Kwa maana hiyo, raia watakuwa na ari ya kuviona vituo vya polisi ni rafiki kwao?

Rai yetu umefika wakati viongozi wetu hasa wanaotoa matamko ya kukemea pale askari wanapokosea, wachukue hatua stahiki na wananchi watangaziwe hatua zilizochukuliwa.