BAADA YA KUINGIA MADARAKANI: Maeneo 10 ya kuboreshwa na mkurugenzi mpya CRDB

Mkurugenzi wa benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela

Muktasari:

Mkurugenzi mpya wa Benki ya CRDB anarithi uongozi wa taasisi hiyo ikiwa na faida ya Sh32.4 bilioni. Kuna mambo 10 anapaswa kuyaboresha kuhakikisha inaendelea kupata faida kwa miaka mingi ijayo.

Mwezi mmoja tangu Abdulmajid Nsekela ateuliwe kuwa mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, amrithi faida ya Sh32.4 bilioni kabla ya kodi iliyopatikana kwenye robo iliyoishia Septemba 30.

Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 62 ikilinganishwa na iliyopatikana kipindi kama hicho mwaka jana au asilimia 16.2 kwa robo iliyoishia Juni ilipopata Sh27.867 bilioni.

Kwa kiasi hicho, CRDB inakuwa imetengeneza faida ya Sh76.2 bilioni kabla ya kodi kwa miezi tisa ya kwanza mwaka huu iliyotokana na ongezeko la mapato ya riba na ada na kamisheni.

Nsekela anachukua mikoba ya kuiongoza benki hiyo kipindi mbacho uwiano wa mikopo chechefu umepungua kutoka asilimia 13.1 mpaka asilimia 8.9 ikilinganishwa na robo iliyopita.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Profesa Haji Semboja anasema kuyaendeleza mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa, menejimenti inapaswa kujikita kwenye mipango endelevu itakayokuwa jumuishi miongoni mwao. “Kwa muda mrefu benki ilikuwa imejiweka kando na siasa. Mkurugenzi mpya naye azingatie hilo, wanasiasa hupenda kufanikisha malengo yao ya muda mfupi,” anasema Profesa Semboja.

Damu hiyo mpya imeipokea taasisi ambayo kwa miongo miwili iliyopita imekuza mali zake mpaka Sh5.9 trilioni huku ikipokea amana za wateja kiasi cha Sh4.5 trilioni na kutoa mikopo ya Sh3.09 trilioni. Mwaka mmoja baada ya Nsekela kuondoka, Juni 2009, CRDB iliorodheshwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Miaka 10 baadaye, Nsekela anaipokea CRDB iliyosambaa nchi nzima ikiwa na mashine 551 za kutolea fedha (ATM) na vituo 1,184 vya mauzo. Ikitoa huduma kwa saa 24 kwa Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa huku ikipata faida na kutoa gawio kwa miaka kadhaa mfululizo.

Kwenye mkutano mkuu wa mwaka 2010, mkurugenzi mtendaji mstaafu, Dk Charles Kimei alisema benki hiyo ni imara kutokana na wafanyakazi waliojitoa na uongozi jadidi.

Mwaka mmoja baada ya kuorodheshwa DSE, dira ya Dk Kimei ilikuwa kuifanya CRDB kuwa benki inayoongoza sokoni kwa kuwaunganisha wafanyakazi wake kote nchini. Alitaka kuona wafanyakazi wanaamini CRDB ni sehemu nzuri kufanya kazi na viongozi wa kijamii, Serikali na wadau wengine kuitambua kuwa ni mshirika muhimu wa maendeleo.

“Hivyo ndivyo ninavyomaanisha ninapoizungumzia CRDB, benki inayoongoza nchini. Ninaahidi tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunatunza heshima hii,” alisema Dk Kimei.

Kuondoka kwa Dk Kimei kwenye usukani wa benki hiyo, kunampa Nsekela changamoto mpya katika maendeleo ya taaluma yake aliyonayo kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Ushindani, mapato

Kuna ushindani mkubwa kwenye soko la fedha uliiongezwa na kampuni za mawasiliano zinazotoa huduma za fedha sasa hivi kutokana na kukua kwa teknolojia.

Kutokana na ushindani huo, zaidi ya benki tano zimefutiwa leseni ya biashara huku nyingine zikilazimika kuungana.

Mhadhiri mwandamizi na mkuu wa idara ya fedha wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Evelyne Richard anasema benki zinapaswa kuangalia namna ya kurahisisha huduma kwani kampuni za mawasiliano zimerahisisha huduma.

“Mtu hahitaji kwenda popote, anatumia simu yake kupata mkopo mdogo au kufanya jambo jingine lolote. Wateja wahamasishwe kutunza fedha ili benki ziweze kukopesha zaidi,” anasema Dk Evelyne.

Mwaka jana, mapato ya riba ya CRDB yalipungua kwa asilimia mbili na kufika Sh560 bilioni kutoka Sh569 bilioni ya mwaka 2016 huku gharama zikipanda kwa asilimia 11 kutoka Sh136 bilioni mpaka Sh151 bilioni ndani ya kipindi hicho.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa miaka minane mfululizo kwa mapato ya benki hiyo kupungua kwani tangu mwaka 2010, yamekuwa yakikua kutoka Sh125 bilioni.

Kwa robo iliyoishia Septemba, mapato ya riba ya benki hiyo yameshuka kwa Sh17.558 bilioni kutoka Sh431.754 bilioni zilizopatikana kwa miezi tisa ya kwanza mwaka jana hadi Sh414.196 bilioni mwaka huu.

Mtaalamu wa masuala ya fedha na huduma za fedha, Reginald Massawe anasema kupungua kwa mapato hayo kumetokana na kushuka kwa riba ya mikopo.

“Nsekela anapaswa aongeze umakini eneo hili kuhakikisha anakuza mapato. Serikali nayo iangalie madhara ya kushuka kwa mapato yatokanayo na riba kwa benki nyingi,” anasema Massawe.

Faida na gawio

Benki ya CRDB imekuwa inapata faida na kutoa gawio tangu mwaka 2010. Mwaka 2015 benki hiyo ilipata faida kubwa zaidi iliyofika Sh128.978 bilioni na mwaka jana ikapata kiasi kidogo zaidi ndani ya kipindi hicho, Sh36.212 bilioni.

Tangu mwaka 2010 ilipopata faida ya Sh47.246 bilioni, haikuwahi kupata chini ya Sh60 bilioni isipokuwa mwaka 2011 ilipopata Sh37.71 bilioni ambayo ni kubwa kuliko iliyopatikana mwaka jana.

Faida ya mwaka jana ilipungua kutoka Sh70 bilioni ya mwaka juzi. Dk Kimei alisema hali hiyo imetokana na kushuka kwa mapato ya riba na ongezeko la mikopo chechefu.

“Kuyumba kwa biashara ya kampuni ambazo ni wateja wa benki pamoja na kuondolewa kwa wafanyakazi hewa na wasiokuwa na vyeti ambao baadhi walikuwa wamekopa ni sababu nyingine,” alisema Dk Kimei.

Licha ya faida ndogo iliyopatikana mwaka jana, benki hiyo ilifanikiwa kutoa gawio la Sh5 kwa kila hisa moja kwa wanahisa wake 2,176,532,160.

Amana za wateja, mali za benki

Kwa mwaka 2010, amana za wateja zilikuwa Sh2.019 ambazo zimeongezeka mpaka Sh4.5 trilioni wakati mali za benki zikipanda kutoka Sh2.305 trilioni hadi Sh5.9 trilioni sasa hivi.

Kutokana na mali ilizonazo, mwaka jana kwa mfano, benki hiyo iliweza kukopa kutoka nje.

Dk Kimei aliwaeleza wanahisa wa benki hiyo kuwa walilazimika kuongeza mikopo kutoka nje kutoka Sh382 bilioni walizochukua mwaka 2016 hadi Sh655 bilioni.

“Kiasi kikubwa cha mikopo hiyo tulichukua kutoka Shirika la Fedha la Benki ya Dunia (IFC) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB),” alisema Dk Kimei.

Ukopeshaji, mikopo isiyolipika

Mwaka 2010, CRDB ilikopesha Sh1.123 trilioni kiasi kikubwa kikielekezwa kwenye sekta ya kilimo kwa asilimia 28 ikifuatiwa na biashara na viwanda kwa asilimia 15.

Mwaka huo, uwiano wa mikopo isiyolipika ilikuwa asilimia 11.5 ingawa kanuni za BoT zinapendekeza kutozidi asilimia 5.0.

Vyote viwili vimeimarika. Mikopo inayotolewa imefika Sh2.893 trilioni mwaka jana. Mikopo isiyolipika ilikuwa asilimia 13.1 Juni, kiwango kikubwa zaidi tangu mwaka 2010.

Hata hivyo, juhudi zilizochukuliwa zimepunguza kiasi hicho mpaka asilimia 8.9 robo iliyoishia Septemba mwaka huu.

Akizungumzia taarifa ya fedha kwa robo ya tatu, Nsekela anaamini: “Tutaimarisha huduma za kidijitali, ubunifu na ufanisi wa huduma zetu kwa mwaka ujao wa fedha. Nina imani maeneo hayo yatatutofautisha sokoni. Tunayaelewa mahitaji ya wateja wetu na tunajitahidi kuyakidhi.”

Matawi na wafanyakazi

Mwaka 2010, benki ilikuwa na matawi 102 pamoja na wafanyakazi 1,438 ambayo yameongezeka na kufika 253 yakihudumiwa na waajiriwa 3,175 waliokuwapo mpaka Septemba mwaka jana.

Hata hivyo, ndani ya mwaka mmoja uliopita, matawi hayo yamepungua hadi 234 na wafanyakazi 63 wakipungua pia mpaka 3,112 Septemba mwaka huu.