MAONI YA MHARIRI: Muda zaidi wa biashara ni muhimu kufikia uchumi wa kati

Saturday November 10 2018

 

Mkakati wa Serikali wa kuifikisha nchi katika uchumi wa kati wa viwanda unaendelea na unatakiwa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo. Ili kuunga mkono jitihada hizo, ushiriki wa kila mtu unatakiwa kwa kadri anavyoweza kulingana na nafasi aliyonayo na fursa iliyopo.

Kwanza viongozi wa Serikali ambao tayari wameweka sera na mipango ya maendeleo wanatakiwa kuwa thabiti katika kusimamia na kuhakikisha kile kilichopangwa ndicho kinachotekelezwa.

Wananchi kwa upande wao, wanatakiwa kushughulika na uzalishaji na ushiriki katika masuala ambayo yatawezesha uchumi wa nchi yetu kukua. Wabunge wetu nao wakiwa na jukumu la kuishauri na kuisimamia Serikali pamoja na kutunga sheria wezeshi, wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu hayo bila kutetereka.

Tulifarijika juzi tulipomsikia Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumzia umuhimu wa Serikali kuweka mazingira ya biashara kufanyika usiku bila wananchi kubughudhiwa ili waweze kutunisha mfuko wa Hazina kwa njia ya kodi.

Akitolea mfano wa baa, Ndugai alisema imekuwa ni kawaida kwa wenye baa kulazimika kufunga ifikapo saa 5:00 usiku, wakati wangeweza kuendelea kuingiza fedha na kulipa kodi zaidi.

Alishangaa kwa nini muda huo ukifika polisi wanaanza kupita na kuwaambia watu wafunge baa akieleza kuwa haelewi kwa nini watu wanazuiwa kufanya biashara wakati wakifanya hivyo Serikali inapata kodi. Spika alitoa kauli hiyo baada ya wabunge kadhaa kujadili Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2019/2010 wakieleza kuwapo kwa kasoro katika mazingira ya kufanya biashara, hali inayosababisha changamoto kwa uwekezaji nchini.

Kwa kuwa Serikali imeyasikia yote hayo, ni matumaini yetu kuwa yatazingatiwa na kufanyiwa kazi na viongozi au watendaji wake.

Inatia moyo hasa kwa kuwa baadhi ya watendaji wameshaanza kuimba wimbo mmoja kama wa Spika Ndugai, wa kutaka mazingira ya biashara yaboreshwe na muda wa kufanya biashara uongezwe hasa katika maeneo ya mijini.

Ni hivi majuzi tu, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alizungumza kupitia Televisheni ya Taifa kuwa ikitokea akawatumia polisi kwenye masuala ya uchumi, basi itakuwa ni kuwaagiza wahakikishe wafanyabiashara wanafanya kazi muda wote kwa usalama na asingependa kutumia amri za kipolisi katika kuendesha uchumi.

Alisema kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao, hivyo wanatakiwa kuweka mazingira salama ili biashara zifanyike nyakati zote; usiku na mchana.

Mtaka pia alizungumzia suala la baa kama Ndugai, akisema anashangaa inakuwaje zinapangiwa muda wa kufungua na kufunga wakati wanywaji wa bia ni watu wenye shughuli tofauti.

Alisema wapo wanaoingia kazini kwa nyakati zisizofanana wakiwamo wanaoingia shifti za jioni au usiku, akihoji iweje mchana wasinywe bia?

Mtaka alikwenda mbali akatoa mfano wa Kenya kuwa ukienda Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta usiku ni kama mchana, watu wanaendelea na biashara muda wote, tofauti na Dar es Salaam au Kilimanjaro ambako usiku huwezi kupata hata usafiri wa haraka. Hata taa za barabarani, Mtaka anashangaa kuwa zipo kwa ajili ya ulinzi na watu kufanya biashara kama ilivyo mchana.

Tunakubaliana na Mtaka na Ndugai kuwa uwekwe utaratibu kuwa watu wasipangiwe muda wa kufanya biashara kana kwamba wateja wote wana ratiba zinazofanana. Tunaamini kwamba Jeshi la Polisi likijielekeza katika kulinda usalama nyakati za usiku, biashara zitaendelea kufanyika.

Advertisement