Wacuba: Vikwazo vya Marekani vinauma, hatujasalimu amri

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Profesa Lucas Polledo (katikati), akiwa na Husna Roussos (kushoto) ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Urafiki kati ya Cuba na Tanzania na balozi wa Vietnam nchini Nguyen Kim Doanh (kulia), akisikiliza mada iliyokuwa ikwasilishwa wakati wa hafla iliyofanyika nyumbani kwake wiki iliyopita. Picha |Khalifa Said

Wakati Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ukiketi wiki iliyopita na kulaani vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Marekani dhidi ya nchi ya Cuba, Wacuba wanaoishi nchini walikutana wiki hiyohiyo kwa lengo la kulaani mbinu mpya za Marekani zinazolenga kuzidi kuitenga nchi yao na nchi zingine za dunia.

Katika hafla fupi iliyofanyika Oktoba 27, 2018 nyumbani kwa Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Oysterbay jijini hapa, raia hao wa Cuba, ambao wanafanya kazi katika sekta za elimu na afya nchini, walilaani vikwazo hivyo dhidi ya nchi yao huku wakisema kuwa vimelenga kudhoofisha na kunyamazisha utu na hadhi wa taifa lao na watu wake.

“Vikwazo hivyo vya kihalifu dhidi ya nchi yetu, ambavyo viliasisiwa miaka 60 iliyopita na kuendelezwa na serikali zilizofuata za Marekani, havijafanikiwa kuwafanya watu wa Cuba wasalimu amri kwa Marekani licha ya ugumu mkubwa ambao watu wetu wamelazimika kupitia katika kipindi chote hicho,” inasomeka sehemu ya kauli ya pamoja ya raia hao.

Uhusiano wachafuka

Uhusiano kati ya Cuba na Marekani umezidi kudhoofika tangu Rais Donald Trump achaguliwe kuwa rais wa Marekani mwaka 2016. Trump amerejesha sera zilizoitambulisha sera ya mambo ya nje ya Marekani dhidi ya Cuba wakati wa vita baridi huku akiimarisha vikwazo vya kibiashara na usafiri, ambavyo awali vililainishwa na mtangulizi wake, Barack Obama.

Chini ya Obama na Rais wa zamani wa Cuba Raul Castro, Marekani na Cuba zilirejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na hata kuunda uhusiano wa karibu, kitu ambacho kilisababisha kila nchi kufungua ubalozi wake kwa mwenzake. Lakini ujio wa Trump madarakani umerejesha suala hili mwanzo kabisa na kufuta kila hatua iliyokwishapigwa na nchi hizo mbili.

Serikali ya Cuba iliwasilisha kwa mara ya 27 ombi la kutaka vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo viondolewe katika mkutano mkuu wa UN wiki iliyopita.

Hatua hii hata hivyo, haikuupendeza uongozi wa Trump ambao inaelezwa kuwa ulijipanga kulipinga ombi hilo kwa kutumia hoja za haki za binadamu ambazo uongozi huo umedai kuwa haziheshimiwi nchini Cuba.

Wiki iliyopita serikali ya Marekani iliwasilisha kampeni yake katika UN ihusuyo shida wanazopitia wafungwa wa kisiasa nchini Cuba. Hata hivyo, kampeni hiyo haikuweza kufanyika kwani wanadiplomasia kutoka Cuba na Bolivia waliivuruga kwa kupiga kelele, kuimba na kugonga meza kitu ambacho kiliilazimu Marekani kughairi kuendelea nayo.

Idadi kubwa ya mataifa katika UN yamekuwa zikiunga mkono kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Cuba kwa kupiga kura kuiunga mkono nchi hiyo katika harakati zake za kufanikisha hilo katika jukwaa hilo la kimataifa.

Mwaka jana, kwa mfano, uamuzi wa UN kutaka vikwazo dhidi ya Cuba viondolewe uliungwa mkono na mkutano mkuu wa UN wenye wanachama 193 na kupata kura 191. Ni Marekani na Israel pekee walipiga kura ya kuukataa uamuzi huo.

Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Profesa Lucas Polledo alisema katika hafla hiyo kuwa serikali ya Marekani inajaribu kuhalalisha tabia ambayo kimsingi inaenda kinyume na jumuiya ya kimataifa.

Vikwazo vikali

Mwenyekiti wa Kamati ya urafiki kati ya Cuba na Tanzania, Salim Msoma alisema vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba kwa takribani miongo sita ni vikali, vya muda mrefu na visivyo vya haki ambayo hakuna nchi nyingine yoyote imewahi kuwekewa.

Alibainisha kuwa si tu vikwazo hivyo vinakiuka mkataba wa UN, bali pia vina sifa ya mauaji ya halaiki kwa mujibu wa kifungu namba mbili cha Mkataba wa Geneva wa kuzuia uhalifu unaotokana na mauaji ya halaiki wa mwaka 1948.

“Ni kikwazo kikuu cha ukuaji wa uchumi wa Cuba,” anasema Msoma. “Vikwazo hivi kwa kiasi kikubwa vinakiuka haki za binadamu za raia wa Cuba na kuingilia uhuru wa nchi hiyo. Kimsingi, lengo kuu la vikwazo hivi ni uchokozi,” alisema.

Maoni haya ya Msoma yanathibitishwa na waraka wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani wa mwaka 1960 ambao uliainisha kuwa lengo kuu la vikwazo hivyo ni kufanya maisha miongoni mwa Wacuba kuwa magumu na hivyo kuchochea kuiondosha madarakani serikali iliyopo.

“Lakini hili haliwezi kutokea,” anasema Msoma. “Wacuba wamekuwa thabiti pamoja na serikali yao katika kupambana na dhuluma hii dhidi yao.”

Kauli chafu na chokozi

Katika mada yake wakati wa hafla hiyo, Kanali mstaafu Isaack Katanda, ambaye ana uzoefu wa miaka mingi katika operesheni za kudumisha amani barani Afrika, alisema hatua mpya zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya Cuba zinalenga kuweka vikwazo zaidi kwa Wamarekani wanaotaka kusafiri kwenda Cuba.

Alieleza kuwa kuimarishwa kwa vikwazo hivyo katika mwaka 2018 kumeifanya Marekani kuzidisha makali ya chuki yake kwa wananchi wa Cuba kwa kuzidi kuminya miamala yao ya kifedha na biashara kwa ikiyaadhibu makampuni na mashirika yenye mafungamano na Cuba.

Cuba haitasalimu amri

Katika hotuba yake ya kufungia wakati wa hafla hiyo, Profesa Polledo, alirudia msimamo na utayari wa serikali ya nchi yake kufanya majadiliano ya heshima na kuanzisha ushirikiano katika masuala yenye maslahi kwa Cuba na Marekani.

Katika namna ambayo imekusudia kuionesha Cuba kama taifa lisilo la kikorofi kwa jirani na hasimu wake, Polledo alisema serikali yake inashawishika kwamba nchi hizo mbili zinaweza zikashirikiana katika hali ya kistaarabu wakati huohuo zikiheshimu tofauti baina yao.

Hata hivyo, Profesa Polledo aliweka masimamo kwamba kamwe isitegemewe kuona Cuba inasaliti uhuru wake wa kujiamulia mambo yake kama nchi au kukubali masharti kutoka taifa lingine lolote lile.

“Mkakati wowote ambao una lengo la kubadilisha mifumo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Cuba, iwe ni kwa njia ya mashinikizo au kwa kutumia njia nyingine zozote zile, zitashindwa kufikia malengo yake,” alisema.