Ufugaji wa kuku unahitaji aina nyingi za ubunifu ili kupata tija

Mojawapo ya ubunifu kwa mfugaji wa kuku ni kulijua vizuri soko lako. Picha na Maktaba

Tumeona mengi katika makala zilizopita, ikiwamo makala ya wiki iliyopita ambayo ilizungumzia jinsi kuku anavyoweza kuhudumiwa kwa chakula na hatimaye kutaga vizuri.

Wafugaji wengi wanashindwa kujua sababu inayochangia kuku wasitage, ilhali kuku wa aina ileile kwa jirani au mtu mwingine wanataga Changamoto hii imekuwa jambo la kawaida kwa wafugaji wanaofuga kuku kwa ajili ya mayai, kwa sababu kuku huchukua muda mrefu tangu anapokuwa kifaranga hadi kufikia hatua ya kutaga.

Mara nyingi mfugaji hutoa chakula kulingana na kile anachoona kina unafuu kwake kifedha bila kujali mahitaji ya kuku hao wakati huo. Mambo haya huwakosesha mapato mazuri wafugaji wengi.

Ubunifu katika ufugaji

Pia, makala ilisisitiza juu ya wafugaji kuwa wabunifu kwa kutumia fursa ipasavyo. Kuwa mbunifu inakupa kuendelea kuwa kwenye soko na kujipanua zaidi. Ubunifu una sura nyingi ambazo si rahisi kuzielezea lakini misingi ya ubunifu katika ufugaji inaweza kuwa sawa kwa kila aina ya mifugo.

Kwa mfano, mfugaji akifahamu kuwa biashara anayoifanya ni biashara ya viumbe hai wenye mahitaji sawa na binadamu, ni rahisi kupangilia shughuli zake. Mfugaji anatakiwa kujua kalenda ya malisho katika misimu ya mwaka.

Malisho ya mifugo hutokana na mazao ya vyakula vya binadamu. Shughuli nyingi za uzalishaji wa mazao hufanyika wakati wa mvua na kuvunwa wakati wa kiangazi. Kwa hiyo mfugaji anaweza kujikusanyia chakula cha mifugo yake wakati wa mavuno kwenye kiangazi, kuyakausha vizuri na kuyahifadhi kwa ajili ya msimu ujao wa mvua.

Ubunifu huu unaweza kufanyika kupunguza gharama za ulishaji kipindi bei ya malisho inapokuwa juu. Ubunifu wa pili ni pale mfugaji anaposoma alama za nyakati kuwa; miezi fulani soko la mayai au nyama huwa zuri.

Hivyo anaingiza kuku kwa mahesabu kwamba kufikia wakati huo atakuwa ameanza kuzalisha na kuuza bidhaa zake. Ubunifu wa tatu ni kutoka sokoni.

Mbinu nzuri kushika soko la bidhaa ni kuwa sokoni muda wote wateja wakufahamu. Wakati ambao soko limeshuka, unatakiwa kuwa na walau kiasi fulani cha bidhaa unachozalisha na kuuza ili kushikilia wateja.

 Ubunifu huu utakufanya uwe na uzalishaji wenye sura mbili; ya kwanza ni uzalishaji mkubwa wakati wa soko na sura ya pili ni uzalishaji mdogo wakati soko limepungua.

Lakini unaweza kusema kwa nini soko linapanda na kushuka wakati idadi ya watu ni ileile na bidhaa unayozalisha ni chakula ambacho ni hitaji lao la muhimu muda wote? Jibu ni kwamba haijalishi umuhimu wa zao kwa watumiaji.

Uwezo wa kununua au kutonunua huongozwa na kipato cha watumiaji. Ubunifu wa nne ni kutokuwa na bei ya juu sana kiasi cha kuwazidi watumiaji kununua.

Ni bora kuuza bidhaa nyingi kwa muda mfupi kwa kupata faida kidogo kidogo kuliko kuuza bidhaa kidogo kwa faida kubwa na kuendelea kubaki na bidhaa pasipo kuuzika na mwishowe kuharibika. Ubunifu wa tano ni kuwa na ubora utakaotambulika kwa wateja.

Kama ni mayai yatambulike ubora wa ndani na nje kwa wateja. Kama ni kuku wa nyama watambulike uzito wa kuuzia sambamba na umri wao, ili wateja wafahamu kuwa ufugaji wako na uuzaji wako unakwenda kwa viwango ambavyo mteja hahitaji kufikiri mara mbili mbili kununua bidhaa yako. Ubunifu wa mwisho ni kubaini tatizo mapema na kulishughulikia kabla halijaleta madhara kwenye biashara yako.