TUONGEE KIUME: Wanaume tusio na hela, tunaongoza kulalamika wanawake wanapenda hela

Sunday January 13 2019

 

Kama una uzoefu wa kuishi kwenye nyumba za kupanga utakuwa unanielewa zaidi nikitaka kuongelea tofauti kati ya mwenye nyumba anayemiliki nyumba nyingi na yule ambaye Mungu kamjalia kuwa na kanyumba kake kamoja na ndo hako hako ambacho dalali alikupeleka, ukapanga.

Kwanza mara nyingi mwenye nyumba anayemiliki nyumba moja huwa mnaishi naye humo humo. Yaani yeye na familia yake hutumia sehemu ya nyumba na vyumba vilivyobaki ndiyo hupangisha.

Bado haijathibitishwa kibaiolojia lakini kuna uwezekano wenye nyumba wa aina hii, neva za miili yao zimeunganishwa na nyumba zao. Yaani ni kama nyumba ni yeye, yeye ni nyumba.

Ukigongelea msumari kwenye ukuta wa nyumba yake ni kama umemgongelea yeye. Akikusikia, hata ikiwa usiku wa manane atakuja kukugongea kujua kulikoni? Mbona unatoboatoboa nyumba yake. Na akiwa mwanamke ndiyo utagundua kwa nini muuza kahawa anatembea na chombo cha moto lakini hana leseni.

Utaambiwa; “Wakati najenga hii nyumba hukunisaidia hata kubeba tofali. Kwa hiyo nakuomba usinitobolee-tobolee nyumba yangu.

Au…

Kama umeajiriwa na bosi ambaye ana biashara moja tu na ndiyo hiyo hiyo anayoitegemea hapa mjini. Mathalani kakupa pikipiki yake uwe bodaboda au upo kwenye saluni yake kama kinyozi ni mtihani. Hesabu hataki ipungue hata Sh 500, na hatakai maelezo mengi. Kwa sababu ndiyo biashara anayotegemea, ukimpunguzia unamlazimisha na nyumbani pia apunguze vitu.

Lakini wenye nyumba wanaomiliki nyumba mbili tatu au mabosi wenye vyanzo vingine vya kutosha vya mapato wala hawana hizo mambo. Wana utulivu kwa kila jambo kwa sababu wanatembea na roho zao, hawaziachi kwenye biashara walizokuachia au nyumba waliyokupangisha.

Naanza kuhisi ni kama kuwa na vitu vinavyokutosha kunakufanya kuwa mtu msafi kwa sababu hata wanaume ambao tunalalamika wanawake wanapenda hela ni sisi ambao tuna pochi za kuungaunga, tunahonga visenti senti vishilingi mbili tatu.

Mwanamke akinyanyua mdomo kukuelezea shida yake na kuomba umsaidie pesa kidogo atatue tatizo unaona ni kama kakuomba figo kakukosea sana. Utaanzisha mijadala kwa kuandika maujumbe marefu marefu kama makala za uchumi kwenye mitandao ya kijamii kutudadavulia jinsi wanawake wanavyopenda pesa na blaa blaa za kutosha.

Wakati wenzetu ambao mifuko yao iko vizuri, ina kiwango cha SGR wala hawana hizo. Kwanza hawangoji mpaka waombwe, wakiona mwanamke amepoapoa tu wanajua kuna tatizo, na kwa sababu mifuko yao iko vizuri, wanaamini matatizo yote yanamalizwa na pesa. Kufumba na kufumbua wanafanya muamala na hiyo kwao sio kuhonga wala kuchunwa, wanapenda kusaidia watu wanaowapenda basi.

Lakini yote kwa yote asilimia kubwa ya wanawake wa mjini, wanapenda kuomba hela.

Advertisement