Wapinzani waweka mikakati kupinga muswada wa vyama vya siasa

Wednesday January 16 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Vyama vya upinzani nchini vimeweka mikakati ikiwamo ya muda mfupi na ya muda mrefu, ambayo vinaamini itavisaidia kupambana dhidi ya muswada wa sheria wa vyama vya siasa na kudai demokrasia.

Mikakati huyo iko ndani ya maazimio yaliyowekwa katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa vyama hivyo ukiwa na lengo la kuchambua muswada na kuangalia athari zinazoweza kusababishwa endapo kupitishwa na kuwa sheria.

Akiwasilisha mipango hiyo, mkuu wa Idara ya maboresho ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Harold Sungusia anasema mipango hiyo imetokana na uchambuzi wa vipengele vyenye athari ndani ya muswada huo.

Akitaja mipango ya muda mfupi anasema ni kubaini maeneo mkakati ya kuushughulikia muswada huo kulingana na wadau na maeneo yao ya umahiri, kupeleka elimu kwa wananchi wengi zaidi kuhusu maudhi na athari tarajiwa za muswada.

“Wananchi tutawafikia kupitia vipindi maalumu vya radio na Televisheni ili kuhakikisha wanafahamu athari hizi na kuwaita washiriki kwa dhati katika midahalo ya kujadili muswada kwa upana na kujiandaa kuwasilisha maoni katika Kamati ya Bunge ili kuondoa malalamiko miongoni mwetu,” anasema Sungusia.

Anasema pia wanapaswa kutambua wabunge watakaosimama kwa dhati kuwasilisha mapendekezo ya wadau dhidi ya muswada huo kwa kuwasilisha bungeni mswada binafsi ili uweze kusikilizwa.

Aliyekuwa mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba alisema wako tayari kuunga mkono kesi na mashauri mengine yaliyopo kwa lengo la kuboresha au kulinda demokrasia nchini ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Hatutajali kesi imefunguliwa au wafuasi wa chama gani bali tutahakikisha kila shauri litakalofika mbele yetu lenye hoja kama hiyo tunalisimamia kwa namna yoyote,” anasema Kibamba

Mipango ya muda mrefu

Lakini wakati hayo mengine yakifanyika ndani ya muda mfupi, miongoni mwa mipango ya muda mrefu ni pamoja na kutafakari sababu za serikali kuandaa muswada huo.

“Lazima tuendelee kujiuliza kwa nini muswada huu uletwe saa hizi, kwa nini sio zamani au baadaye, nani mwathirika, nani aliyelengwa zaidi, tukishapata majibu tuendelee kuchukua tahadhali zaidi,” anasema Sungusia.

“Lakini pia tukumbuke kwamba hakuna sheria nzuri na kwa mtu yoyote hata anayeitunga na kuifurahia kuna wakati inaweza kumgeukia na kumuumiza ila kwa sasa hawaoni kwa sababu ya ushabiki,” alisema.

Anasema kufufua mchakato wa kupata Katiba mpya na kuuendeleza kupata katiba itakayoweka miundo mbinu sahihi ya demokrasia endelevu ni miongoni mwa mambo yatakayochangia kuboresha hali ya kisiasa nchini tofauti na zamani.

“Huwezi kufanya maboresho ya sheria bila kuwa na katiba nzuri badala yake sheria inapaswa kutungwa kwa kufuata katiba inayoongoza nchi na si kuikiuka,” anasema Sungusia.

“Pia Tanzania ni nchi pekee katika nchi za Afrika ya Mashariki ambayo haijasaini mkataba wa Afrika wa demokrasia, chaguzi na utawala bora, hivyo tumepanga kuendeleza kampeni hii hadi pale serikali itakaporidhia kusaini,” anasema Sungusia.

Vilevile wamepania kuwezesha miswada binafsi na kukusanya rasilimali kwa ajili ya kuendeleza demokrasia na misingi ya utawala bora ni miongoni mwa mipango ya muda mrefu iliyowekwa na vyama hivyo.

Hata hivyo, pamoja na mipango hiyo, wapinzani wamepania kuendeleza madai ya katiba ikiwamo na kupata Tume huru ya uchaguzi ambayo wajumbe wake hawafungamani na chama chochote.

“Hii itawapa uhuru katika kusimamia uchaguzi bila upendeleo au kwa kufuata maagizo kutoka sehemu ambayo inaweza kuwalazimisha matokeo yawe ya namna gani,” alisema.

Vilevile wanataka kiwepo kifungu cha kuwezesha matokeo ya urais kupingwa badala ya uamuzi wa mwisho kuishia tu Tume ya Uchaguzi na mtu yoyote mwenye ushahidi aruhusiwe kusimama mahakamani kupinga matokeo ya urais.

Sungusia anahoji: “Mbona nchi za wenzetu hili jambo lipo, sisi tunaogopa nini kukaa wiki au mwezi bila kumwapisha Rais? Wanapopitisha sheria hii ni lazima waweke muda maalumu kuwa ni ndani ya siku ngapi baada ya kutangazwa matokeo mtu anaweza kuweka pingamizi la kuapishwa rais mteule.”

Katika malengo hayo, Kibamba alizungumzia suala la mgombea binafsi akisema linaweza kupunguza gharama kwa kuwa kiongozi wa kuchaguliwa akivuliwa uanachama anaweza kusimama na kuomba kura kama mgombea binafsi.

“Tunataka tufanye utafiti tujue ni kiasi gani huwa kinatumika katika kila uchaguzi na shilingi ngapi hupotea katika kurudia chaguzi ambazo watu wanajivua wenyewe uanachama na kupoteza sifa halafu wanagombea tena,” alisema Kibamba.

Matatizo ya muswada

Akiyataja miongoni mwa matatizo yanayoweza kutokana na muswada huo ni pamoja kufifisha kufifishwa kwa misingi ya utawala bora. “Suala hili litadhoofisha miundombinu ya ushiriki na ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi, uhuru wa kujumuika na kuunda au kujiunga na vyama na kubwa zaidi ni kuhatarisha amani na utengamano wa taifa kwa siku zijazo,” anasema Sungusia.

Advertisement