Mbinu tano za kukuza ari ya wafanyakazi

Katika maeneo ya kazi wapo watu hufanya kazi kwa sababu tu wanamwogopa bosi.

Jitihada yao kazini inategemea sheria na vitisho kutoka kwa bosi. Inapotokea bosi hayupo karibu, watu hawa hukosa msukumo wa kazi na matokeo yake huharibu.

Tija kwenye maeneo ya kazi, kwa kiasi kikubwa, hutegemea namna wafanyakazi wanavyohamasika kufanya kazi.

Kila mfanyakazi anapokuwa na msukumo wa kufikia malengo aliyojiwekea, kazi ya kiongozi

Wake haiwi ngumu.

Namna gani kiongozi wa ofisi anaweza kuweka mazingira yanayowahamasisha wafanyakazi kujituma? Mbinu gani zinaweza kutumika kukuza ari ya kazi miongoni mwa wafanyakazi?

Makala haya yanaangazia matano yanayosaidia kukuza motisha ya wafanyakazi.

Mazingira bora ya kazi

Hamasa ya kazi inaanzia kwenye namna unavyomwezesha mfanyakazi kutekeleza kazi yake bila vikwazo.

Hapa tunazungumzia upatikanaji wa vitendea kazi vya msingi vinavyomwezesha mfanyakazi wake kutimiza wajibu wake.

Lakini pia, mazingira bora ya kazi maana yake ni kumwezesha mfanyakazi kutumia vipaji vyake ipasavyo.

Moja wapo ya sababu zinazoongeza motisha ya kazi ni mtu kuona mamna gani anaweza kutumia uwezo alionao kikamilifu.

Kadhalika, masilahi mazuri yanampa mfanyakazi utulivu wa nafsi. Mfanyakazi mwenye msongo wa mawazo wa namna atakavyoendesha maisha yake, hawezi kuwa na hamasa ya kufanya kazi kwa kujituma.

Mlipe mfanyakazi wako kiwango kinacholingana na makubaliano mliyojiwekea. Kama huna sababu ya msingi, lipa madai yoyote ya haki kulingana na kazi aliyoifanya.

Kuaminika na kuheshimika

Kila binadamu analo hitaji la kuaminiwa. Unapokuwa na uhakika una mtu anayemheshimu na kukuamini, unakuwa na motisha ya kufanya vizuri zaidi kukidhi imani yake.

Kama kiongozi kazini, unahitaji kuwa na tabia ya kuonyesha unaamini utendaji wa watu wako pasipo kuwaingilia bila

sababu.

Unaweza kuonyesha imani kwa namna nyingi. Kwa mfano, badala ya

kumfuatilia mtu kwa karibu mno, mpe kiasi fulani cha uhuru wa kufanya kazi kwa namna anayoona inafaa muhimu asiharibu kazi.

Hitaji kuona matokeo ya kazi badala ya kudhibiti kila kinachofanywa ikiwa si lazima.

Kadhalika, kuwaamini wafanyakazi kunakwenda sambamba na kuwaheshimu. Heshima kwa watu walio chini yako –iwe ni kwa maneno na vitendo vyako –inakutengenezea mazingira ya kuheshimiwa.

Epuka kuonekana unawadharau watu kwa kuwatendea kama watoto.

Hata wanapokuwa wamekosea onyesha staha kwa namna unavyoshughulika makosa yao.

Kutambuliwa na kushirikishwa

Kutambuliwa ni kuonyesha kuelewa nafasi ya mfanyakazi wako kwenye ofisi, idara, kampuni au taasisi.

Unapomtambua mfanyakazi, unamfanya ajisikie kuthaminiwa. Kwa mfano, kufahamu jina na kumtambua kwa

nafasi aliyonayo inatuma ujumbe kuwa unathamini uwepo wake.

Kadhalika, namna bora ya kuthibitisha kuwa unawatambua wafanyakazi wako ni kuwafanya wajione ni sehemu ya taasisi au kampuni yako.

Washirikishe kwenye maamuzi hata kama unajua wewe ndiye mwenye sauti ya mwisho. Omba mawazo ya watu waliochini yako. Onekana ukiandika mawazo unayoyapokea.

Kile kinachowezekana kufanyiwa kazi, kitekeleze. Unapofanya hivi kwa dhati watu watakuwa na ari ya kazi.

Kueleweka kwa malengo

Moja wapo ya mambo yanayofanya watu wakose ari ya kazi, wakati mwingine ni kutokueleweka kwa malengo ya taasisi.

Hali hii hufanya kila mtu ajikute anafanya kile kinachomjia kichwani ili naye aonekane anachapa kazi.

Fanya jitihada wafanyakazi wajue kampuni au taasisi inalenga kufika wapi.

Malengo ya muda mrefu na ya muda mfupi yaeleweke. Kwa mfano, kama ni kampuni, ifahamike mnataka kupata mafanikio gani katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kila mmoja aelewe mwelekeo wa pamoja. Lakini ili malengo hayo ya kitaasisi yawe na maana, lazima uhakikishe kila mmoja anajua anapaswa kufanya nini.

Ainisha majukumu ya kila mfanyakazi kuepusha mwingiliano usio na sababu.

Kila mmoja afanye kazi yake bila kuingilia majukumu ya mwenzake.

Kadhalika, ni vyema na wewe kama kiongozi ukatabirika. Hakikisha waliochini yako wanajua kwa hakika unatarajia nini kwao. Kutabirika kwako kama kiongozi kunarahisisha kazi ya watu kukidhi matarajio uliyonayo.

Usalama wa ajira

Watu wanapenda kuwa na uhakika na kesho. Hofu ya kufutwa kazi, kuonewa, kudhulumiwa, inaondoa motisha kazini.

Ukitaka kuongeza ari ya kazi kwa wafanyakazi wako, wafanye wajisikie wako salama.

Njia ya kwanza kumhakikishia mtu usalama wake ni kumpa mkataba.

Hili ni sharti la kisheria na kisaikolojia. Mfanyakazi anapokuwa na mkataba anaouridhia anakuwa hana sababu ya kuwa na wasiwasi na kesho.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano: 0754870815 Twitter @bwaya