Kibano cha sheria mpya kwa vyama vya upinzani

Pamoja na shinikizo la vyama vya upinzani, asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla, Bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ambao wengi wameutafsiri kuwa una lengo la kuirudisha Tanzania katika mfumo wa chama kimoja.

Muswada huu unaosubiri saini ya Rais John Magufuli kuwa sheria, umekuja huku kukiwa na migawanyiko ya wazi ya kisiasa, kitu ambacho ni hatari kwa usalama na ustawi wa nchi.

Wachambuzi na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania wamesema kupitishwa kwake kunaashiria giza nene linaloweza kuyafunika maendeleo ya kidemokrasia ambayo Tanzania ilishayafikia.

Nic Cheeseman, profesa wa masuala ya kidemokrasia kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza ameandika katika mtandao wa Twitter akionyesha kusikitishwa na hatua ya wabunge wa Tanzania kupitisha muswada huo.

“Kupitishwa kwa muswada huu kunaashiria kifo cha taratibu na cha maumivu ya demokrasia,” aliandika msomi huyo ambaye pia ni mwandishi wa kitabu kinachoitwa ‘Jinsi ya Kuiba Uchaguzi‘.

Akirejea kauli ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ya kuufananisha muswada huu na sheria iliyowahi kupitishwa mwaka 1933 na Adolph Hitler wakati wa utawala wa Kinazi nchini Ujerumani, Rachael McLellan katika mtandao wa Twitter anasema ingawa hoja ya Zitto inaweza kuonekana imeenda mbali sana, lakini hadhani kwamba haina sahihi kabisa.

McLellan ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Princeton, Marekani akibobea katika eneo la vyama vya upinzani nchini Tanzania, anaandika:

“Muswada huu unakusudia kufanya utii wake wenyewe, kama zilivyo sheria nyingine za hivi karibuni kuwa haiwezekani tena mtu kuitii na bado akafanya kazi ya upinzani.

“Hii si sahihi kabisa kwani vyama vya upinzani ni muhimu kwa midahalo na masuala ya uwajibikaji. Vinaweka vikwazo kwa serikali kuiepusha kutumia vibaya madaraka yake.”

Shida ni nini?

Uchambuzi wa Mwananchi unaonesha vipengele kadhaa ndani ya muswada huu ambavyo si tu vinaweza kuathiri vyama vya upinzani bali pia vinaifanya dhana nzima ya mfumo wa vyama vingi nchini kutoweka.

Muswada huu unampa msajili wa vyama vya siasa mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa ndani ya vyama pamoja na michakato ya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa kupitia vyama hivyo.

Kuna hofu kwamba kifungu hiki kinaipa nafasi serikali kupitia msajili ambaye ni mteule wa Rais kuchagua nani wa kushindana na mgombea wa chama tawala katika uchaguzi mbalimbali.

Muswada huu pia unavitaka vyama vya siasa kutunza orodha ya wanachama wake ambayo muda wowote msajili anaweza kuomba apatiwe. Kushindwa kufanya hivyo kunaweza kupelekea chama kusimamishwa kufanya shughuli zake.

Wakati hili linaweza kuonekana ni jambo la kawaida, kimsingi linaleta mashaka kwani haijulikani msajili anaweza kufanya nini na orodha hiyo ya wanachama wa chama husika.

Suala jingine lenye utata ni upigaji marufuku wa vikundi vya ulinzi ndani ya vyama vya siasa, wakati ripoti kadhaa zimewahi kulilalamikia Jeshi la Polisi kuwa linakipendelea chama tawala

Hivi karibuni tu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana aliibua utata baada ya kutoa salamu ya ‘Kidumu Chama cha Mapinduzi’ wakati alipokuwa wilayani Butiama katika mashindano ya mbio ya Mwalimu Nyerere ambayo ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 19 tangu kifo cha Mwalimu.

Vilevile, kuna wakati maofisa wa Polisi wametuhumiwa hata kushiriki katika zoezi la wizi wa kura katika uchaguzi na kushindwa kuchunguza matukio ya wapinzani kushambuliwa na hata kuuawa.

Matukio hayo ni sababu za vyama vya upinzani kuamua kuunda timu zao za ulinzi wa viongozi na mali za chama. Lakini sasa muswada huu unataka vikundi hivi vya ulinzi kufutwa na kazi zote za ulinzi kubaki mikononi mwa polisi.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa mara ya kwanza vyama vinne vya upinzani vilishirikiana chini ya mwavuli wa Ukawa na kusimamisha mgombea mmoja kwa nafasi za ubunge na urais, kupitia sheria hii uwezekano wa kufanyika kwa kitu kama hicho uko katika hatihati.

Hii ni kwa sababu muswada unaweka sharti kuwa endapo vyama vitaamua kuungana basi vyenyewe vifutiwe usajili, na unasubiri waziri ndiye atangaze kanuni za kufanya hivyo.

Kutokana na kibano hicho, watu wenye uwezo, kama vile wafanyabiashara, hujiweka mbali na shughuli za vyama vya upinzani kukwepa usumbufu wa vyombo vya dola.

Wachache wanaoguswa na mawazo ya vyama hivi huweka mahusiano yao na michango yao ya kifedha kwa vyama vya upinzani kuwa siri kubwa, lakini hii haitawezekana tena kufuatia kupitishwa kwa muswada huu kwani unavilazimisha vyama vya siasa kuonyesha kwa msajili vyanzo vya mapato na mali zao. Kushindwa kufanya hivyo kutapelekea chama kufutiwa usajili.

Muswada pia unamtaka mtu au taasisi yoyote inayotaka ama kutoa mafunzo ya elimu ya uraia kwa wanachama wa chama fulani au kuwajengea uwezo itoe taarifa katika ofisi ya msajili.

Baada ya kupokea taarifa, msajili anaweza kuruhusu au kusitisha zoezi hilo huku akitoa sababu za kufanya hivyo. Sababu hizo hazipo katika muswada. Vyama vya upinzani vinahofu kwamba kifungu hiki kitawaathiri kwa sababu watashindwa kupata mafunzo kutoka kwa vyama rafiki vilivyopo katika sehemu mbalimbali duniani.

Pia, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya kuishutumu ofisi ya msajili kwa kuchochea migogoro ndani ya vyama. Japo msajili amekuwa akikanusha, lakini kwa kuingiza katika muswada kifungu ambacho kinampa nguvu kuomba taarifa yoyote za chama kutoka kwa kiongozi au mwanachama yeyote kunafanya wengi wasiupe uzito ukanushaji wake.

Si kila taarifa kuhusu taasisi fulani inaweza kutolewa, hiki ni kitu ambacho kinafahamika. Baadhi ya taarifa za taasisi ni siri ambazo kutolewa kwake kunaweza kuiingiza taasisi husika kwenye mtikisiko na hata mwisho wake. Chama kitakuwa na uhakika gani, kwa mfano, kama taarifa zake za kimkakati haziwezi kutumika dhidi yake na washindani wake. Isitoshe, si kila mwanachama au kiongozi wa chama anaweza kutoa taarifa kuhusu chama. Kitaasisi, ni katibu mkuu tu ambaye taarifa zinaweza kuombwa kwake na akazitoa.

Kwa muswada huu pia, chama cha siasa kinaweza kusitishiwa ruzuku yake katika kipindi ambacho kinaihitaji sana kwa ajili ya kuendesha shughuli zake kwa sababu tu msajili wa vyama anaamini kwamba uongozi wa chama hauna uwezo wa kusimamia uwajibikaji wa ruzuku hiyo.

Lakini kama hiyo haitoshi, muswada pia unampa mamlaka ya kukifutia usajili chama chochote ambacho anadhani kilipata usajili kwa njia zisizo sahihi.

Vipi ikitokea msajili akaja kudhani hivyo siku moja kabla ya uchaguzi mkuu na kukifutia usajili chama kikuu cha upinzani?

Mapambano yanaendelea

Desemba 20 mwaka jana wanasiasa watatu walifungua kesi katika Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura wakitaka muswada huo usipelekwe bungeni kujadiliwa kwani walijua ungepitishwa tu bila ya kujali vipengele vinavyodaiwa kutishia uhai wa vyama vya upinzani. Waliofungua shauri hilo ni Zitto Kabwe na wanachama wengine wawili wa CUF, Joram Bashange na Salum Bimani.

Lakini Januari 14 mwaka huu, Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi hiyo kwa kile ilichoeleza kuwa ni waombaji kuchanganya maombi mawili katika shauri moja ambapo ombi la kwanza ni kufuta kifungu cha 8 cha kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Haki na Wajibu na Ombi la pili ni kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Akizungumzwa muda mfupi baada ya mahakama kutupilia mbali kesi yao, Zitto alisema: “Tunauheshimu uamuzi wa mahakama, lakini tutaendelea kupigania haki zetu kupitia mahakama hizihizi kwani bado tuna imani nazo.”