BARAZA LA SALIM: Kero hizi za usafiri Zanzibar hadi lini?

Wednesday April 10 2019

 

By Salim Said Salim

Usafiri wa magari ya abiria katika maeneo mengi ya miji na vijijini Unguja na Pemba umegubikwa na matatizo ya kila aina.

Ukiitafakari hali ilivyo unaweza kuwa na dhana kwamba madereva na makondakta wa magari haya hawaongozwi na sheria na hawatakiwi kuwa watu wenye ustaarabu na uungwana.

Mbali ya wengi wao kutojali sheria za usalama wa abiria wao na wengine wanaotumia barabara, wapo wanaoyageuza magari haya kama kumbi za kufyatua matusi ya kila aina wakati wa safari huku muziki wenye kelele ukipigwa ndani ya gari wakati wote.

Ni kawaida kuwaona madereva wengi wakizungumza na simu ya mkononi wakati wakiendesha hayo magari kwa kasi na wakisimama kwenye eneo la hatari kama kwenye kona, chini au juu ya kilima.

Namna ambavyo baadhi ya magari haya yanavyojaza abiria kama samaki ndani ya mkebe ni hatari tupu. Kinachoshangaza ni kuona mara nyingine hizi gari hupita sehemu ambazo wapo askari wa Usalama Barabarani na kuruhusiwa kuendelea na safari kama vile zilikuwa salama kuendelea na safari.

Pale inapotokea dereva na kondakta kuambiwa wamezidisha abiria utaona askari amechukua maelezo kuonyesha dereva au kondakta au wote wawili watafunguliwa mashtaka.

Abiria waliozidi hawateremshwi na gari huendelea na safari. Huu si utaratibu mzuri kwa sababu ni sawa na kumwambia dereva endelea na uvunjaji wa sheria na kuhatarisha maisha ya abiria.

Karibu kila siku utaona wanafikishwa mahakamani madereva wanaokatisha safari na kulazimisha abiria wao kujitafutia usafiri mwingine wa kuendelea na safari zao au kuwapandisha katika magari mengine.

Hata pakiwemo wagonjwa ndani ya gari, watu wenye ulemavu au wazee wenye kupanda gari na kuteremka kwa shida, jua likiwa kali au mvua kubwa ikiwa inanyesha hawa madereva na makondakta huwa hawajali.

Kwa hakika ujeuri na ufedhuli wa madereva na makondakta wa gari za abiria Visiwani umevuka mipaka ya ustaarabu na unapaswa kukomeshwa.

Kwanza ni kwa abiria kuwa na sauti moja ya kukataa kunyanyaswa na kuchukua hatua za kutoa taarifa polisi wakati wanapofanyiwa vitendo visivyostahili.

Pili kikosi cha askari wa Usalama Barabarani kiachane na muhali wa kutowachukulia hatua za sheria kila anayefanya makosa haya yanayohatarisha maisha ya watu au kusababisha kwa makusudi usumbufu kwa abiria wao kama kutowafikisha mwisho wa safari zao.

Lakini, jingine muhimu ni wanaofanya makosa haya wanapofikishwa mahakamani nadhani hii adhabu ya hivi sasa ya Sh20,000 au 30,000 haijasaidia kwa vile ni ndogo sana na ndio maana uvunjaji wa sheria unaendelea.

Nadhani ipo haja ya kuzipitia sheria na kuzifanyia marekebisho yanayostahiki, lakini pia kuwepo na kumbukumbu nzuri zitakazoonyesha wanaorudia makosa.

Katika baadhi ya nchi madereva na makondakta wanaoonekana hawajali sheria za usalama hata baada ya kuonywa na kupewa adhabu kwa mara ya kwanza au ya pili hupewa adhabu kali zaidi ili kuwa somo kwao na wengine.

Miongoni mwa adhabu hizo ni kumnyang’anya dereva leseni kwa miezi kadhaa au hata mwaka mmoja. Hii inasaidia kupunguza ujeuri wa madereva.

Hili pia huwa somo kwa madereva kwa vile watakuwa wanajua kwamba hawataachiwa kuchezea maisha ya abiria au kuwaletea usumbufu watu wenye ulemavu, wagonjwa na wazee.

Advertisement