2018: Mwaka wa kilio cha masoko kwa wakulima

Saturday December 29 2018

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Kilio kikubwa cha wakulima kwa mwaka 2018, ni kusuasua na kuporomoka kwa ya bei ya mazao sokoni.

Wakati kwa wakulima wa zao la korosho wakipata kicheko baada ya Serikali kuingilia kati, wakulima wa mazao mengine waliozungumza na Mwananchi wanasema imewabidi wauze kwa bei ya hasara mradi tu warejeshe gharama kidogo waliyotumia wakati wa kilimo.

Mkulima wa mahindi na ufuta katika kijiji cha Ulaya, wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Rubanga Mapesi anasema badala ya kunufaika na kilimo chao, wanadidimizwa.

“Kinachoumiza ni bei ya pembejeo ambayo ipo juu , unalima halafu wakati wa kuuza hakuna soko mwisho wafanyabiashara wanakulalia kwa kununua bei wanayotaka wao. Kweli kilimo cha siku hizi kimegeuka cha kujikimu na njaa tu sio cha maendeleo. Tunalima ili tule,” anasema.

Mkulima Razaq Mtele Malilo kutoka mkoani Lindi anasema katika misimu miwili iliyopita zao la ufuta lilinunuliwa kuanzia Sh2,500 hadi Sh3000 kwa kilo, jambo lililowafanya wengi wahamasike kulima.

Anaeleza kuwa maajabu ni kwamba bei ya zao hilo katika msimu huu imeporomoka hadi kufikia Sh1,500 na 1,600 hivyo kuwasababishia hasara wakulima wengi.

“Kibaya zaidi mwaka huu pia yalitokea majanga ya mafuriko yaliyosababisha kusombwa kwa mazao ya chakula shambani kama mahindi, mihogo na mazao mengine, hivyo tulitegemea ufuta zaidi kujikimu kiuchumi na ufuta wenyewe bei ndio hiyo,” anasema.

Mapesi anasema katika wilaya ya Kilosa mwaka huu, wameuza kilo 30 za ufuta kwa Sh150,000 wakati misimu mingine waliuza mpaka Sh250,000.

Anasema gunia moja la mahindi linauzwa kati ya Sh24,000 hadi 40,000 wakati misimu mingine waliweza kuuza Sh70,000 hadi 100,000 katika kipindi kama hiki.

“Kusema kweli wakulima tumeumia sana, hivi unadhani ukiuza Sh24,000 wakati umevuna gunia nane kwa eka moja, utapata nini? Huwezi kufanya maendeleo hata kidogo,” anasema na kuongeza;

“Maisha yamezidi kuwa magumu kwa sababu kilimo tunachokitegemea kimekuwa kigumu zaidi, yaani kwa kweli tunalima tuishi tu ila sio kilimo kituinue kiuchumi.”

Mfanyabiashara wa mahindi katika kijiji cha Mbalizi mkoani Mbeya anasema anauza debe moja kwa Sh6,000.

“Misimu mingine muda kama huu huwa tunauza hadi Sh10,000 kwa debe moja lakini sasa hivi hali imekuwa mbaya, kama mimi nauza bei hii mkulima anauza debe moja hadi Sh3,000 au 4,000,” anasema Anitha Mwambiga, mkazi wa Mbalizi.

Mkulima wa viazi mviringi, katika kijiji cha Magoda mkoa ni Njombe anasema mwaka huu wameuza zao hilo kwa hasara.

“Kama mimi niliuzia shambani, walanguzi wananunua kwa bei wanayoitaka wao sisi hatuna nguvu ya kupanga n kibaya zaidi lumbesa inapigiwa kelele majukwaani tu huku chini wakulima tunateseka sana,” anasema Farida Kilasi, mkazi wa Magoda.

Wakulima wa zao la Karoti mkoani Tanga walisema kiloba cha zao hilo walichokuwa wanauza mpaka Sh10,000 wamelazimika kuuza kwa Sh5,000.

“Ukikaa nazo muda mrefu zinaoza kwa hiyo inabidi uziuze kwa bei wanayoitaka wafanyabishara sio sisi wakulima,” anasimulia.

Walia mipaka ya masoko kufunguliwa

Wakulima hao wanasema kinachoweza kuongeza thamani ya mazao yao ni mipaka ya masoko kufunguliwa.

“Kama mahindi yetu tutaruhusiwa yauzwe nchi za nje, hali itakuwa nzuri zaidi. Tunaomba mipaka ifunguliwe na wafanyabiashara wa nje waruhusiwe kuja kununua mazao yetu ili kuwe na ushindani kwenye soko,” anasema Mapesi.

Katika warsha ya wadau wa kilimo iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Dk Sinare Yusuph Sinare anasema ni vizuri Serikali ikaongeza bajeti ya kilimo ili sekta hiyo ifanye vizuri.

“Bado kilimo chetu kipo nyuma kwa sababu masoko ya mazao ni changamoto, mazao yameshuka bei kwa kiwango kikubwa.’’ anaeleza.

Anasema makubaliano yaliyofikiwa kwenye Azimio la Maputo yalikuwa ni kutenga asilimia kumi ya bajeti kwenye kilimo.

Mkurugenzi mkuu wa taasisi inayo jishughulisha na masuala ya kilimo mkoni Iringa, (BRITEN) Josephine Kaizer anasema kitakachowasaidia wakulima ni umoja.

Anawashauri wakulima hao kuunganisha nguvu zao na kuunda mnyororo mmoja ili wawe na sauti moja na kuweza kupanga bei ya mazao wanayoitaka.

“Utafiti na uchunguzi mwingi tulizofanya zinaonyesha kuwa wakulima wananyonywa na wafanyabshara, kwa sababu hawana nguvu ya kupanga bei ya mazao yao wakati wanapaswa kufanya hivyo. Sauti moja itakuwa mkombozi mkubwa wa wakulima,” anasema.

Novemba 27, mwaka huu Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alisema wizara yake imetuma watu kwenda kutafuta masoko ya kilimo nje ya nchi ili kuwapatia wakulima taarifa sahihi za masoko ya mazao yao.

Katika warsha hiyo ya ACT, Hasunga anasema msimu huu umekuwa na mavuno mazuri hivyo Serikali tayari imeamua kufungua mipaka ili wakulima wauze mazo yao popote.

“Tumefungua mipaka ili mtu auze mazao yake mahali popote, pia tayari watu tumewatuma wakaangalie masoko nje ya nchi kwenye nchi kama Sudani, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia,” alisema.

Anasema sekta ya kilimo imekua hadi kufikia asilimia 7.1 ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano ikilinganishwa na ukuaji w asilimia 1.9 uliokuwapo hapo kabla.

Advertisement