2019 mwaka wako kulima matikiti

Saturday February 2 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Ni tunda ambalo kwa sasa limetawala soko kwa walaji. Halina msimu hivyo mwaka mzima walaji wana uhakika wa kulipata.

Ni tunda linalopendwa kwa sababu lukuki ikiwamo ile inayowavutia wengi ya kusaidia ‘heshima ya ndoa’.

Wataalamu wa afya wanasema tunda la tikiti lina faida nyingi za kiafya ikiwamo kuwa na vitamin C kwa wingi, ambayo ni muhimu katika uimarishaji wa kinga mwilini.

Makala haya yanalenga kukupa mwanga utakaokuwezesha kuanza mradi wa kilimo hiki ambacho wengi wamekuwa wakikikimbilia katika miaka ya karibuni.

Una mtaji wa kutosha?

Kilimo cha matikiti kinahitaji uangalizi wa karibu. Ni cha muda mfupi usiozidi miezi mitatu, lakini kina harakati nyingi zinazomlazimisha mkulima kuwa na mtaji wa kutosha kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mradi.

Unahitaji kuwa na mtaji wa kununua au kukodi eneo la kilimo, mbegu, madawa, mbolea, vibarua, mifumo ya umwagiliaji (kwa wanaofanya kilimo cha umwagiliaji), usafirishaji na gharama nyinginezo.

Kimsingi, gharama ya mtaji inategemea mambo mengi ikiwamo ukubwa wa mradi wako. Kwa mfano, anayepanga kulima matikiti katika ukubwa ekari moja hawezi kuwa sawa na anayepanga kulima ekari tano.

Ni wakati wa kuwaona wataalamu wa kilimo hiki, kuzungumza na wakulima wenye uzoefu ili kupata picha halisi ya mtaji. Kumbuka hakuna gharama maalumu. Ziko tofauti za kijiografia, kijamii na nyinginezo zinazofanya kwa mfano mtaji wa eka moja mkoani Pwani ukawa tofauti na mtaji wa ekari hiyohiyo mkoani Mwanza.

Hata hivyo, kwa kuzungumza na wenye uzoefu, baadhi ya gharama zinaweza kuepukika. Kwa mfano, gharama ya vibarua inaweza kupungua ikiwa mkulima mwenyewe akaingia shamba badala ya kuacha kila kitu kifanywe na wengine. Na hili ni muhimu hasa kwa mkulima mdogo anayeanza mradi.

Ardhi yako ni sahihi kwa zao hilo?

Kilimo cha matikiti kinahitaji ardhi yenye rutuba na siyo ardhi yoyote; ardhi ya shamba lako lazima iwe na ubora ili mazao yaweze kusatwi vizuri.

Matikiti maji yanastawi kwenye udongo wa aina yoyote lakini unaohifadhi maji ni mzuri zaidi na uwe na kiwango cha ucahchu (pH) kuanzia 6 – 6.7.

Kumbuka pia kwamba, shamba lako linatakiwa kuwa karibu na mkondo wa maji, na kama hakuna maji ya kutosha tengeneza mifereji ili kurahisisha umwagiliaji.

Ifahamike kwamba matikiti yana asilimia 93 ya maji yake ya asili hivyo mkulima anatakiwa kumwagilia maji mengi ili yastawi vizuri. Si hilo tu bali yanahitaji mwanga wa jua kwa saa nane kila siku hivyo shamba linatakiwa kuwa eneo ambalo mwanga huo unapatikana.

Maji

Matikiti maji yanahiaji maji ili yaweze kukua vizuri, na si vibaya kama yatapandwa kipindi cha mvua kwa sababu shamba litakuwa na maji ya kutosha.

Hata hivyo, kama mradi upo katika maeneo yanayopata mvua chache (yenye ukame) tengeneza mfumo wa umwagiliaji kwa sababu kama mmea wa tikiti hautapata maji ya kutosha matunda yake yatakuwa machungu na utakosa soko kwa sababu hakuna atakayenunua.

Mfumo huu unaweza kuwa wa kutumia maji ya mabwawa, mito, ziwa , visima na vyanzo vingine. Mtaalamu wa kilimo Abdul Mkono matumizi ya maji yanategemea aina ya udongo

“Upo udongo unaohifadhi maji (ufinyanzi) na unaopoteza maji kwa haraka, kwa hiyo kwa udongo unaohifadhi maji kwa siku mkulima anaweza kumwagilia mara moja, na kwa udongo usiohifadhi maji amwagilie kwa siku mara mbili,” anasema.

Wadudu na magonjwa

Katika vitu ambavyo vinakwamisha mafanikio ya mkulima na ambavyo kwa hakika vinaweza kumkatisha mtu tamaa ni wadudu na magonjwa ya mimea.

Mkono anasema wadudu wasumbufu wa mazao wasipodhibitiwa wanaweza kusababisha hasara kubwa, hivyo anashauri kupiga dawa kila baada ya siku saba mpaka 14.

Wadudu na magonjwa yanahitaji weledi mkubwa kuyashughulikia na hapa ndipo wataalamu na wakulima wazoefu wanapohitajika kwa ajili ya kutoa uzoefu wao wa aina ya dawa zinazopaswa kutumika kwa tija.

Uvunaji wa matikiti

Kawaida matikiti hukomaa kati ya siku 70 hadi 90 na mkulima hatakiwi kuvuna chini ya siku hizo ni vyema kusubiri hadi yakomae.

Je utajuaje kama matikiti yamekomaa? Mkono anasema hatua hii ni muhimu kuzingatia hasa kwa mtu ambaye ni mgeni.

Anasema mkulima anaweza kutambua kama matikiti yapo tayari kwa kuangalia kwenye kikonyo ambapo kinaanza kunyauka na ukigonga kwenye tunda linalia kama ngoma.

Njia nyingine anasema ni mkulima anaweza kuchukua matikiti kutoka kila kona ya shamba na kuyakata kuangalia kama yameiva.

“Njia hii ya kukata ni njia yenye uhakika kwa sababu ukiyakata yote na kuonyesha yameiva ujue na mengine yameiva, lakini pia zamani tulikuwa tunaangalia rangi ukiona limekuwa la njano ujue limeiva lakini sasa hivi kuna mbegu nyingi ambazo zipo hata za kupauka,”anaeleza.

Soko la matikiti

Hili ni eneo nyeti katika mradi wowote wa kilimo. Hata hivyo, kwa zao hili uhakika wa soko katika maeneo mengi ya nchi upo hasa ikiwa mkulima atakuwa na mtandao na ufahamu wa kutosha wa masoko.

Kabla ya kuanza kuvuna mkulima anatakiwa kuandaa mazingira ya soko ili baada ya kuvuna anajua anakwenda kumuuzia nani, unaweza kupata soko kwa kutembelea masoko madogo lakini pia mkulima anaweza kuuliza wakulima wengine mahala wanapouzia.

Shaibu Issa ni dalali wa matunda katika soko la Buguruni, anasema soko la matikiti linakuwa siku hadi siku kutokana na matunda hayo kupendwa zaidi na hayana msimu maalumu.

“Mzigo wa matikiti ukikaa sokoni ni siku mbili na katika mkoa huu yanauzika sana labda ni kutokana na hali ya joto, lakini matunda mengine ambayo tunaweza kukaa nayo hapa hadi wiki moja na wakati mwingine yanaanza kuharibika kama vile mfano maembe,” anasema.

Mfanyabiashara wa matikiti

Lameck Nkwabi anayeuza matunda Buguruni jijini Dar es Salaam, anasema kwa siku anaingiza Sh. 70,000. Anachofanya ni kununua tikiti na kisha kulikata vipandevipande jambo analosema linaweza kumuingizia hadi Sh 15,000 kwa kila tunda.

“Matunda mengine nauza pia, lakini kama unavyoona mwenyewe wateja wengi ni wa matikiti,” anasema Nkwabi akiwa amezungukwa na wateja wake.

Advertisement