Adui mkubwa ukosefu wa kipato cha uhakika

Tangu tupate uhuru miaka 57 iliyopita, tumekuwa tunajitahidi sana kupambana na matatizo mengi tuliyokuwa nayo lakini hatujafanikiwa kwa sababu tunapambana na matatizo ambayo si ya msingi.

Matatizo mengi tunayopambana nayo ni viashiria vya tatizo la msingi ambalo ni ukosefu wa kipato cha uhakika na endelevu.

Kipato endelevu cha uhakikani kile kipato ambacho kinatupa uhakika wa kukipata kwa muda mrefu na ambacho kinaweza kukidhi matatizo yetu ya msingi kwa wakati fulani.

Wakati tukizungumza mahitaji ya msingi lazima tutambue kuwa yanatofautiana kati ya mtu na mtu kufuatana na mambo mengi. Kwa mfano mkulima ambaye hana shamba lake binafsi anakuwa na kishamba kidogo cha kukodi ambacho analima kujipatia chakula. Ana sehemu ya kuishi na vilevile huwa anategemea kufanya vibarua kwa watu ili kupata kipato cha kujikimu kukidhi mahitaji yake ya msingi – kitoweo, maji, malazi mavazi na matibabu. Mahitaji haya ni yale yenye ubora duni kwa mfano chakula ni cha ubora wa chini, maji ni adimu na machafu, malazi ni kibanda cha matope na paa la majani, mavazi yake ni mitumba na matibabu yake kwa kiasi kikubwa ni ya mitishamba na dawa za mganga wa kienyeji. Hawa wakulima wa chini starehe yao ni pombe za kienyeji na ngoma za kwenye sherehe.

Kwa wengine wenye maisha ya juu zaidi kwa mfano msomi mwenye kazi nzuri au mfanyabiashara mwenye biashara kubwa yenye kumpatia faida kubwa mahitaji yake ya msingi hayatofautiani na ya yule mkulima wa kipato cha chini.

Hawa wenye vipato vikubwa wanahitaji chakula, maji, malazi, mavazi na matibabu ila tofauti na hawa watu wa juu ni kuwa chakula chao ni cha ghali zaidi kwa vile kina ubora wa hali ya juu. Maji yao ni safi na salama. Malazi yake ni nyumba kubwa, mavazi ni nguo za bei mbaya na matibabu yake nia ya daktari wa uhakika wa ndani na hata wa nje. Starehe za wenye kipato cha juu ni vinywaji vya bei kubwa na kuangalia runinga zenye masafa ya kila aina ya habari na starehe.

Lakini wote hawa wana mahitaji ya msingi ambayo yanatofautiana na tatizo lao la msingi ni kipato cha uhakika na endelevu.

Hawa walio na kipato cha juu ni wachache sana na hawazidi asilimia 35 ya Watanzania wote na wao hawana kipato cha uhakika na endelevu hivyo nao wana hofu.

Kama tukikubali kuwa tatizo letu la msingi ni ukosefu wa kipato endelevu tutatambua kuwa kwa njia moja au nyingine kila Mtanzania anayeishi anapata kipato kiasi fulani kama nilivyooanisha hapo juu.

Changamoto yetu ni tufanye nini tupate kipato endelevu na cha uhakika ambacho kitatutosheleza mahitaji yetu ya msingi na mahitaji mengineyo ya lazima kama elimu, afya, usafiri, miundombinu mbalimbali, starehe na burudani.

Namna ya kukipata

Tukishatambua tatizo hilo hilo tutaanza na kuboresha vyanzo vyetu vikuu vya mapato ambavyo kwa nchi yetu ni kilimo hapa ninamaanisha ni pamoja na mifugo, uvuvi, misitu na mazao yake chakula, maji salama, kujenga makazi, ambacho kinatupatia mapato ya kununulia mahitaji yetu ya mavazi na mahitaji mengineyo.

Kwa mfano tunaanzia na yule mkulima mdogo mwenye debe moja la mahindi ajengewe uwezo aweze kulisaga na kuuza unga ambao unaweza kumpatia faida ya ziada kuliko kuuza mahindi yenyewe.

Kwa yule mfugaji anayekamua maziwa lita tano kwa siku kutoka kwenye ng’ombe wake ajengewe uwezo akamue lita 20 kwa siku. Kwa yule mkulima anayeuza mfugo kwa bei ya macho auze kwa kilo yaani mfugo upimwe ajue ana uzito kiasi gani na apange bei kwa kilo moja moja. Kwa yule mvuvi anayevua baharini ajengewe uwezo angalau auze samaki wake kwa mnada badala ya kumuuzia mtu wa kati akiwa ndani ya maji.

Hivyo tutatekeleza kilimo cha kibiashara, ambacho kitatufanya tutumie rasilimali zetu tukifanya kazi na wataalamu ambao kwa kutumia mashine na teknologia za kisasa tutaboresha uzalishaji kwa wingi, ubora na kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani nje na ndani ya Tanzania badala ya kuuza mali ghafi ambayo hayajaongezewa thamani. Hivyo tutakuwa tunazalisha mazao na bidhaa tunazohitaji kwa ajili ya viwanda vyetu. Kwa kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani kwa kushirikiana na wadau wengine tutashiriki kupanga bei badala ya kupangiwa bei na kupata kipato kikubwa na endelevu.

Wakulima watakuwa wanajenga na kuendeleza masoko na bei zao badala ya kutegemea masoko na bei za wachuuzi ambao malengo yao ni tofauti na ya wakulima. Wakulima wanazalisha na kuuza kwa bei moja tu sokoni na kujenga uhusiano wa muda mrefu na mlaji, lakini wachuuzi wananunua na kuuza kwa bei zinazobadilika kulingana na manunuzi yao na hawajali kujenga mahusiano wa muda mrefu kwani wachuuzi wanasukumwa na faida ya wakati huo wanapouza. Kupitia kilimo chetu tutatambua umuhimu wa kilimo cha kisasa na cha kibiashara cha umwagiliaji ambacho itabidi tuvune mvua, tujenge mabwawa, miundombinu ya umwagiliaji, tuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji na kutumia maji kama zao la kibiashara ili kuzalisha mazao yatokanayo na kilimo chenyewe, mifugo, uvuvi na bidhaa za misitu kwa mwaka mzima. Kwa kutumia mbinu hizo tutakuwa tumetatua tatizo la kipato cha msimu na kisichotabirika na tukawa na kipato cha uhakika na endelevu kwa muda mrefu.

Ili kupata kipato endelevu lazima tufanye kazi kwa pamoja na tuhakikishe mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo anakuwa tajiri kabla ya wengine. Wakulima, wavuvi na wafugaji wadogo ambao ndio wengi wakiwa matajiri, kwa kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani kwa bei yao waliyopanga kwa kushirikiana na wadau wengine, kutakuwa na mzunguko mkubwa wa fedha.

Wakulima matajiri wanahitaji bidhaa bora kwa vile wana uwezo wa kununua na kuchochea maendeleo ya viwanda vitakavyotengeneza bidhaa hizo. Wakulima matajiri watahitaji huduma nyingi na bora hivyo watahitaji wafanyakazi wengi wenye elimu na watakaolipwa ujira mkubwa na kufanya vipato vya wafanyakazi kuongezeka.

Wakulima, wafugaji na wavuvi matajiri watahitaji vitendea kazi na teknologia kubwa na zenye ubora wa hali ya juu ambao watachochea utafiti wa teknologia, utengenezwaji wa mashine na teknologia sahihi ambazo zitakidhi mahitaji ya watu na viumbe wengine. Wakulima, wafugaji na wavuvi matajiri wakishirikiana na viwanda na wafanyakazi wenye vipato na kulipa kodi.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji

Africa Rural Development Support Initiative (ARUDESI) Simu: 0715-301494/0752-110290