Afcon U-17 nafasi ya kutangaza utalii

Kwanini mataifa duniani yanagombea kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia? Mataifa ya Afrika yanagombea kuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika? Kuna mengi nyuma ya kuwa mwenyeji wa fainali hizo.

Kwanza, mataifa yanapata fedha kama mwenyeji kuwa nchi mwandaaji. Mfano Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) hutoa mamilioni kwa taifa mwenyeji wa fainali zake.

Kinachofuata, mbali na kutangazika duniani, lakini pia uboreshwaji wa miundo mbinu ya barabara, viwanja, ujenzi wa viwanja vipya na uboreshwaji wa vile vya zamani na wafanyabishara.

Hayo ni mashindano makubwa, Tanzania iko kwenye ramani ya kuwa taifa mwenyeji wa mashindano makubwa ya vijana Afrika kwa walio chini ya miaka 17.

Matarajio makubwa ni uboreshwaji wa miundombinu ikiwemo barabara, viwanja, maeneo ya mawasiliano lakini pia kuboreshwa huduma mbalimbali za kijamii.

Hoteli zitaingiza fedha kwa zile ambazo timu zitakaa na zile ambazo maofisa na watu wengi watakaofika kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa wachezaji watafikia.

Kufanyika kwa fainali za mwaka huu ambazo kila mmoja anataka kuona Tanzania ikilibakisha kombe nyumbani, ni njia ya kutangaza utalii kwa kuwa ujumbe mzito kutoka mataifa saba nchi washiriki watafika.

Akiwa mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa tayari ametia ndimu kwa kuliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kitu cha kwanza na kikubwa ni kuhakikisha Tanzania inatwaa ubingwa katika fainali hizo zitakazoanza Aprili 14 kwa Tanzania kuanza na Nigeria.

Majaliwa alitoa agizo bungeni, mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto.

Mbunge huyo alimtupia swali Waziri Mkuu akitaka kufahamu Serikali imehusika vipi na mashindano hayo ya Afcon na mkakati wa kuendeleza utalii nchini.

Waziri Mkuu anasema maandalizi yote yanaendelea kufanyika na Serikali imejiandaa kupokea wageni hao watakaofika kwa ajili ya mashindano hayo.

Anasema TFF inaendelea na maandalizi ya mashindano hayo baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo.

Alisema Watanzania wanatakiwa kuwa wazalendo na kuipa ushirikiano timu yao ili kuhakikisha inaibuka mshindi kwenye fainali hizo.

UTALII

Waziri Mkuu anasema Wizara ya Maliasili na Utalii itatumia mashindano hayo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Anasema: “Tutawapeleka Kilwa wakaone majengo ya zamani yaliyokaliwa na Waarabu na maeneo mengine yenye vivutio,” anasema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kutumia fursa ya mashindano hayo kufanya shughuli mbalimbali zitakazowapa kipato.

Pamoja na Waziri Mkuu kusema hayo, hakika Tanzania itanufaika kwa kiasi kikubwa. Dunia itakuwa ikiiangaza Tanzania, mataifa ya Afrika yatakuwa yakiiangaza Tanzania lakini zaidi ni kuutangaza utalii.

Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii kama Mbuga za Wanyama, maziwa na mlima mrefu Afrika, Mlima Kilimanjaro.

Haina ubishi kwamba ujio wa timu saba za vijana utaitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali za utalii.

Kama kutakuwa na utaratibu wa usafiri, wageni wanaweza kwenda kuona Mbuga za wanyama au mlima Kilimanjaro wakati wapo hapa nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Professional Adolf Mkenda anasema suala hilo wamelikabidhi kwa Bodi Utalii Tanzania ambao watajipanga na kujua watatupa vipi fursa hiyo.

Akizungumza na Spoti Mikiki, Profesa Nkenda anasema: “Ni mapema kusema tutafanya nini lakini tumeshawapa kazi hiyo Bodi ya Utalii (TTB) wakae na wajue nini cha kufanya katika mashindano hayo halafu ndio tutaweka wazi mwelekeo wa Tanzania na azma ya utalii.”

Mmoja wa wafanyabiashara katika soko la vinyago Mwenge, Ally Abdallah anasema inawezekana wakanufaika na uwepo wa mashindano hayo lakini tu endapo watapata fursa ya kuruhusiwa kupeleka biashara zao uwanjani au katika hoteli watakazofikia timu Shiriki.

“Hizo timu kuja mpaka huku kuangalia biashara za vinyago tunazofanya sidhani Kama wataweza lakini nafikiri wahusika wangeruhusu kuwepo na hata na maonyesho ya biashara kama hizi ndani au hata nje ya uwanja ili kuwavutia wageni” alisema Abdallah.

Wafanya biashara nao wamo

Kati ya watu wengine watakaonufaika na mashindano hayo ni wafanyabiashara ndogo ndogo ikiwemo mama lishe na wauza jezi, maji na wafanyabiashara.

Wafanyabiashara hao ambao hukaa nje ya uwanja watapata fursa ya kuuza bidhaa mbalimbali kwa mashabiki watakaofika kutazama mechi hizo.

Pia wafanyabiashara wengine ambao wanakuwa ndani ya uwanja ambao huuza vinywaji,vitafunwa na ice cream nao watavuna pesa nyingi katika mashindano hayo kwani watapata fursa ya kuuza bidhaa zao kwa mashabiki na hata wachezaji.

Mmoja wa wafanyabiashara wa vinywaji kwenye Uwanja wa Taifa, Naima Hassan alisema wanasubiri kwa hamu kubwa mashindano hayo ili waweze kupata pesa.

“Kwa kweli tunayasubiri kwa hamu hayo mashindano kwani naamini yatatupatia kipato kwa sababu tutafanya biashara kwa mashabiki watakaonufaika kutazama mechi hizo”alisema Naima