Aina tano za uongo ambao wagonjwa wanapenda kuwaambia madaktari

Sunday February 24 2019Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

By Dk Chris Peterson

Tabia ya kutosema ukweli kwa daktari ipo kwa wengi. Huenda sababu ikawa ni aibu mathalani inapotokea mgonjwa ana tatizo nyeti la kiafya na muhudumu wake wa afya au daktari wake ni wa jinsia tofauti.

Lakini aibu nyingine husababishwa na tofauti ya umri na hasa inapotokea kuwa umri wa daktari ni sawa na wa mgonjwa.

Ifahamike kuwa, katika sehemu ambazo unatakiwa kuwa huru na mkweli basi ni kwenye chumba cha daktari. Ukweli utamsaidia daktari wako akupe huduma bora zaidi kutokana na kile ulichokipitia siku chache kabla hujapata tatizo.

Sikunywa pombe

Wagonjwa wengi hukumbwa na aibu kueleza kwa daktari kama wamekunywa pombe muda mfupi kabla ya kwenda hospitali kwa matibabu ya dharura.

Wakati unafikiria kumdanganya mtoa huduma wako wa afya unapaswa kuufahamu ukweli kwamba unywaji wa pombe unaweza kutoa majibu tofauti na tatizo lako kiafya ikiwa unalazimika kufanyiwa vipimo vya aina mbalimbali.

Nimeacha kuvuta sigara

Unaweza kudhani ni jambo la kawaida ili kumficha mtoa huduma wako kama unavuta sigara, kuna umuhimu mkubwa yeye kujua ukweli huu. Baadhi ya tiba hasa ya vidonge inaharibiwa na utendaji kazi wake mwilini na ile sumu inayopatikana kwenye moshi wa tumbaku, kitaalamu Nicotine. Baadhi ya dalili za matatizo mbalimbali ya kiafya husababishwa na uvutaji sigara kama vile kukohoa mara kwa mara, kupungua uzito kwa kasi na maumivu makali ya kifua.

Ni vyema kumwambia daktari kuwa pamoja na dalili hizi lakini pia unavuta sigara kama una tabia hiyo.

Sikufanya tendo la ndoa

Hapa ndipo kwenye tatizo kubwa wagonjwa wengi wanakuwa wagumu eneo hili hasa inapofika kwenye tiba ya magonjwa ya zinaa na afya ya uzazi kwa ujumla. Sababu kubwa hapa ni aibu.

Wengi hujikuta wanapata magonjwa ya zinaa kutokana na tabia ya kufanya ngono isiyo salama wakati mwingine na washirika tofauti tofauti ndani ya kipindi kifupi.

Sina magonjwa ya zinaa

Kama una gonjwa lolote la zinaa basi unapaswa kukubaliana na ukweli kuwa una ugonjwa huo. Lakini hata kama ulikuwa na gonjwa la zinaa hapo awali, daktari pia anapaswa kujua. Unaweza ukaona aibu kusema lakini unapaswa kujua ukweli kuwa baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kuwa hatari kama hayakupatiwa tiba stahiki.

Pia ni vyema kufahamu kuwa hata kama uliwahi kuwa na ugonjwa wowote wa zinaa na baada ya muda ukatoweka, upo hatarini kujirudia usipotibiwa.

Sina tatizo la nguvu za jinsia

Eneo lingine ambalo wagonjwa wangu huwa wagumu kusema ukweli ni kwenye nguvu za jinsia. Kukosa nguvu za jinsia ni tatizo linaloathiri jinsia zote mbili.

Japo imezoeleka wanaume mara nyingi ndio wenye tatizo hili lakini hutokea hata kwa wanawake wakati wa kufanya tendo la ndoa.

Hii inaweza kuashiria matatizo mbalimbali kiafya kama shinikizo la damu (kuwa la juu au la chini), kisukari na magonjwa na mengine. Hivyo ni vyema kumjulisha daktari bila kujali aibu na hasa ikitokea unalipata tatizo hili ukiwa umri haujafikia uzeeni. Kwa kufanya hivyo utamsaidia daktari kukupa tiba ya uhakika ikiwamo yale ya kisaikolojia.

Advertisement