Ama kweli kila mwaka mpya una mapya yake

Saturday December 29 2018GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

“Mwaka Mpya ni ukurasa wa kwanza katika siku 365 zitakazoufuatia.

Ni ukurasa mpya usio na maandishi, hivyo chochote utakachokiandika kitatangulia mbele ya kurasa hizo nyingine. Jaribu kuandika mema ili mwaka wako usimame katika wema. Hiyo ndiyo tafsiri yangu kwa yaliyonukuliwa kutoka kwa Brad Paisley, mwanamuziki wa Marekani.

Nukuu hii inanikumbusha tulivyofanya mara tulipoona nyota ikikatiza angani katika siku hiyo.

Kila mmoja alinuiza kwa sauti au kwa kunong’ona yale aliyopenda yamtokee katika mwaka huo.

Pia nakumbuka katika desturi za Ulaya watu walinuiza kwenye visima vya kale vilivyojulikana kama wishing wells katika siku ya kwanza ya mwaka.

Siku hizi mbili (ya mwisho na ya mwanzo wa mwaka) zimepewa umuhimu wa kipekee katika jamii zetu. Zipo taratibu zilizoigwa kutokea zama zile na baadhi yake zingali zinafuatwa mpaka hivi sasa. Zipo za kiimani, kimila na hata za kichawi zinazoendelezwa duniani kote; hata kule kwenye dunia ya kwanza.

Pamoja na kwamba watu wanahamasishana kuanza mapya mara mwaka mpya unapogeuka, bado tamaduni za kale za jamii fulani zinazidi kupanuka kiasi cha kuambukiza kwa wengine.

Mwandishi mmoja alisema, “Maneno ya mwaka jana yalihusiana na mwaka huo, mwaka mpya unasubiri maneno mengine…”

Hata hivyo ukiachilia mbali idadi kubwa inayofunga na kufungua mwaka kwa sala na dua, bado ipo idadi kubwa nyingine inaendeleza manuizo kama walivyofanya babu zao. Utamaduni huu umeonekana kuchukua kasi kubwa kuanzia mwaka 2000 ambao ni mmoja kati ya miaka iliyotabiriwa mengi zaidi.

Kwa wengi hii ni siku ya kuepukana na kila jambo baya. Kuna watu wanaamini kuwa chakula cha mwaka mpya ni lazima kiwe maalum. Hapa nyumbani kuna mazoea ya kupika pilau, biriyani au chakula cha sherehe ambacho si mara kwa mara kinatumika. Wazungu wanapendelea chakula kinachokaushwa kwa moshi wakiamini kuwa ndio njia ya kuondoa mikosi.

Kwa sababu mwisho wa mwaka ni kipindi cha mvua kwenye ukanda wa tropiki, wengi hupenda kuoga mvua wakiamini kuondoa mikosi ya mwaka unaoagwa. Lakini wengine hawaogi, kufua wala kufagia uwanja siku ya mwisho wa mwaka kwa kuhofia kufukuza bahati.

Jamii fulani huahirisha shughuli za msiba kuepusha kufanyika wakati wa sikukuu ya mwaka mpya. Kwa mujibu wa taratibu za jamii hizi, shughuli zozote zitakazofungua mwaka kwenye jamii zitashamiri katika mwaka mzima. Hivyo sikukuu ya tarehe moja huzingatiwa kipekee sana.

Wageni wa mwanzo kabisa kwenye sikukuu nao wanamaanisha mambo tofauti. Katika nyumba wanazoishi jinsia ya kike wageni wa kiume huashiria ndoa, na kwenye nyumba za wasela wageni wa kike huleta baraka ya aina hiyo. Pia kama umejaliwa watoto wa kike pekee, watoto wa kiume wakitangulia kuingia nyumbani huleta baraka ya uzazi wa watoto wa kiume kwenye familia hiyo.

Wapo wanaootesha mimea maalum na kuvaa nguo za bahati katika siku hiyo. Wengine huamini kuwa wakifunga ndoa tarehe moja ya mwaka mpya basi watadumu kwa muda mrefu zaidi. Kwenye baadhi ya sehemu hata wanyama wanapumzishwa kwenye malisho mabichi.

Kitu kingine kinachovutia zaidi ni kutokuchinja wanyama kwa baadhi ya watu.

Inaaminika kuwa iwapo utachinja hata ndege katika siku hii muhimu utakabiliana na upotevu na upungufu wa bahati pamoja na fedha.

Wanaongeza kuwa kula mboga za majani kama kunde na spinachi wakati huu kunavutia utajiri.

Zipo imani za kishirikina katika Ulaya zinazoelekeza kuwa paka au mbwa wanapolia watu wanapaswa kuelekeza nyuso zao pande tofauti na zinakotokea sauti hizo. Zinasisitiza kuwa wanyama wakilia hukaribisha watu waovu katika mwaka mzima unaokaribishwa.

Masuala ya imani huenda yakawa yanatekelezwa kwa nguvu sana wakati wa sikukuu ya mwaka mpya. Kama nilivyotangulia kueleza, wengi huaga na kukaribisha mwaka kwenye nyumba za ibada. Lakini wapo wanaokesha kwa masangoma au kufanya mambo tofauti yanayotafsiriwa kama ushirikina.

Na kwa sababu imani ni matumaini ya mtu binafsi, hata yale yanayotajwa kuwa ushirikina huhesabiwa kama imani na washiriki wake. Kinachozingatiwa ni kanuni za kikatiba ambapo yeyote anakuwa huru kuamini chochote ili mradi tu asivunje sheria zilizowekwa.

Haishangazi kuona nyumba zilizoning’inizwa tunguli au ndimu milangoni katika siku ya mwisho au ya mwanzo wa mwaka. Wapo wanaoamini kuwa kufanya hivyo kunazuia pepo wachafu, hivyo wataishi bila kusumbuliwa katika kipindi cha mwaka mzima.

Ushirikina mwingine unazuia matumizi ya fedha. Kama tarehe moja ya Januari unatarajia kutafuta au kulipwa ni wazi hautafanikiwa katika mataifa fulani fulani. Watu wanafanya manunuzi siku chache kabla ya mwaka mpya na hawako tayari kuuanza mwaka kwa kulipa au kutoa hata senti.

Kifupi ni kwamba mwaka mpya wako ni siku mpya. Isikukute ukiwa na maumivu yoyote ya mwaka ulipita au fikra mpya ambazo si nzuri. Usithubutu kuuaga mwaka ukiwa apeche alolo. Fanya kila linalowezekana angalau uwe na vijisenti vya kula nyumbani na kukidhi angalau wageni wawili. Hii ndio ileile ya kula au kuvaa vizuri kabla hujaupokea.

Advertisement