Amegoma kunitambulisha kwa familia yake, nifanyeje?

Sunday April 14 2019

 

By Anti Bettie

Nimeishi naye kwa miaka sita sasa, cha kushangaza kila nikimuomba anitambulishe kwa jamaa zake hataki.

Nataka kupeleka posa ila hadi anitambulishe kwa baadhi ya ndugu zake kwanza.

Nifanyeje?

Nakujibu kwa heshima ya huyo dada unayeishi naye, tofauti na hapo ningekaa kimya, unaishi na mwanamke kinyumba kwa miaka sita na hujatoa hata posa kisha unataka akupeleke kwa ndugu zake?

Hilo haliko sawa, akutambulishe kwanza kwa ndugu zake ndiyo unaotaka kuishi nao?

Acha mzaha na binti wa watu bwana, peleka posa kwao umuoe.

Kwa tamaduni za Kiafrika mwanamke unaishi naye tu kienyeji siyo rahisi kukutambulisha kwa jamaa zake. Ukiutaka utambulisho huo tena rasmi anza mikakati ya kumuoa acha kumchezea na kujiona una haki ya kutambulishwa kwa familia yake. Funga naye ndoa uwajue ndugu zake kihalali.

Wanaume hamuwafikishi wenza wenu kileleni...

Habari Antie nimeolewa mwaka wa tatu sasa lakini kufika kwenye mshindo kwangu ni mara moja kwa mwaka.

Kila ninavyojitahidi sifanikiwi.

Nifanyeje?

Hili ni swali linaloulizwa na wanawake wengi, wanaume inabidi mjitafakari katika hilo kama kweli mnafanya kazi inayowahusu ipasavyo.

Wanaume jitahidini kuwatafuta wenza wenu ashki zao zilipo, tofauti na hapo mtabaki kujisifu mnawaridhisha kumbe wanaigiza ili wapumzike kwa sababu hawaoni dalili za kufanikiwa na nyinyi mpo bize mkiamini mnachokifanya bila kuwashirikisha hao mnaofanya nao.

Wanawake na nyinyi pia semeni kama hamridhiki, kulalamika bila ya kuchukua hatua ya kuwaeleza wenza wenu kuwa hamridhiki, acheni kudanganya hata kama mmechoka.

Unaposhiriki ukiona sehemu kakushika unaridhika mwambie asiache, shirikiana naye, usione haya huyo ndiyo mumeo kwa sababu usipofanya hivyo hutafurahia raha ya tendo maishani mwako.

Vunjeni ukimya semeni mnapoona mnatumika bila kumaliza, lazima ufike mshindo, usikubali kulipuliwa.

Hataki nijiendeleze kielimu

Habari. Naomba unisaidie mumeo wangu hataki nijiendeleze kielimu.

Nifanyeje?

Kwanza kwa faida ya wanaume kumuendeleza mwanamke ni kuendeleza jamii, hivyo msiwabanie wenza wenu kujiendeleza kielimu.

Inawezekana wapo wanawake ambao hata kama hawajasoma wanaelewa mnapojadiliana, lakini wengi wao wakiwa hawajasoma inakuwa ngumu kuelewana kati yenu kwa sababu vitu vingi anakuwa hajui.

Shagaangu na wewe angalia muda unaomwambia suala lako la kusoma, tena ukiwa na sababu maalumu za kufanya hivyo badala ya kumueleza juu juu.

Hakikisha unamrai akusikilize, ukizungumza naye suala asilolipenda kikawaida kawaida hawezi kukuelewa, tumia mbinu za kike na hakikisha hicho unachosoma kinakutoa sehemu moja kukupeleka nyingine.

Wanawake pia muwe na busara kwenye maisha ya kawaida ili iwe rahisi mnapokuwa na jambo la msingi la kujadili na wenza wenu iwe rahisi kusikilizwa, ukiwa unazungumza pumba kila siku, hata ukiwa na jambo la maana hawezi kukusikiliza.

Advertisement