Anza hivi mradi wako wa kuku wa asili

Unapofikiria kutaka kuanzisha mradi wa kuku wa kienyeji, unapaswa kuzingatia baadhi ya mambo muhimu. Makala haya yanakusaidia kuangazia baadhi ya mambo hayo.

Ili upate kundi lenye kuku bora huna budi uchague jogoo bora na matetea bora wa kuzalisha kundi lako.

Angalia sifa zifuatazo unaopotaka kuchagua kuku wa kuanza mradi wako:

1. Tetea na jogoo wawe na umbo kubwa. 2.Wanaokua haraka. 3. Wenye uwezo wa kustahimili magonjwa. 4.Matetea wanaoweza kutaga mayai mengi. 5.Matetea wanaoweza kuatamia na hatimaye kutotoa vifaranga kwa wingi na kuvilea. 6.Jogoo unaowachagua kwa ajili ya matetea au makoo yako wasiwe na uhusiano wa damu.

Ukiishachagua kuku wazazi wa kundi lako, changanya jogoo na matetea kwa uwiano wa jogoo mmoja kwa matetea 10 hadi 12. Ukiwa na matetea 20 utahitaji kuwa na majogoo wawili.

Hapa nchini kwetu zipo aina tofauti za kuku wa asili ambao wana sifa tofauti. Wafugaji wengi hufuga kutegemeana na uwezo wa kuku kuhimili magonjwa, kuwa na uzito mkubwa, utagaji wa mayai mengi n.k.

Koo za kuku wa asili wenye sifa za namna hii ni aina ya Bukini, Kuchi, Kuchere na wa kawaida wasio na ukoo maalum.

Hawa kwa ujumla wao wakitunzwa vizuri wana uwezo wa kufanya vyema katika mazingira ya nchi hii kwa sababu wameshayazoea.

Kuatamia na kuangua mayai

Baada ya jogoo kupanda matetea au makoo, hawa watataga mayai. Mayai yanaweza kutotoleshwa kwa njia ya asili au kwa kutumia vifaa vya kutotolesha.

Kutotoa kwa njia ya asili

Hii inafanyika kwa kuku kuatamia mayai kwa hatua zifuatazo:

1. kuandaa kiota

• Kiota kiandaliwe kabla kuku hajaanza kutaga kwa kukiwekea nyasi kavu na kuzisambaza kwa kutengeneza muundo wa kata au sahani iliyozama kidogo.

• Kiota kinyunyiziwe dawa ya unga kuua wadudu kabla na baada ya kuweka nyasi. Iwapo kuku atajiandalia kiota chake mahali panapofaa aachwe hapo ila kiota kiwekewe dawa ya kudhibiti wadudu.

2. Maandalizi ya kuku anayetaka kuatamia

Dalili za kuku anayetaka kuatamia ni kutoa sauti ya kuatamia, kusinyaa kwa ushungi wake, hapendi kuondoka kwenye kiota, hupenda kujikusanyia mayai mengi

Kuku mwenye dalili za kutaka kuanza kuatamia akaguliwe ili kuhakikisha kuwa hana wadudu kama utitiri, chawa, viroboto n.k. wanaoweza kumsumbua wakati wa kuatamia. Akiwa na wadudu watamsumbua hataweza kutulia kwenye kiota na kuatamia vizuri. Matokeo yake ataangua vifaranga wachache.

Hivyo kuku mwenye wadudu mnyunyizie dawa ya unga kabla hajaanza kuatamia ili kudhibiti tatizo hili.

Kuku anapotaga mayai yaondolewe na kubakiza moja kwenye kiota ili kumwita kuku kuendelea kutaga. Kuku akiwa tayari kuatamia awekewe mayai kwa kuatamia. Kwa kawaida kuku mmoja anaweza kuatamia vizuri mayai 10 hadi 13 kwa wakati mmoja.

Kipindi cha kuangua mayai ni kuanzia siku 20 baada ya kuatamia. Ukitaka kutotolesha vifaranga wengi kwa wakati mmoja, kuku akianza kutaga yakusaye mayai yake na kumbakizia yai moja ili aendelee kutaga.

Makala kwa hisani ya Rural Livelihood Development Company