App hizi za elimu kuvutia wengi 2019

Tuesday January 8 2019

 

By Elizabeth Tungaraza

Kukua kwa sayansi na teknolojia kumesababisha vijana wengi nchini kuendelea kuvumbua ‘Apps’ mbalimbali.

Tunapouanza mwaka 2019, ni vyema kuangalia app chache ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika sekta ya elimu kwa jumla.

SOMA App

Hii ilizinduliwa mwezi Februari 2017, chini ya mwanzilishi wake Isaya Yunge. ‘App’ hii inapatikana katika simu na inatoa furasa za kielimu hasa kwa wale wanafunzi ambao wanakosa mikopo.

App hii inasaidia wanafunzi kupata ufadhili wa kimasomo nje ya nchi.

Tangu imeanzishwa zaidi ya wanafunzi 450 wamenufaika kwa kupata ufadhili kupitia SOMA ‘App’ na Jumla ya kiasi cha Dola za Marekani 850,000 zimetumika kulipia wanafunzi kutoka Tanzania, Uganda,Rwanda, na Nigeria.

‘App’ hii inaruhusu mwanafunzi kuingiza matokeo yake na yenyewe inakusaidia kukutafutia chuo kulingana na matokeo kwa kufananisha na aina ya ufadhili unaouhitaji.

Jumla ya watumiaji 2000 hutumia ‘App’ hii kila siku na jumla ya watu 18,500 wameipakua.

Wakati huo huo jumla ya watu 950 kwa mwaka jana walipata ufadhili wa kulipiwa kila kitu. Kupitia App hii Isaya Yunge alitunukiwa tuzo na Malkia Elizabeth wa Uingereza.

MyElimu App

Hii pia imefanya vizuri mwaka jana na inaendelea kufanya vizuri katika sekta ya elimu chini ya mwanzilishi wake Given Edward. Kupitia App hii mwanafunzi anaweza kujifunza kupitia video zenye sekunde 15 ambazo atazipata kupitia mitandao mbalimbali kama instagram na twitter.

App hii inasaidia wanafunzi wote ngazi ya Sekondari kujifunza kwa njia ya majadiliano, ambapo mwanafunzi yeyote kutoka popote pale Tanzania anaweza kuanzisha mjadala kuhusu somo lolote au mada yoyote ile na ikajadiliwa na wanafunzi wengine.

Pia hata yule ambaye hatokuwepo hewani wakati wa mjadala akiingia ataona na kusoma kila kitu wenzake walichojadili.

Kupitia ‘app’ hii Given alitunukiwa tuzo na Malkia Elizabeth wa Uingereza. Anasema wakati anaianzisha ilikuwa na wanafunzi 157, lakini mpaka sasa ina jumla ya wanafunzi 42,000 wanaoitumia kila mwezi.

Kupitia App hii wanafunzi wanatiana moyo, kuelekezana pale mtu asipoelewa.

TESEA APP

‘App’ hii ilizinduliwa katikati ya mwaka jana chini ya mwanzilishi wake Abdul Mombokaleo. ‘App’ hii inapatikana katika simu za mkonon na Ipad maalumu.

Kupitia App hii walimu na wanafunzi wa ngazi ya sekondari wanaweza kujadiliana na kuelekezana.

Abdul anasema wazo lilikuja ili kusaidia kuinua na kuboresha mazingira ya elimu Tanzania ukizingatia bado kuna ukosefu wa vitendea kazi kama madarasa, vifaa vya kufundishia, maktaba na maabara za kutosha pamoja na upatikanaji wa vitabu. Vile vile kuna tatizo la Watanzania wengi kutopenda kujisomea.

Mombokaleo anasema kupitia ‘App’ hii mwanafunzi ana uwezo wa kwenda kujisomea zaidi kwa kuwa kuna upatikananji wa zana za kujifunzia za kutosha.

Hivyo mwanafunzi akifundishwa bado ana nafasi kubwa ya kwenda na kujifunza kiundani zaidi na huko ana uwanja mpana wa kujifunza kutoka kwa walimu tofauti na wanafunzi tofauti kutoka Tanzania .

Mpaka sasa jumla ya watumiaji 3000 wamepakua na kunufaika na ‘app’ hii.

Advertisement