Asia DC anayepambana na mimba utotoni

Kati ya masuala aliyoanza kupambana nayo mara baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa ilikuwa ni kuhakikisha anapambana na tabia ya watoto wa kike kuacha masomo baada ya kupata mimba na kwenda kufanya kazi za uyaya mijini.

Asia Abdallah anaamini watoto wa kike na kiume wanaweza kutimiza ndoto zao kama watapewa malezi na elimu bora.

Ni ukweli usiopingika kuwa, kazi za ndani ni kikwazo kwa wasichana wengi wa mkoa wa Iringa hasa wilaya hiyo ya Kilolo.

Baadhi ya wazazi huona ni afadhali mtoto wa kike akimaliza darasa la saba akafanye kazi za ndani badala ya kuendelea na masomo, hata kama anakuwa amefaulu.

“Niliwaambia kabisa viongozi wa vijiji, wazazi na hata walezi kwamba sitataka kusikia eti mtoto wa kike amefaulu halafu anapelekwa Dar es Salaam kufanya kazi za ndani,” anasema Asia.

Anasema kati ya vitu vinavyomnyima usingizi ni ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Sipendi kusikia mtoto amebakwa au kulawitiwa. Kwa kweli hii ni changamoto tunapambana nayo,” anasema.

Anasema kiuhalisia, mtoto anahitaji kupendwa, kuenziwa, kutunzwa na si kuumizwa tena kwa makusudi.

Amefanya nini tangu ateuliwe?

Anasema yapo mambo mengi yaliyofanyika wilayani Kilolo tangu awamu ya tano ilipoingia madarakani, yeye akiongoza wilaya.

“Natimiza wajibu wangu ipasavyo katika kusimamia sekta zote muhimu ili Kilolo isiwe nyuma. Iendelee kusonga mbele na mwisho wa siku wananchi wawe na uchumi imara,” anasisitiza.

Katika elimu anasema aliikuta wilaya hiyo ikiwa na hali mbaya na wakati mwingine ikishikilia mkia kwenye matokeo ya mitihani.

Anasema alichofanya katika kukabiliana hilo, ilikuwa ni kuwahamasisha wadau wa elimu kila mmoja kwa nafasi yake akiamini ushirikiano wa kada zote unaweza kuinua taaluma ya wilaya hiyo.

“Baadhi ya shule zilikuwa zinawalalamikia walezi au wazazi wanaotaka binti zao wasifanye vizuri ili wakifeli wakafanye kazi au kuwaozesha. Baada ya kutangaza kuwachukulia hatua wazazi na walezi wenye tabia hizo, mambo yalianza kubadilika, kiwango sasa kimepanda.

Takwimu za Kilolo zinaonyesha kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 71.14 mwaka 2015 hadi zaidi ya 85 kwa miaka iliyofuata.

Mafanikio mengine katika sekta ya afya akisema, “Tunaendeleza ujenzi wa hospitali ya wilaya uliokuwa umesimama kwa ukosefu wa fedha, tunachotaka ni wananchi kupata huduma stahiki za afya ndani ya wilaya. Tumekamilisha ujenzi wa zahanati za Kipaduka na Ndingisivile pamoja na wodi ya kulaza wagonjwa iliyojengwa kwa ushirikiano na kampuni ya New Forest.Ameendelea kuwahimiza wananchi kuachana na kilimo cha kujikimu na badala yake wajikite kwenye kilimo cha biashara ambacho kinachoweza kuwainua kiuchumi.

Mbali na mazao ya chakula, yapo mengi ya biashara na mkakati mkubwa ni kuwapo kwa viwanda. Anasema ndani ya wilaya hiyo kimejengwa kiwanda cha nyanya cha Dabaga kitakachosaidia wakulima kusindika mazao yao.