Asilimia 42 ya walioachana hutamani kurudiana na wenza wao

Sunday November 25 2018

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Imebainika kuwa asilimia 50 ya wanandoa hujuta muda mchache baada ya kupeana talaka.

Licha ya Utafiti wa kufuatilia kaya Tanzania (National Panel Survey) wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuonyesha kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka kutoka asilimia 1.1 mwaka 2008/09 hadi asilimia 2.1 mwaka 2014/15, wanandoa hujutia kuachana kwao.

Pamoja na hayo, watakaokuwa na nafasi ya kunusuru ndoa zao ni wanandoa wanne kwa kila 100 ambao wametengana, jambo linaloashiria huenda nao wakatalikiana siku zijazo iwapo hawatapata suluhu ya kudumu ya tofauti zao.

Wanaweza kunusuru kutokana na matokeo ya Utafiti uliofanywa na gazeti la mtandaoni la Daily Mail ulibainisha kuwa asilimia 50 ya wanaoachana hujutia kuachana na wenza wao.

Jarida hilo lilieleza kuwa asilimia 42 ya waliokuwa wakipambana kurudisha ndoa zao baada ya kila mmoja kukaa kwake na kubaini amemkumbuka mwenzake, asilimia 21 wanaishi na wenza wao sasa baada ya kufanikiwa kuzinusuru.

Nusu ya hao walisema kuwa baada ya kurudiana ndoa yao imekuwa imara kuliko mwanzo.

Miongoni mwa wanawake wanaojutia kutalikia na mumewe ni pamoja na mwandishi maarufu wa vitabu Jane Gordon.

Gordon ambaye ametunga vitabu maarufu kama My Fair Man, Stepford Husbands na hard Pressed aliwaambia waandishi wa jarida la Daily Mail ambao walifanya utafiti huo uliohusisha watu 2000 , kuwa alijutia kuachana na mumewe muda mfupi baada ya kuchukua hatua hiyo.

Mama huyo wa watoto watatu alisema kuwa aliachana na mumewe waliyeishi kwa miaka 25 bado anajutia kitendo hicho licha ya kupita miaka 12 sasa.

“Tulipofikia maamuzi ya kuachana , nilijua nimepata suluhisho la matatizo yangu, baada ya kupata talaka, nilibaini kuna kitu hakipo sawa, ”alisema Gordon.

Jarida hilo limeeleza kuwa utafiti huo ulihusisha watu 2000 wanaume na wanawake kutoka nchi za Ulaya , ambao wameachana au waliopo kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka mitano.

“Kupeana talaka ni hatua mbaya kwenye uhusiano na wakati mwingine kutamka neno nataka talaka yangu hutokea wakati wa malumbano na hasira.

“Lakini ukikaa chini ukitulia utabaini kuna kitu umefanya, lakini hakuna ulichonusuru na ukitaka kuvirudisha kama vilivyo utakuwa umechelewa, ”alisema mmoja wa wanawake waliohojiwa.

Utafiti huo ulibaini kuwa mmoja kati ya watu watano hujuta muda ule ule baada ya kupewa au kutoa talaka.

“Niliomba talaka kwa hasira kutokana na mambo aliyokuwa akinifanyia, lakini aliponipa alinipa na adhabu inayoniumiza hadi leo ya kunikatalia kuondoka na watoto wangu.

“Nilijutia talaka na nimekuwa mtumwa kwa sababu nilijikuta bado nampenda na watoto wangu natamani kusikia habari zao kila mara, ”anasema Siwazuri Abdallah mhudumu kwenye hospitali ya umma hapa jijini.

Anasema miezi sita baada ya kutalikiana walianzisha uhusiano wa kimapenzi ambao pia haukudumu kwa sababu kila mmoja alikuwa anatamani kitokee kitu kilichoshindikana.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka anasema kuwa vijana wengi huoa au kuolewa bila kujua thamani ya ndoa, ndiyo maana hudai talaka bila kutafakari matokeo yake hujutia.

“Ndoa imethaminiwa kwenye dini na iwapo mmoja kati yao atadai talaka kila kilichomo duniani hulalamika, kwa umuhimu huo lazima waliotalikiana watapata mshituko na mara nyingi huomba kurudiana, ”anasema Mataka.

Mataka anafafanua kuwa ndiyo maana kwa Waislamu kuna muda wa miezi mitatu wa eda ya ndoa, hii inasaidia kila mmoja kujitafakari kama kweli amemchoka mwenza wake.

Wanasaikolojia wanena

“Kisaikolojia mtu yeyote uliyekuwa naye karibu, achana na mwenza wako, hata kama amekuudhi hasira zikipoa kama ulimsemea maneno ya hovyo utajutia. “Kwa wenza ndiyo zaidi, kulingana na watu niliowahi kukutana nao kuhusu ushauri wa kindoa na kuachana asilimia 90, walikuwa wakiomba ushauri wa jinsi watakavyoweza kurudi kuishi kama zamani na wenzao wao waliojaribu kuachana, ”anasema Modester Kamongi mtaalamu wa saikolojia.

Kamongi anasema kuwa wanawake ndiyo mara nyingi huwa wa kwanza kujirudi kama wameachana kwa makosa ya kifamilia, wanaume hujirudi iwapo wameachana kwa makosa ya usaliti.

“Wanawake mara nyingi kesi zao ni wivu, matunzo ya familia, wanaume kushutumiwa kuwa na uhusiano, kuzaa nje ya ndoa, ila kwa waliozaa ukiwauliza wana muda gani tangu waachane hakuna aliyezidi mwaka mata ni miezi mitano, sita, ”anasema.

Anasema anapowasikiliza hubaini kila mmoja kuona thamani ya mwenzake anapokuwa mbali naye , wakiwa pamoja hawathaminiani.

Anafafanua kuwa ana ushahidi wa ndoa kadhaa zilizo na furaha na amani leo hii baada ya kuachana na kurudiana, ambapo kabla ya kufanya hivyo walikuwa wakilaumiana sana na kulumbana kwa kila jambo.

Anaeleza kuwa “Hata wale wasiorudiana , husukumwa na kiburi na aibu, lakini kisaikolojia hakuna ambaye hamkumbuki mwenzake kwa namna moja ama nyingine, na hii hutokea mapema baada ya kuachana”.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Dar es Salaam Josephine Tesha anasema kuwa zipo sababu nyingi za wanandoa walioachana kujuta, ila kurudiana kwa sababu ya watoto, kujuana vizuri na kila mmoja kutambua thamani ya mwenzake akiwa mbali zinajirudia. Anasema wanandoa wengi hufikia maamuzi ya kuachana linapotokea jambo kati yao linalowafarakanisha, hivyo wanakuwa hasira zinazosababisha wafanye maamuzi bila kufikiri mara mbili.

“Kila mmoja hujiona yupo kwenye matatizo na talaka ndiyo njia pekee ya kuepuka, ”anasema.

Anafafanua kuwa wanapokaa mbalimbali kama wana watoto watawasiliana au kukutana mara kadhaa na kujikuta wamekuwa marafiki.

Anasema, “Wanapowasiliana wakiwa mbalimbali kila mmoja anamsoma mwenzake na kugundua kitu kipya na kuona alikosea kuachana naye, ”anasema.

Anaeleza kuwa wapo walioachana na kukasirikiana kabisa, lakini baada ya muda mrefu au mfupi huongozana kuomba ushauri wafanye nini kumaliza tofauti zao.

Advertisement