UCHAMBUZI: Awamu ya Magufuli na wasomi vichomi

Ndiyo! Wameifanya Bongo iwe hapa ilipo. Kwa sababu Mswahili akipata elimu huamini ni daraja la kujitenganisha na jamii inayomzunguka. Kumbe mtu anaelimika ili asaidie jamii. Lakini kwetu usomi ni fimbo kwa mnyonge. Inauma.

Hata watu wakiwa katika mabishano. Msomi atakimbilia kwenye usomi wake. Kwamba hawezi kubishana na asiyesoma, badala ya kumsaidia kupitia elimu yake.

Tuna hasara kubwa zaidi kwa wasomi kuliko faida. Kwa sababu madudu mengi yaliyopo yamefanywa au kuletwa na wao. Fuatilia.

Wasomi kwa mataifa ya wenzetu wamejikita kwenye utendaji. Kwetu wanaacha utendaji wanajikita kwenye siasa na shughuli haramu. Hata waliopo kwenye utendaji wapo ni kwa ajili ya matumbo yao na siyo kujenga nchi au kusaidia jamii. Inasikitisha.

Mikataba ya hovyo kwenye madini ilisainiwa na wasomi na wengi bado wapo kwenye nafasi nyeti. Ubinafsishaji holela kwenye mashirika ya umma ulifanywa na wao. Sheria mbovu zilitungwa na wao. Hawa ni janga kama majanga mengine. Kikokotoo cha pensheni kilicholeta balaa, wahusika ni wasomi wetu. Bungeni kilipitishwa kwa wingi wa kura zao. Wakiwamo maprofesa na madaktari waliosusa kazi ya kufundisha watoto vyuoni na kujikita kwenye siasa. Hawana soni.

Walituaminisha kwa nguvu kuwa kikokotoo kipya ni nafuu kwa wastaafu. Wakatuzodoa sana. Haohao wakawa wa kwanza kushangilia Rais alipositisha. Wakidai kuwa ni Rais wa wanyonge. Hawakutaka tupinge sheria ya kikokotoo, sasa wanataka tuandamane kupongeza hatua za Rais kuzuia. Wasomi wetu ni vichomi. Alah! Kumbe walijua kwamba walichopitisha si rafiki kwa wanyonge? Kichekesho!

Kila kitu nchi hii kinapangwa au kuratibiwa na wasomi. Kwa maana hiyo mkwamo wowote unachagizwa na akili za viumbe tunaowaita wasomi. Mitaro ikitapisha maji mitaani ni kazi ya wasomi. Ujenzi wa kiholela ni kazi yao. Wasomi kichomi.

Majuzi Naibu Waziri wa Viwanda, Injinia Stella Manyanya alipiga goti kwenye mvua kuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa asaidie umeme ufike kwao Nyasa. Huyu ni msomi wa daraja la juu, mzoefu kwenye chama na serikali. Hebu mtafakari kidogo.

Ina maana hajui Sera za chama kuhusu maendeleo vijijini? Kupeleka umeme sehemu mpaka Waziri Mkuu apigiwe goti? Wananchi nao masikini wakashangilia kwa nguvu. Ni wajibu wa serikali, na yeye kama Naibu Waziri alitakiwa amweleze kwa niaba yao. Magoti ya nini wakati ni haki na wanalipa kodi?