Baada ya miaka minane, babu wa Loliondo bado aendelea kutoa kikombe

Ni miaka minane sasa tangu Serikali ilipotangaza kuwa inaifanyia utafiti dawa ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile, maarufu kwa jina la “Babu wa Loliondo”, dawa iliyovuta watu kutoka kila kona ya nchi hadi Samunge mkoani Arusha, lakini ikapoteza umaarufu baada ya miezi sita.

Iliaminika kuwa kikombe kimoja cha dawa hiyo iliyotokana na kuchemsha aina ya mti unaopatikana Samunge, kilitosha kutibu ugonjwa wowote ambao muhitaji alikuwa nao, na ingawa wengi walitoa ushuhuda wa kuponywa na dawa hiyo, hakukuwepo na ushahidi wowote wa kisayansi kuthibitisha ufanisi wake.

Vifo vya watu vilivyofuata baadaye vikiaminika kuwa vilitokana na baadhi ya wagonjwa wa Ukimwi kuacha kutumia dawa za kufubaza Virusi vyaUkimwi, vilianza kupoteza matumaini ya watu kwa dawa hiyo.

Kilichofuata ilikuwa ni kupungua kwa misururu mirefu ya magari yaliyobeba watu wa kawaida, viongozi, raia wa kigeni na wengine kuelekea Samunge kwa Babu.

Lakini Mchungaji Mwasapila, ambaye katika mahojiano na vyombo vya habari baadaye alisema alinunua magari kutokana na mafanikio ya dawa yake, hakuacha huduma hiyo.

Miaka minane baadaye, mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) anasema bado anaendelea na tiba hiyo na kwa siku anatoa huduma kwa watu hadi kumi, akiwauzia kikombe kimoja kwa bei ileile ya Sh500, bei ambayo anadai alipewa na Mungu na kwamba gharama za usafiri kuifuata ni za mgonjwa.

Alianza kutoa huduma hiyo iliyojulikana ‘kikombe cha babu’ mwaka 2010 na mwaka 2011 ilipata umaarufu kiasi cha maelfu ya watu walimiminika katika Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro.

Watu maarufu, wafanyabiashara na viongozi wa siasa na Serikali kutoka ndani na nje ya Tanzania walimiminika Samunge kupata ‘kikombe cha babu.’

Msongamano wa watu waliokuwa wakienda Samunge, foleni ya magari barabarani na foleni ya waliokuwa wakisubiri kunywa dawa kuliifanya Serikali kushtuka na kuamua kuchunguza usalama wa dawa hiyo kwa afya ya binadamu na kama inatibu.

Wizara ya Afya iliunda timu ya wataalamu kutoka taasisi nne za Mamlaka ya Chakula na Dawa (kwa sasa inaitwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba-TMDA), Taasisi ya Utafiti wa Dawa Asili ya Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Jopo hilo lililokwenda Samunge Machi 2011, lilitangaza matokeo mwaka huo limeridhika kuwa kipimo cha kikombe anachotumia Mchungaji Mwasapila hakina madhara yanayotambulika kwa matumizi ya binadamu.

“ Kwa hatua tuliyofikia na taarifa tulizonazo za dawa hii mpaka sasa, tumeandaa na tunakamilisha taratibu, ili tuweze kufuatilia maendeleo ya kiafya ya wagonjwa 200,” inasema taarifa ya jopo hilo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa wagonjwa hao walikubali kushiriki katika utafiti huo, ili kuona maendeleo yao kiafya, baada ya kunywa dawa na kwamba utafiti huo unafuata vigezo vyote vya kitaifa na kimataifa.

“Pia tumeweka utaratibu madhubuti wa kufuatilia matumizi ya mti huu, kama “mmea tiba”, katika sehemu nyingine za nchi yetu, kwa kuwa tuna taarifa kuwa makabila mbalimbali yamekuwa yakitumia mti huu kama tiba. Makabila hayo ni pamoja na; Wagogo, Wamasai, Wabarbaig na Wasonjo kule Samunge.”

Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi hakuwa tayari kuzungumzia maendeleo ya ufuatiliaji wa dawa hiyo, akisema ni miaka mingi imepita.

Si Waziri wa Afya wala Naibu Waziri waliopatikana kuzungumzia suala hilo.

Kauli ya Babu

Lakini huduma ya Mwasapile kijijini Samunge inaendelea japo si kwa kasi kama ile ya mwaka 2011 na mchungaji huyo anasema jitihada hizo za kuiingiza mabara kuipima hazitafanikiwa.

“Dawa yangu haiwezi kupimwa maabara kwa sababu ni wito niliotumwa na Mungu kwa kunionyesha mti wa mrizariza,” alisema Mchungaji Mwasapile wakati Mwananchi ilipomtembelea kijijini kwake wiki iliyopita.

Anasema maagizo aliyopewa na Mungu ni kutibu watu akiwa Samunge na asiondoke kwenda sehemu nyingine zaidi ya hapo.

Anasema kabla ya kuwapa wagonjwa, huwa anaiombea dawa hiyo kwanza na kwamba kwa kuwa magonjwa yote yanaletwa na Mungu na dawa hiyo inatibu magonjwa yote, lakini anatahadharisha kuwa mgonjwa anayetumia dawa za hospitali hatakiwi kuacha.

Babu anasema kupungua kwa wagonjwa nyumbani kwake kumesababishwa na uzushi kwamba amefariki dunia na uzushi huo alidai ulienezwa katika nchi za Kenya na Uganda.

“Kutokana na uzushi huo, hivi sasa kwa siku napata wastani wa wagonjwa wasiozidi kumi. Naamini iko siku idadi itaongezeka,” alisema mchungaji huyo.

Siku hiyo muda wa saa 11:00 jioni kulikuwa na watu watano wakisubiri kunywa dawa.

Kuhusu kusajili dawa yake kama sheria ya tiba asili inavyoelekeza, Mwasapile alisema hawezi kusajili dawa yake kwa kuwa anachofanya ni kutekeleza maagizo ya Mungu.

Hata hivyo, Wizara ya Afya imekuwa ikihimiza umuhimu wa kuboresha dawa asili ili zianze kutengenezwa viwandani,

Agosti mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yaliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwahimiza waganga wa jadi umuhimu wa kuboresha dawa zao na zitengenezwe viwandani.

“Ni ukweli usiopingika kuwa dawa nyingi za kisasa hutengenezwa kutokana na mitidawa, elimu ya mwanzo kabisa ya matumizi ya miti hiyo kutumika kama dawa inatokana na waganga wa tiba asili,” alisema.

“Tanzania ina rasilimali kubwa ya mitidawa na wapo waganga wenye ujuzi katika hilo. Hivyo basi, ni vyema wataalamu wa tiba ya kisasa na waganga wa tiba asili mshirikiana kwa lengo la kuboresha na kuendeleza huduma na dawa za tiba asili.”

Mazingira ya kijijini

Kijiji cha Samunge kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 200 kwa barabara kutokea Mto wa Mbu na zaidi ya kilomita 70 kutoka makao makuu ya halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, kina mawasiliano ya simu na umeme.
Nyumba zake nyingi ni za kizamani ila katika mji wa Babu kuna jengo la matofali ya kuchoma ambalo halijakamilika.
Pia, kuna magari manne anayoyamiliki, malori matatu na gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser.

Jiko analotumia kuchemshia dawa limejengwa kwa mifuko kama ile inayotumika kuwekea mbolea na kuna kibanda cha udongo.
Sehemu ya wageni ni ndogo ambayo imewekwa mifuko ya kama ya mbolea kwa ajili ya kivuli.