Baadhi ya mazuri niliyojifunza Uzunguni

Sunday November 18 2018Freddy Macha

Freddy Macha 

Jingine muhimu nililojifunza ni kuwaelewa Wazungu. Zamani nikikua, Mzungu alikuwa mithili ya sinema. Kiumbe wa sayari nyingine. Yote mazuri. Mweupe kama Mzungu. Nimeishi nao miongo mingi. Kwa kila aina ya mitego na njia. Ni wanadamu tu...

Miezi kadhaa iliyopita nilikuwa nikisafiri kwa gari moshi.

Matreni Majuu huenda kasi na ni usafiri mzuri kuzidi magari na ndege. Si aghali; tena salama zaidi.

Safari ya saa tano kwa gari yaweza kuwa saa mbili tu kwa treni la kasi.

Gari moshi lilijaa sana. Ilikuwa Jumapili jioni. Kila mtu anarejea nyumbani baada ya mapumziko ya wikiendi. Kituo cha tatu baada ya safari, akapanda mama mmoja na mwanae. Mvulana. Nilimkisia miaka kumi. Akiburuta sanduku. Mama alimfuata nyuma akimpa “ndogo ndogo.” Hata kama hukuwasikiliza ulihisi pana kasheshe ya chini chini....

Hapakuwa na nafasi ya kukaa. Ikabidi mama na mvulana wasimame ukumbini kuelekea kijimkahawa ndani ya mashine hii iendayo kasi mali ya tajiri maarufu Richard Branson.

Baada ya vituo viwili, vitatu, pale nilipokaa palipatikana nafasi baada ya abiria wawili kushuka. NIkawaashiria mtu na mwanae waje. Mtoto akaburuta sanduku, akiangaliwa kwa ukali na mama. Mtoto akauliza aweke wapi sanduku.

Mama akapiga kite kama akichushwa.

Nikamwonesha mtoto mahali pa kuliweka sanduku.

Wakakaa.

Mama akasema ahsante.

Mtoto akachomoa simu. Sasa anadonoa donoa na kuigusa gusa.

Baada ya sekunde chache tu, nikaisikia harufu kali ikitapakaa. Haikuwa vigumu kuing’amua. Mama alikuwa kauchapa sawasawa. Macho yamelegealegea. Kila mara akishusha pumzi ni kama tarumbeta. Mara aegemee kiti, mara ajinyoshe, au kuinama mbele kumkazia macho mwanae.

“Uko sawa, Robert?” .

Mtoto akaitikia kwa kichwa bila kusema. Bado akiikagua simu yake.

Kando kando kila abiria na lwake. Wengi katika simu zao, kama ilivyo desturi miaka hii.

Punde Robert akanyanyuka.

“Unakwenda wapi?”

“Msalani.”

Ikabidi nisimame kumpisha bwa’ mdogo.

“Jamani samahani. Anasumbua sana.”

Nikamwambia mama asijali. Nimeshalea. Watoto huwa na haja zisizo simile.

Mzazi akatabasamu.

Kitambo kidogo mvulana akarudi.

Akarejea katika simu yake. Gari moshi hilo na njia. Muda ukaenda weeee. Mara...

“Mama.”

Mzazi akang’atuka usingizini.

“N’na kiu.”

“Tukifika London , tutanunua maji.”

“Mama siwezi kusubiri hadi London.”

Mama akaniangalia miye kama kudai kero imefikia mipaka sasa.

“Haya...basi.”

Mama akachopoa pochi. Akampa mtoto kadi ya benki. Mtoto akaenda zake kununua maji.

“Na wewe unataka?” mama akaniuliza. Nikasema ahsante n’nayo maji.

Itaendelea............

Wakati kijana kaondoka, mama akapiga kwikwi. Akanitazama weee.

“Vipi uko sawa?”

Mama akasema hakuna noma.

Robert aliporudi na maji, akamrudishia mamake kadi na kuanza kunywa..

Akaendelea kuchezea simu.

Mara mama kapiga kelele.Kisha akajirudi.

“Mama! Acha!” Mtoto akamwonya kwa kunong’oneza.

Kifupi mama alikuwa chakari.

Akasinzia.

Gari moshi na njia.

Hazikupita hata dakika tano.

“Nimechoka kweli. Robert jamani, nimechoka. Tukifika tu ntalala fofofo.”

Baada ya muda gari moshi likatua London.

Advertisement