Baraka Magufuli; Kutoka kijiji cha Bwanzi mpaka 'viunga vya Ikulu'

Aina yake ya ucheshi na mavazi yamewafanya mashabiki wambatize jina la Baraka Magufuli lakini jina lake halisi ni Baraka Mwakipesile. Alizaliwa miaka 21 iliyopita mjini Mafinga wilayani Mufindi, lakini kwa sasa anaishi kijiji cha Bwanzi wilayani humo mkoani Iringa.

Video yake akifanya ucheshi kumuigiza Rais John Magufuli katika mahafali ya Shule ya Sekondari Mdabulwa ndiyo iliyobadilisha maisha yake.

Akiwa amevalia kofia ya kijani na tai ndefu alimuigiza Rais Magufuli huku nyuma yake akiwa amesimama mtu mfano wa mlinzi akiwa na kofia aina ya bareti nyekundu.

Baraka anasema siku hiyo alilazimika kuomba ruhusa kwa bosi wake ili aweze kwenda kutumbuiza.

Lakini kwa kuwa alipanga kumuigiza Rais, aliona ni vyema awe na mlinzi na hapo wazo la kumuomba mfanyakazi mwenzake huyo ampige tafu lilikuja. “Nilimuona kijana yule anayeonakana nyuma yangu katika video ile anisaidie, kwa bahati nzuri alikubali na kwa kutumia usafiri wa baiskeli tulikwenda kuifanya kazi hiyo,” anasema Baraka.

Anasema hakujua kama alirekodiwa wakati akifanya ucheshi huo, lakini anamshukuru aliyefanya hivyo kwamba ndiye aliyemfungulia njia.

Kwake bado ni muujiza hasa baada ya Rais Magufuli kumtambulisha mwenyewe akitaka amuigize.

“Kwa kijana niliyekulia kijijini, televisheni na simu za kisasa ninaziona tu kwa watu, huu kwangu ni muujiza lakini nashukuru Mungu kwa umaarufu nilioupata.”

Alianzaje kumfuatilia Rais Magufuli?

Anasema amekuwa akivutiwa na Rais Magufuli tangu alipokuwa Waziri wa Mifugo, namna alivyokuwa akitamka takwimu za samaki katika Ziwa Victoria.

“Nilikuwa nikivutiwa na uzungumzaji wake. Katika hali isiyotarajiwa nilijikuta tu namuigiza uongeaji wake,” anasema.

Kazi ya sanaa

Anasema kazi ya sanaa aliianza tangu mwaka 2016. “Tofauti na sasa hivi wakati huo nilikuwa nikiifanya bure kwa kupita katika hafla mbalimbali kwa kuomba kuonyesha kipaji changu,” anasema.

“Moja ya hafla hizo ni pamoja na harusi, mahafali ya shule na matamasha yanayofanyika kijijini kwetu kwa kumuomba mshereshaji nafasi na kila nipoigiza natunzwa fedha ambazo zilikuwa zikinisaidia mimi na familia yangu.”

Kupitia huko ndiko watu wanachukua video na kuzirusha katika mitandao na hapo ndipo ikawa mwanzo wa kuanza kujulikana, na video iliyompa umaarufu zaidi ni ile aliyokuwa katika mahafali shule ya Sekondari Mdabulo.

Mafanikio aliyopata

Anasema, “sasa hivi kwa kweli nafanya kazi hadi niitwe na wahusika, kwani hata siku niliyokutana na Rais nilikuwa nimealikwa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mufindi, Netho Ndilito na kuwekwa katika ratiba ya kuburudisha.”

Anasema, kwa bahati mbaya ratiba hiyo ya Rais ilivurugika, kwani awali ilipangwa ahutubie uwanjani lakini ikabadilishwa akahutubia stendi akiwa anapita.

“Na wakati huo nami nilikuwa mbele ndipo hapo akaniita. Pia, kumekuwepo na simu nyingi nikipigiwa za shoo, jambo lililonilazimu kuwa na meneja ambaye ananimpangia ratiba na Mei mwanzoni natarajiwa kuwa Sumbawanga.”

Mafanikio mengine aliyoyapata ni heshima kuongezeka.

“Na napata thamani kwani sikuwahi kufikiria kufikia katika ofisi za gazeti la Mwananchi kuhojiwa.”

Kazi nyingine

Anasema mbali ya kuigiza anafanya kibarua katika kiwanda cha Mufindi Tea and Cofee wilayani Mufindi.

“Hata siku ambayo nimeonekana kwa Rais nilikuwa nimeombewa ruhusa kwa meneja wangu wa kazi anayeitwa Hekima Sanga na mkurugenzi wa Halmashauri ya Mufindi, Ndilito ambaye ndiye alinialika katika tukio hilo,” anasema.

Kuhusu kumuigiza Rais Magufuli anasema, “sitaacha kisa tu atakuwa kamaliza muda wake wa uongozi, mbona wasanii kama Steve Nyerere hadi leo akisimama na kuongea sauti ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere watu wanacheka na kufurahi.”

“Vilevile kwa Mr. JK naye hivyohivyo hayupo madarakani, lakini msanii huyo akimuigiza watu wanavunjika mbavu kwa kucheka jambo linaloonyesha ni namna gani Watanzania wanapenda kusikia sauti za viongozi wao mara kwa mara.