Basata hawajui Rose Mhando anafanya nini Kenya

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limesema linapata ukakasi kufuatilia sakata la kuumwa kwa msanii wa muziki wa Injili, Rose Mhando kwa kuwa hadi sasa hakuna taarifa sahihi zinazoeleza Rose yupo wapi , anafanya nini na aliondokaje nchini.

Hivi karibuni msanii huyo alionekana katika video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonyesha akiwa anaombewa katika moja ya kanisa nchini Kenya, huku akiwa ameungua vidole vya mikono.

Akilizungumzia hilo, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema imewawia vigumu kumfuatilia msanii huyo kwa sababu hawajui hata aliondoka kwenda huko kwa shughuli gani.

Badala yake Mngereza alisema kumekuwa na watu tofauti tofauti wakijitokeza na kudai ni wasemaji wa msanii huyo jambo ambalo linawawia vigumu wamuamini nani ukizingatia kuwa hawajui aliondokaje na hawajawahi kumpa kibali cha kwenda huko.

“Inawezekana watu wakaanza kutulaumu kwa nini hatumfuatilii msanii huyu, lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kukurupuka bila kujua aliondokaje hapa nchini, kama alienda kwa shughuli zake binafsi tutajuaje ?

“Ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza mara kwa mara wasanii ni vema wanaposafiri kupitia kwetu kupata kibali ili hata wanapopatwa na tatizo iwe rahisi kujua wapi pa kuanzia japokuwa hii haina maana hatutamfutilia kwani tutafanya hivyo pale tutakapopata taarifa sahihi kwa watu sahihi, ”alisema katibu huyo.

Rose ni kati ya wasanii walioleta mapinduzi katika muziki wa injili ikiwamo kupendwa na watu wa madhehebu mbalimbali na vibao vyake kama ‘Nibebe’, ‘Pindo la Yesu’ na ‘Utamu wa Yesu’ vikitamba na kumpa umaarufu.