Bashe ameingia mitini na hoja yake ya utekaji, demokrasia

Sunday November 25 2018

Mbunge wa Nzega kupitia CCM,Hussein 

Mbunge wa Nzega kupitia CCM,Hussein  Bashe.Picha ya Maktaba 

By Luqman Maloto

Mwandishi wa habari aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, ametimiza mwaka mmoja tangu alipotoweka Novemba 21. Dhana kubwa ya kutoweka kwake ni ile inayosema alitekwa na watu wasiojulikana.

Kada wa Chadema, Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, pia ametimiza miaka miwili tangu alipotoweka. Nadharia yenye nguvu kuhusu kutoweka kwake ni kwamba alitekwa na watu wasiojulikana.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye, ametimiza mwaka mmoja na miezi minne, tangu alipochukuliwa nyumbani kwake Julai mwaka jana. Ipo wazi kuwa watu waliomchukua Kanguye na kuondoka naye mpaka leo ni jamii ya watu wasiojulikana.

Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini alipigwa risasi na kufariki dunia Februari 16, mwaka huu, alipokuwa kwenye daladala, wakati polisi walipokuwa wakiwadhibiti viongozi na wafuasi wa Chadema waliokuwa wakielekea kwenye ofisi za Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni kudai barua za utambulisho wa mawakala.

Chadema walikuwa wakilalamikia kuchelewa kupewa hati za viapo na barua za utambulisho kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Kinondoni uliofanyika Februari 17, mwaka huu.

Vilevile ziliokotwa maiti nyingi kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na Mto Ruvu. Mpaka leo hakujawa na maelezo wale waliokufa ni akina nani, sababu ya vifo vyao na akina nani walio nyuma ya vifo hivyo. Ni sawa kusema waliookotwa wamekufa ni watu wasiojulikana, kama vifo vyao vilitokana na mkono wa mtu, basi waliowaua nao ni watu wasiojulikana na wamekufa kwa sababu isiyojulikana.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alipigwa risasi nyingi Septemba 7, mwaka jana, mchana kweupe, alipokuwa anawasili nyumbani kwake Dodoma, baada ya kumaliza kikao cha asubuhi bungeni. Ni mwaka mmoja na zaidi ya miezi miwili sasa tangu tukio hilo lilipotokea.

Watu waliomshambulia Lissu hawajakamatwa na hawajajulikana. Lissu yupo Ubelgiji akiendelea na matibabu. Polisi Tanzania wanasubiri Lissu na dereva wake warejee nchini ndiyo wawahoji. Dereva pia yupo Ubelgiji. Mwaka mmoja na zaidi ya miezi miwili imepita, polisi wanasubiri Lissu na dereva wake warejee ndipo ama wakamilishe au waanze upelelezi.

Hivi karibuni mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’, alitekwa na kushikiliwa kwa siku nane. Waliomteka ni watu wasiojulikana. Kutekwa hadi kuachiwa kwake ni mchoro usioeleweka. Inasikitisha na inaudhi jinsi Watanzania wanavyochezewa utadhani wapo kwenye mchezo wa mazingaombwe. Hata hivyo, mwisho kabisa, waliomteka MO ni watu wasiojulikana.

Mwanamuziki wa Hip Hop, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu, walitekwa mwaka jana. Walishikiliwa kwa siku tatu kabla ya kuachiwa. Waliowateka kisha kwenda kuwatelekeza ufukwe wa Bahari ya Hindi, Ununio, Dar es Salaam, bado hawajulikani.

Ukimya wa Bunge

Niliwahi kuandika kwamba mfululizo huo wa matukio, unatosha kulifanya Bunge kutikisika kwa ama hoja nzito kuwasilishwa na kujadiliwa au kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa matukio yote ambayo yametajwa. Hata hivyo, Bunge bado halijatekeleza hilo.

Mara kadhaa wabunge wamejitahidi kusema bungeni na kuomba angalau muda mfupi wa Bunge ili kusitisha hoja nyingine na kujadili masuala hayo yenye kugusa usalama wa wananchi. Mara zote mipango hiyo imekuwa ikikwama kwa sababu kiti cha Spika hakijawahi kuruhusu.

Aprili mwaka jana, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alikiomba kiti cha Spika, kilichokuwa kimekaliwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa Bunge liridhie kusitisha shughuli nyingine na kujadili kadhia hiyo ya upoteaji, utekwaji na mauaji ya watu. Hoja hiyo ilikataliwa.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alizungumza kwa hisia bungeni hadi kutoa machozi, kwamba hata yeye amewahi kutekwa na kudhalilishwa.

Pamoja na kilio hicho ambacho kiliambatana na tuhuma kwa maofisa usalama kuhusika na utekaji, hoja hiyo haikupewa nafasi bungeni.

Swali; kwanini bunge la wananchi linanyamazia haya hadi linashindwa hata kuunda kamati ya kibunge ili isaidie kuwapa majibu wananchi juu ya mfululizo huo wa matukio yenye kuogofya? Mpaka leo wananchi hawajui nini kimetokea Kibiti, Rufiji na Mkuranga, mauaji yaliyotokea, chanzo chake na wahusika ni akina nani?

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara ‘Bwege’, amewahi kuzungumza bungeni kuwa polisi walivamia mpaka misikiti jimboni kwake, wakawapiga risasi waumini, wengine walikufa na wapo ambao walichukuliwa lakini hawakuwa wamerudishwa mpaka siku alipozungumza. Hoja ya Bwege haikulifanya Bunge lione uzito wa kujadili.

Hoja ya Bashe

Bashe, alizungumza na vyombo vya habari mapema mwaka huu kuwa angewasilisha bungeni hoja binafsi ili Bunge liunde kamati maalumu ya kuchunguza vitendo vya utekwaji, mauaji, ukiukwaji wa haki za binadamu na demokrasia.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alijibu akisema Bashe alikuwa anababaisha tu wananchi, kwa sababu hana hoja. Alieleza kuwa hoja ya Bashe inapaswa kuanzia ndani ya kambi ya wabunge wa chama chake (CCM) ili iungwe mkono ndipo iwasilishwe bungeni.

Baada ya hapo Bashe amekuwa kimya. Swali ni je, Bashe aliogopa kuwasilisha hoja hiyo ndani ya kambi ya chama chake? Au aliwasilisha ikakosa uungwaji mkono?

Kama hoja hiyo haikuungwa mkono na wabunge wa CCM hicho ni kituko cha kiasi gani? Au Bashe ameamua kuingia mitini na hoja yake baada ya maelezo ya Spika Ndugai?

Advertisement