UCHAMBUZI: Bila fikra mpya vichwani mwetu tunatwanga maji

Wednesday March 13 2019

 

By Padri Privatus Karugendo

Nina imani kubwa kwamba hata mimi na wewe tukiingia madarakani hatutafanya tofauti. Maana yake ni kwamba Watanzania wote ni wale wale.

Utamaduni wa kukataa kukubali ukweli na kutafuta mchawi ni wa “Kitanzania” Wale ambao hawajaingia kwenye mfumo wa “Kitanzania” ni watoto wadogo na wengine hawajaota meno. Wengine ambao tumeishi na kuziishi serikali za awamu nne, hatuna jipya.

Hii haina maana kwamba tukate tamaa na tusifanye kitu. Hapana. Kukata tamaa ni dhambi kubwa. Ni bora kuendelea kupambana kwa nia na malengo ya kutoa mchango wetu katika hali yetu.

Na tuache tabia ya kumtafuta mchawi nje ya taifa letu. Ni upuuzi kukataa kuuona ukweli wa yanayotokea na kusukuma lawama nje ya nchi. Ni lazima kukubaliana na hali yenyewe.

Hivi mimi au wewe tukishika madaraka tutapata wapi mbinu za kumaliza rushwa ya Tanzania? Kama sisi hatupokei rushwa, shangazi, mjomba, kaka, baba, mama au rafiki wanapokea. Kwa njia moja au nyingine, na sisi tunapokea rushwa.

Mimi ninaliangalia suala la rushwa kwa njia hii. Kwa njia moja ama nyingine sote tunashiriki kwenye rushwa. Ndugu yako anapokuchangia Sh1 milioni wakati mtoto wako anaoa, kama unaujua mshahara wa ndugu yako ni laki mbili na wewe ukaipokea, si unashiriki rushwa? Kapata wapi hiyo milioni.

Bila kuwa na mfumo wa kubadilisha fikra za watu, hata ingeingia serikali ya malaika aliyeshuka kutoka mbinguni, ni lazima watu wataendelea kula rushwa, kuiba na kuiuza nchi yao.

Ninakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere, ya “tumepumbazwa kiasi cha kutosha, tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha na tumenyonywa kiasi cha kutosha.”

Alijitahidi kupambana na unyonge wetu. Na kwa kufanikisha hili alikazania elimu iliyokuwa imeundwa chini ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Elimu hiyo ililenga kukomboa fikra ya Mtanzania hatua kwa hatua. Hayakuwa maneno matupu, ni mawazo yaliyokuwa na vitabu na yalikuwa na shule. Kivukoni, haikujengwa kwa bahati mbaya.

Bahati mbaya mpango wa Mwalimu haukukamilika. Athari za kutawaliwa zilikuwa kubwa kiasi kwamba alishindwa kabla ya kutukomboa.

Nchi zote zilizoendelea, zimeendelea kwa vile zinapenda nchi zao. Katika nchi hizi hakuna mtu anasomba pesa kutoka ndani ya nchi na kupeleka nje ya nchi.

Kinyume chake ndio kinafanyika, wanachota nje na kupeleka ndani. Nchi zote zilizoendelea, watu hawakukimbia na kuzamia kwenye nchi nyingine. Walitafuta elimu na pesa na kurudi kwenye nchi zao.

Panahitajika shule za mawazo za kila chama cha siasa. Panahitajika vitabu vinavyoelezea sera na malengo ya vyama siasa. Hoja yangu imelala hapo. Badala ya kupiga kelele kumlalamikia JPM, tuonyeshe mifumo tuliyonayo ya kubadilisha fikra za watu.

Kula rushwa, kushindwa uzalendo, kuiuza nchi, ni ugonjwa wa akili. Mtu anakuwa na matatizo kichwani. Ili kuondoa matatizo hayo ni lazima kuwa na dawa. Na dawa ya akili, ni kuilisha akili fikra pevu zenye ukombozi wa kifikra.

Huwezi kubadilisha fikra kwa risasi na maguvu ya polisi wala jeshi. Huwezi kubadilisha fikra kwa kupambana na wananchi bali kuleta fikra pevu.

Padre Privatus Karugendo

+255754633122

Advertisement