Bob Rudala aibukia kwa Jhikoman

Saturday March 9 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Ni dansi gani la wanandoa ambalo halikutumia wimbo Nimekuchagua Wewe kati ya mwaka 2004 - 2010. Ni miongoni mwa nyimbo maarufu zilizotumika katika ufunguzi wa dansi la harusi.

Ni fursa aliyoiona iliyompa matunda tarajiwa kwani kwa wakati huo nyimbo nyingi zilizotumika katika ufunguzi wa dansi za harusi zilikuwa za Kizungu kama vile ‘I will Always Love You wa Whitney Houston, From This Moment (Shania Twain) au At Last (Etta James).

“Kilichonisukuma kuandika wimbo huu ni uhitaji na kusema ukweli Mungu alijibu maombi kwani ulipendwa sana na nina furaha kuwa miongoni mwa watu nilioleta mapinduzi,” anasema Bob Rudala.

Yupo wapi sasa?

“Siwezi kusema nipo wapi kwa kuwa ninazunguka duniani nikifanya kazi ninayoipenda ambayo ni muziki,” anasema.

Akiwa na Vipaji Band yenye wasanii saba, hupiga muziki nchi mbalimbali duniani na ndiyo sababu ya kupotea kwake nchini.

Anamtaja Winston Ludo mwenye asili ya Zimbabwe kuwa ndiye anayesimamia kazi zake kwa kuwatafutia matamasha katika mataifa mbalimbali duniani.

“Tumefanya shoo katika nchi za Ujerumani, Ufaransa, Urusi, Hispania na kwingineko duniani. Muziki ndio maisha yetu na kusafiri imekuwa sehemu yake.”

Kuhusu lugha anasema muziki ni lugha inayotambulika na mataifa yote ndio maana wanamuziki kama Mbilia Bell, Olive Mtukudzi, wanaimba kikwao na wanakubalika duniani kote.

“Muziki ni hisia tu kwa hiyo unaweza kuimba lugha yoyote na ukaeleweka, sio lazima kuimba lugha fulani ili ukubalike. Unaweza kugusa hisia bila kuimba lugha wanayoielewa,” anasema.

Wimbo mpya na Jhikoman

Kimsingi siyo wimbo mpya ila ni Remix ya Nimekuchagua wewe ambao wamefanya katika mahadhi ya Afroreggae.

Kukamilisha kazi hiyo amemshirikisha mkaliw a reggae nchini, Jhikoman anayefanya kazi chini ya bendi ya Afrika Kabisa.

Video ya wimbo huo inapatikana katika mtandao wa Youtube.

Advertisement