Calisah: Bila Wema Sepetu nisingetoboa

Saturday February 9 2019

 

By Nasra Abdallah,Mwananchi

Mwaka jana ilikuwa ni bahati kwa upande wa Tanzania baada ya mwanamitindo maarufu nchini Calisah Abdulhamidu ’Calisah’ kuibuka mshindi katika mashindano ya Mr Afrika.

Katikashindano hilo lililofanyika, Desemba 2 mwaka jana, jijini Lagos nchini Nigeria, Calisah aliwabwaga washiriki wengine 22.

Anasema pamoja na kwamba alishapata mwaliko wa kushiriki mashindano hayo miaka miwili mfululizo, hakuweza kutokana na kutokuwa na mdhamini wa kumgharamia kusafiri hali iliyomlazimu kuuza gari ili kuifanikisha.

“Nakumbuka mwaka juzi lilifanyika nchini Marekani, na mwaka jana Nigeria, na yote nilipata mualiko lakini nilishindwa kwa kuwa unatakiwa ujigharamie na mimi sikuwa na fedha.

“Lakini mwaka huu nilipopata mwaliko tena, nilisema nitapambana kufa kupona, kwani baada ya kuzunguka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kuomba msaada wao nilikwama.

“Mwisho wa siku niliamua niuze gari langu ili kupata nauli kwani baadhi ya watu huwezi kuwafikia zaidi wanaweza kukubeza kwa kulinganisha umaarufu ulio nao na kukuona kuwa umekuwa ombaomba,” anasema.

Historia yake

Calisah kabla ya kuingia katika fani ya uanamitindo miaka mitano iliyopita, alikuwa modo wa maduka, yaani wale wanaume wanaovaa nguo nzuri na kukaa nje ya maduka ya nguo Kariakoo kama njia mojawapo ya kuwavutia wateja.

Kazi hiyo anasema alikuwa akiifanya huku akiwa anasoma sekondari, ambapo ilimwezesha kujilipia ada na kumlea bibi yake ambaye walikuwa wakiishi naye baada ya baba yake kumtimua nyumbani kwa makosa ambayo anadai alibambikiziwa na mama yake wa kufikia.

Mazingira hayo magumu ya maisha, anasema ndio yaliyochangia kutofanya vizuri katika mtihani wake wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Temeke.

Ilibidi arudi Kariakoo na kufanya kazi ya kuuza nguo, lakini baada ya kuona haina maslahi aliamua kwenda kusoma masuala ya usanifu kurasa na kupata kazi katika kampuni inayojishughulisha na kutengeneza filamu na kazi za muziki.

“Kama unavyojua mtafutaji hachoki, huku nako nilipoona mambo hayaendi sawa, nikaamua kujiajiri katika kutengeneza cover za filamu mwenyewe,” anasema.

Anasema baadaye alikutana na mbunifu wa nguo, Martin Kadinda, ambaye alimuona ana sifa za kuwa mwanamitindo na ndipo hapo akamkutanisha na waandaaji mbalimbali wa maonyesho ya nguo na safari yake ikaanzia hapo.

Katika shughuli hizo za kupanda jukwaani na kuonyesha mavazi anasema kwamba ndipo akajikuta akikutana pia na mrembo Wema Sepetu.

Calisah anasema mrembo huyo aliwahi kukutana naye katika maonyesho ya mavazi zaidi ya mara tisa na mwaka 2016 kujikuta wanaanzisha urafiki ambao uliendelea hadi wakawa wapenzi.

Anakiri kwamba katika mafanikio aliyonayo leo, Wema ana mchango mkubwa kwani alimkutanisha na watu mbalimbali.

Wakati kuhusu tukio la picha zao za faragha zilizosambaa anasema ilikuwa ni katika njia ya kutafuta kutoka wakati ule japokuwa anajutia, kwani amejifunza unaweza kutoka hata bila ‘kick’.

Hata hivyo anasema anachoshukuru pamoja na yaliyotokea waliyamaliza na yeye na Wema kwa sasa ni marafiki.

Akimzungumzia kuwa ni mwanamke wa aina gani, anasema Wema ni mchapakazi, ana huruma na ana nyota kali ambayo karibu kil mwanaume anayekuwa naye hufanikiwa.

Anaongeza kuwa anashukuru kwa hatua aliyofikia na kueleza kuwa anaamini mpaka sasa yeye ndiye mwanamitindo anayelipwa pesa ndefu hapa nchini.

Matarajio yake

Katika matarajio yake Calisah anasema ni kuwa na bidhaa zake na kwa kuanzia atakuwa na maji ambayo yanaongeza nguvu kwenye mwili, sidiria na boxer za kike na za kiume zitakazokuwa na jina lake.

Pia ana mpango wa kuanzisha taasisi ya kuzalisha wanamitindo wengine vijana hususani kwa wale wanaopenda kazi hiyo kutoka moyoni.

“Maji yamekuwa mengi na yanaendelea kuzalishwa kila uchwao, lakini mimi nimeona nije na maji ambayo yatakuwa na kitu ndani yake kwa afya ya binadamu,” anasema Calisah.

Advertisement