Chama aeleza matukio ya ushirikina Yanga-2

Wiki iliyopita tulipata simulizi ya kusisimua ya aliyekuwa beki kiraka aliyetamba katika klabu mbalimbali za soka nchini wakati huo Ligi Kuu Tanzania Bara ikiitwa Daraja la Kwanza, Rashid Idd ‘Chama’.

Katika maelezo yake na gazeti hili, Chama alifunguka mambo mengi ikiwemo asili ya jina Chama na alivyopitia kipindi kigumu katika klabu ya Yanga kabla ya kuzitumikia kwa nyakati tofauti Majimaji, Pamba, Ndovu na Taifa Stars.

Sehemu iliyopita tuliona namna Chama alivyorejea Yanga akitokea Pan Africans alikocheza kwa muda mfupi ambako alikutana na changamoto ya kupata namba katiika kikosi cha kwanza.

Itakumbukwa katika kikosi hicho ndipo Yanga iliunda ngome imara katika safu ya ulinzi ambayo ilipachikwa jina la ukuta wa ‘Berlin’.

Ukuta wa Berlin ni maarufu duniani ulitenganisha sehemu mbili za Jiji la Berlin (Ujerumani) ukiwa na urefu wa kilomita 45.3.Ukuta wa Berlin ulikuwa mfano ulijulikana zaidi kwa jina la ‘pazia la chuma’ katika Ulaya lililotenganisha nchi za kikomunisti za Ulaya Mashariki na Magharibi.

Pamoja na changamoto ya kupata namba kikosi cha kwanza, Chama anakumbuka namna alivyokumbana na imani za ushirikina ndani ya klabu hiyo kongwe yenye maskani makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Ushirikina

Nguli huyo anakumbuka matukio mbalimbali ya imani za ushirikina yaliyofanywa na idadi kubwa ya viongozi wa klabu zilizokuwa zikishiriki mashindano hayo ikiwemo Yanga.

Moja ya matukio ya ushirikina anayokumbuka Chama ni mchezo baina yao na timu iliyokuwa tishio katika soka enzin hiyo ya RTC Kigoma iliyokuwa na mfungaji wake hatari Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’.

Makumbi alipachikwa jina la ‘Homa ya Jiji’ kutokana na umahiri wa kuzifunga mara kwa mara Simba na Yanga.

Chama anasema mwaka 1987 wakati wakijiandaa kucheza na RTC Kigoma, usiku wa manane akiwa wamelala na beki mwenzake Allan Shomari, walifuatwa na mchezaji wa timu hiyo (jina tunalo) aliyekwenda kuwaamsha. “Baada ya Kugongewa kwa muda mrefu, ndipo Shomari akanishauri tuamke na kwenda kumsikiliza kwa sababu itaonekana hatuna nidhamu, japo tulihisi kuna kitu cha tofauti kitakuwa kinaendelea nyuma ya pazia

“Baada ya kutoka nje tulimkuta mganga wa kienyeji na mayai yameandikwa kwa lugha ya kiarabu na wachezaji wamemzunguka, hapo nikapatwa na mshtuko, kasha nikawatazama wenzangu

“Tulipoona vile huku tukiwa na hasira ya usingizi tukachukua mayai kwa mganga na kuyapasua kisha kurudi ndani kulala, baada ya kuyavunja wachezaji wengine wakawa wanacheka, mganga kuona vile akaondoka kwa hasira tusijue wapi anakoelekea,” anasimulia Chama.

Anasema asubuhi viongozi wa Yanga walipata taarifa na walitoa taarifa kwa kocha Shabani Marijani asiwapange wakihofu huenda wana lengo la kuihujumu timu ili ifungwe lakini kocha aligoma.

“Kocha alishikilia msimamo wake kwamba lazima tucheze kwasababu tumefanya mazoezi wiki nzima kujiandaa na mchezo huo. Lakini baada ya mvutano kocha alikubali akapanga kikosi chake na Yanga tulishinda maboa 5-0,”anasema Chama.

Chama ambaye ameweka makazi yake mkoani Arusha, anasema mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Edgar Fongo aliyekuwa nyota wa mchezo baada ya kupiga ‘hat trick’ mabao matatu.

Baadhi ya wachezaji anaokumbuka walicheza mchezo huo ni kipa Joseph Fungo, Mohammed Mkweche, Omari Hussein, Charles Mkwasa, Juma Mkambi, Fongo na Shomari.

Mastaa

Chama anasema enzi zake soka ilichezwa kwa kiwango cha juu na ilikuwa ngumu kocha kupanga kikosi kwa kuwa kila mchezaji alikuwa na sifa ya kucheza kikosi cha kwanza.

Kocha huyo anakumbuka kwa uchache baadhi ya nyota aliocheza nao akina Juma Pondamali, Mohammed Mkweche, Kassim Manara, Mohammed ‘Adolf’ Rishard na Amri Salim.

Wengine ni Mohamedi Salim, Ahmed Amasha, Willy Kiango, Madaraka Selemani, Peter Tino, Octavian Mrope na Andrew Kabisama.

“Kipindi chetu ilikuwa ni vigumu kumtaja mchezaji bora kwenye timu ya Taifa kutokana na kuwepo kwa vipaji vingi ndio maana hata wachezaji kutoka mataifa ya nje walikuwa wachache tofauti na sasa.

“Ilikuwa mtu akiingia uwanjani hata uliyekaa nje unamkubali, akitoka anayeingia anaonekana mzuri zaidi ya yule aliyekuwa mwanzo. Hii ilitokana na mfumo wa michezo ulivyokuwa unaendeshwa hapa nchini kuanzia shuleni hadi klabu kubwa,” anasema Chama.

Chamaa anasema kilichongia kiwango cha soka kupanda ni uwepo kwa kampuni, mashirika, majeshi na wizara mbalimbali zilikuwa na timu za michezo yote jambo ambalo kila mtu alikuwa anafurahia mchezo kwa kuwa lilikuwa ni jambo la wito.

Katika muendelezo wa makala haya usikose kufuatilia namna Chama alivyoshiriki Fainali za Afcon mwaka 1980 nchini Nigeria.